Msemaji Kasema: ''Uongo Ukisemwa Sana Hugeuka Kuwa Kweli''

Msemaji Kasema: ''Uongo Ukisemwa Sana Hugeuka Kuwa Kweli''

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
Waswahili tuna msemo, ''Fumbo mfumbie mjinga mwerevu atatambua.''
Mimi nimelitambua fumbo na wapi limeelekezwa.

Tatizo ni historia ya uhuru wa Tanganyika.
Msemaji kaandika anasema:

UONGO UKISEMWA SANA HUGEUKA KUWA UKWELI

SEHEMU YA KWANZA

Mtanange wa leo hii ni kuhusu Harakati za Uhuru wetu kulingana na taarifa nyingi zinazosambaa mitandaoni, nasi tunazipokea kama zilivyo bila kujiuliza maswali magumu. Hivi katika taarifa zote hizi UKWELI ni upi? Na kwa nini tunazungumzia baadhi ya watu kuliko Falsafa ilopelekea madai ya Uhuru wetu. Je, dhamira yetu katika kujitawala ilikuwa kumuondoa Mkoloni mweupe na kumweka Mkoloni mwingine mweusi ama tulikuwa na malengo mengine kabisa hayakufikiwa?

TUMETOKA WAPI?
Nikiacha pembeni mapambano ya Makabila dhidi ya Wakoloni kama yale ya Abushiri, Wahehe na Wachagga na makablila ya kusini walopigana vita vya MajimajI maana maelezo yatakuwa marefu na hatukufanikiwa kwa hayo.

Bila shaka itapendeza zaidi nikijikita kwenye harakati za Uhuru wetu KITAIFA maana hapa kuna somo kubwa tumejifunza pale tuliposhindwa vita kutokana na kukosa Umoja wa pamoja Kitaifa kupambana na Ukoloni. Na tuliweza tu kufanikiwa pale tulipoungana sote kama Taifa moja, kwa nguvu ya pamoja kushinikiza Uhuru wa nchi yetu. Je, tuliwezaje kufikia haya?

WAZO – An Idea
Huwezi kuzungumzia Uhuru wa nchi za Kiafrika pasipo Kuuzungumzia Umoja wa Watu wenye asili ya Kiafrika walounda chombo cha kupigania haki zao kiitwa Pan African Association ( Pan – Africanism 1897). Umoja huo haukuwa kwa Afrika pekee kwa maana ya wakazi wa Afrika bali ulitanguliwa na falsafa ya Kujitambua Waafrika dhidi ya Ubaguzi wa rangi ya mtu mweusi katika tawala zote Duniani Umoja huo ndio haswa waasisi wa fikra, wazo na walowasha cheche za harakati katika Ukombozi wa bara la Afrika kupitia wasomi, Diaspora na vyama vya Watumishi wa Umma (Civil Servants).

Kwetu sisi, mara kwa mara nimesoma makala za baadhi ya waandishi wakibeza chama cha African Assocition ya Tanzania kilichoundwa mwaka 1929 kama kilikuwa ni kijiwe cha kahawa! Waandishi hawa wameshindwa kuumiza vichwa vyao kujiuliza mbona vijiwe vya kahawa vilikuwepo hata kabla ya kuundwa kwa chombo hiki? Na iweje vyombo kama hiki viundwe karibu nchi zote wanachama wa Pan African Association?

Kuna wengine wamediriki hata kusema chama hiki cha African Association Tanzania, kilikuwa chama cha Walevi kwa sababu Chama hicho kilikuwa na bendi ya muziki ikiitwa African Association jazz band bila kutambua kwamba muziki huwa na nyimbo ambazo hubeba ujumbe mzito kwa lugha ya jamii husika. Licha ya kwamba kama tulivyotoka kwenye vitabu, Magazeti na Radio kwenda komputa na luninga, mbona leo hii tunabeba simu za mitandao mpaka kwenye Ma-baa kwa malengo yale yale ya mawasiliano na hatujidharau kwa ulevi wetu!

MWANZO
Chama cha Watu weusi cha Pan African Association (Pan Africanism) kilizinduliwa rasmi mwaka 1897 huko Marekani na Diaspora kwa dhumuni la kupigania haki za watu weusi kote duniani kutokana na Waafrika kutengwa Kijamii, Kisiasa na Kiuchumi. Wakati ule Wakoloni hawakuruhusu watu weusi kuunda vyama vya Siasa wala kuunda taasisi yeyote ya kupigania haki Usawa na Uhuru wao. Watu weusi kote duniani walikuwa na changamoto sawa haijalishi waliishi nchi za nje ama ndani ya Afrika.

Hivyo, Mtazamo (envision) na maazimio (manifesto) ya Diaspora hao ilikuwa kuunda chombo cha Kijamii (Social Association) chenye dhamana ya kuunganisha (Unify) mataifa yote ya Afrika ambayo Waafrika kote duniani Wenye asili ya weusi (race) wataweza kujitambua kudai haki, Usawa na hata ikibidi warudi kwao Afrika na Kujitawala wenyewe ‘Back to Africa'

Hilo ndio chimbuko la Pan Africanism kifalsafa, hivyo wakaunda vyombo viwili muhimu sana 1. Jumuiya ya Waafrika (African Association) na 2. Baraza na Wawakilishi (Congress) ambalo kikao cha kwanza kabisa lilifanyika mwaka 1900 mjini London Uingereza. Kikao cha pili kilifanyika mjini Paris mwaka 1921, cha tatu London mwaka 1923, cha nne mwaka 1927 New York, Marekani na kikao cha tano mwaka 1945 kilikuwa Manchester, Uingereza. Vikao vyote hivi ni kabla ya Uhuru wa nchi za Kiafrika ukiacha Liberia na Ethiopia ambao tayari zilikwisha jitawala wakati wa kikao hiki cha tano mwaka 1945. Kikao hiki cha tanl ndicho kilichoshirikisha Wanaharakati Wengi kutoka bara la Afrika na inasadikiwa zaidi ya Wawakilishi 70 walihudhulia.

Hivyo basi hoja mtambuka ni kuzama zaidi katika kuutafuta Ukweli wote juu ya harakati za Uhuru wa nchi yetu na laiti Wazee wetu wangeweza kuweka kumbukumbu za historia yetu katika Maandishi na wazi zikifundishwa mashuleni na kuwekwa katika maktaba zetu, basi leo hii tusingekuwa na hadithi nyingi za Uongo na Ukweli juu ya harakati za Uhuru wetu kwa sababu wao walikuwa wasomi, walimu wetu na ndio wao waloshiriki kikamilifu katika harakati hizo chini ya mwamvuli wa Pan Africanism.

HARAKATI ZA KWANZA - Tanzania
Kuna kumbukumbu mbili kinzani juu ya Waasisi wa harakati za Uhuru toka kuanzishwa kwa African Association hapa Tanzania mwaka 1929. Na kwa bahati mbaya sana hakuna kiongozi wala mzee hata mmoja alojitokeza yeye binafsi kuuweka Ukweli ni upi na Uongo ni upi hali ambayo imezua mushkeri katika maktaba ya Habari na kumbukizi za harakati za Uhuru wa nchi yetu. Taarifa nyingi za watafiti ni habari zilizotokana na simulizi (hearsay) kutoka watu mbali mbali, kwa wakati tofauti lakini nazo hazijitoshelezi kwa sababu hazitoki katika maktaba ya chama isipokuwa habari za simulizi kuhadithiwa na watu binafsi.

Taarifa ya kwanza ni ile inayosema Chama cha African Association kilianzishwa na Ali Said na Ramadhan Ali (Wazaramo) wakiwa Wanachama wa chama cha awali cha Watumishi wa Umma -Tanganyika Territory African Civil Service Association (TTACS) kilichoasisiwa na Mzanzibar aitwaye Martin Kayamba mwaka 1922. Jina la Martin Kayamba ndilo linatajwa zaidi kuwa ndiye muasisi wa AA.

Hakuna taarifa zaidi ya shughuli na utekezaji wa chama hiki bara na visiwani chini ya Uongozi wa waasisi hawa isipokuwa maelezo ya jumla na kwa uchache yanayowahusu zaidi Watumishi wa Umma (Civil Servants).
Taarifa nyiingine ni ile tunayoifahamu wengi wetu ambayo tumeambiwa chama cha African Association kilianzishwa na Kleist Sykes mwaka 1929 baada ya kukutana na kushawishiwa na mwalimu James Aggrey Diaspora wa Marekani mwenye asili ya Ghana mwaka 1924. Kleist Sykes akiwa na wenzake Mzee bin Sudi, Cecil Matola, Suleiman Mjisu and Raikes Kusi (Watumishi wa Umma) waliunda chama hiki cha African Association na Cecil Matola mwenye asili ya Malawi akawa rais wa kwanza wa AA.

Japokuwa African Association hakikuwa chama rasmi cha Kisiasa nchini bali kupigania HAKI za Watumishi wa Umma kutokana na Ubaguzi wa rangi kama ilivyo ada ya Pan African Association.

Mtazamo wa Kifalsafa wakati ule ulikuwa kama ule wa kina Martin Luther King au Mandela walijikita zaidi kupigania Haki na Usawa wa WATU weusi na sii Uhuru wa nchi. Wakati wa Mkoloni Msomi mtu mweusi akiwa Daktari basi alipokea mshahara nusu ya Daktari Mtumishi mwingine mzungu au Mhindi japokuwa ana elimu na ujuzi mdogo kuliko daktari mweusi.

Dr. James Aggrey alikuwa msomi na mwanachama wa chama cha watu weusi Marekani - American Negro Academy kikihusishwa Kifalsafa na Pan Africanism. Dr. James Aggrey aliitwa Pan Africanist na alipokuwa Africa alifanikiwa kuwashawishi na kuwaelimisha wengi juu ya haki zao na baadhi ni viongozi mashuhuri kama Hastings Banda wa Malawi, Mnamdi Azikiwe wa Nigeria na Kwame Nkrumah wa Ghana.

Kwa bahati mbaya sana Dr.James Aggrey alifariki mwaka 1927 Marekani, lakini malipo yake hakupewa heshima alostahili katika kumbukizi na Harakati za Uhuru wa nchi za Afrika zaidi ya jina la mtaa mmoja Kariakoo - Miafrika Ndivyo Tulivyo.

Hivyo, hata kumbukumbu ya taarifa hii ya Kleist na wenzake pia haikujitosheleza zaidi kutuelimisha juu ya Uongozi wa chama hiki Bara na Visiwani. Kulikuwa na mahusiano gani kati ya Uongozi wa chama hiki kati ya Tanganyika na Zanzibar?. Je, Ni sababu zipi zilopelekea utengano baina ya Zanzibar na Bara? Je, ilitokana na Utaifa dhidi ya Umoja wa nchi za Afrika (Africa Nationalism vs Pan Africanism ) ama kulikuwa na changamoto nyinginezo?

Je, ni Kina nani walikuwa Viongozi wa AA Kitaifa (Bara na Zanzibar)? Ama kule Zanzibar kati ya 1929 hadi 1948 kina nani walikuwa viongozi? Maana sote tunafahamu kwa Uchache sana kuwa chama cha African Association iliendelea kuwepo Zanzibar hadi mwaka 1957 walipoungana na Shiraz Party kuzindua chama kipya cha Kisiasa (Afro - Shiraz Party).

- Ukweli ni upi?
Nitaendelea na Sehemu ya pili ya Harakati – Kuzaliwa kwa TAA.

Mohamed Said akajibu kama ilivyo hapo chini:

Imenilazimu kusema kitu kuhusu historia ya uhuru wa Tanganyika kwa kuwa nimeandika kitabu kusahihisha historia ya TANU ambayo kwa miaka mingi watu waliamini kuwa ndiyo historia ya kweli ya kwanza ya Julius Nyerere katika harakati hizi na ndiyo historia yenyewe ya African Association.

Bwana Mkandara anauliza ukweli ni upi?

Nampa jibu kuwa ukweli wa historia ya uhuru upo katika kitabu nilichoandika, ‘’The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924 – 1968) The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika," (1998).

Halikadhalika ukweli wa historia ya kuasisiwa kwa African Association upo katika Seminar Paper iliyoandikwa na mtoto wa Abdul Sykes ambae ni mjukuu wa Kleist Sykes, Daisy Sykes Buruku, ‘’The Townsman: Kleist Sykes.’’
Hii Seminar paper imehifadhiwa East Africana, Maktaba ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Seminar Paper hii ni sura katika kitabu alichohariri John Iliffe, Modern Tanzanians, Nairobi, 1973, uk. 95 - 114.

Muhimu hapa nieleze kuwa hayo yaliyoandikwa na Daisy Sykes yanatoka katika moja ya nyaraka alizoacha babu yake Kleist Sykes ambae alikuwa katibu muasisi wa African Association mwaka wa 1929 na kwa hakika ni mswada wa kitabu ambacho hakikuchapwa hadi alipokuwa amefariki mwaka wa 1949.

Mimi nikapiga hatua moja mbele ya Daisy.

Wakati Daisy yeye kaandika historia ya babu yake, Kleist Sykes mwaka wa 1968 akieleza vipi African Association iliasisiwa mwaka wa 1929 mimi nikaandika historia ya baba yake Daisy, Abdul Sykes mwaka wa 1998 kueleza vipi TANU ilivyoasisiwa mwaka wa 1954.

Kazi hizi mbili zote zikitumia Nyaraka za Sykes kama ‘’primary source.’’

Msemaji kaandika na amemtaja Martin Kayamba na kusema kuwa ni Mzanzibari.

Ukweli ni kuwa Martin Kayamba ni Mbondei na kwa kuwa ni rika la Kleist Sykes nimemsoma vya kutosha Martin Kayamba wakati natafiti kitabu cha Abdul Sykes.

Katika kitabu alichohariri John Iliffe, ‘’Modern Tanzanians,’’ moja ya sura katika kitabu hicho mwandishi akiwa Iliffe mwenyewe ni ‘’The Spokesman: Martin Kayamba,’’ uk. 66-94.

Atakae anaweza kumsoma Martin Kayamba katika kitabu alichoandika:
The Autobiography of Martin Kayamba, ‘’The Story of Martin Kayamba Mdumi, MBE, of the Bondei Tribe,’’ kitabu hiki amehariri Margery Perham, Ten Africans, uk. 175-272.

Kuna kosa lingine kuhusu kuhusu Dr. Aggrey.

Dr. Aggrey ni Mwafrika maarufu sana na historia yake ni maarufu pia.

Dr. Aggrey alisoma Columbia University, New York lakini si Mmarekani ni Mwafrika kutoka Ghana wakati wake ikiitwa Gold Coast.

Mwalimu Google anaweza kutusaidia kumfahamu.
Nimeandika haya ili yawe msaada kwetu sote katika kuijua historia ya kweli ya nchi yetu.

Hakika uongo ukisemwa sana huja ukawa kuwa ukweli.
Historia hii ilifutwa ukapachikwa uongo na uongo ule watu wakauamini ukawa ndiyo ukweli.

Leo watu wanaanza Alifu kwa kijiti.
Wanaisoma upya historia ya TANU.
 
Back
Top Bottom