Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi: Kaya 1,373 zenye Watu 8,364 zimeshahama Ngorongoro kufikia Aprili 2024

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi: Kaya 1,373 zenye Watu 8,364 zimeshahama Ngorongoro kufikia Aprili 2024

Ojuolegbha

JF-Expert Member
Joined
Sep 6, 2020
Posts
1,278
Reaction score
797
TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU MAENDELEO YA MPANGO WA UHAMAJI WA HIARI KUTOKA ENEO LA HIFADHI YA NGORONGORO KWENDA MSOMERA NA MAENEO MENGINE YA NCHI

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi leo Mei 26, 2024 amezungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya mpango wa uhamaji wa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha kwenda Msomera mkoani Tanga na maeneo mengine ya nchi.

IMG-20240526-WA0076.jpg
IMG-20240526-WA0080.jpg
IMG-20240526-WA0078.jpg

photo_2024-05-26_15-32-01.jpg

photo_2024-05-26_15-32-06.jpg

photo_2024-05-26_15-32-10.jpg

===========

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU MAENDELEO YA MPANGO WA UHAMAJI WA HIARI KUTOKA ENEO LA HIFADHI YA NGORONGORO KWENDA MSOMERA NΑ ΜΑΕΝΕΟ MENGINE YA NCHI

Mobhare Matinyi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali. Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Jumapili, Mei 26, 2024: Saa 7:30 Mchana.

UTANGULIZI
1. Itakumbukwa kwamba kuanzia mwaka 2022 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianza kutekeleza mpango wake wa kuwahamisha kwa hiari wananchi wanaoishi ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha, kwenda katika maeneo mapya yaliyotengwa.

2. Maeneo hayo ni vijiji vya Msomera wilayani Handeni na Saunyi wilayani Kilindi mkoani Tanga; na Kitwai wilayani Simanjiro, mkoani Manyara. Maeneo haya yana ukubwa wa kilomita za mraba 4,210, yaani mara tatu ya eneo la jiji la Dar es Salaam ambalo ni kilomita za mraba 1,393.

3. Uhamishaji huu wa hiari kutoka hifadhini Ngorongoro unasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). Ujenzi wa makazi mapya unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) ikishirikiana na wizara za sekta husika.

4. Inatarajiwa wakazi karibu 100,000 ndio watakaohamia katika maeneo hayo matatu makubwa. Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro linalotumiwa na binadamu lina ukubwa wa kilomita za mraba 3,700 kati ya kilomita za mraba 8,292 za eneo lote la hifadhi, au takribani asilimia 45.

5. Mpango mzima wa Serikali ni kujenga nyumba 5,000 ambazo zinatarajiwa kwamba zitachukua kaya zitakazohamia katika eneo hilo huku zingine zikihamia kwa hiari kwingine ndani ya nchi.

6. Mpangilio wa mradi mzima ni kujenga nyumba 2,500 katika kijiji cha Msomera ambacho ndicho kinachopokea watu hivi sasa; nyumba 1,500 Kitwai na nyumba 1,000 Saunyi. Ujenzi wa nyumba hizi unafanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa gharama za Serikali.

TAKWIMU ZA UHAMAJI
7. Tangu awamu ya pili ianze tarehe 24 Agosti, 2023 hadi 28 Aprili, 2024, kaya 822 zenye watu 5,354 zimeshahama ambapo 745 zenye watu 4,855 zimehamia Msomera na 77 zenye 499 zimeenda maeneo mengine ya nchi. Idadi ya mifugo iliyohama na wananchi hawa wa jamii ya wafugaji ni 21,136.

8. Katika awamu ya kwanza ya zoezi hili ambalo lilianza tarehe 16 Juni, 2022 hadi tarehe 18 Januari, 2023, jumla ya kaya 551 zenye watu 3,010 zilihama ambapo kaya 503 zenye watu 2,692 zilihamia Msomera na kaya 48 zenye watu 318 zilichagua kwenda kwenye maeneo mengine ya nchi kwenye mikoa zaidi ya nane. Jumla ya mifugo iliyohama katika awamu hii ilikuwa 15,321.

9. Hivyo basi, katika awamu zote mbili tangu mpango huu ulipoanza mwezi Juni 2022 hadi Aprili 2024, jumla ya kaya 1,373 zenye jumla ya watu 8,364 zimeshahama. Katika kijiji cha Msomera hadi sasa zimeshaenda kaya 1,248 zenye watu 7.547 na maeneo mengine kaya 125 zenye watu 817 huku jumla ya mifugo ikiwa 36,457 ambapo 30,314 ni kwa Msomera na 6,143 ni kwenye maeneo mengine nchini.

TAKWIMU ZA UJENZI WA NYUMBA

10. Katika kijiji cha Msomera kwenye eneo A, B, C na D tayari nyumba 1,000 zimeshakamilika huku nyumba 737 zikiwa zimeshahamiwa na wananchi. Nyumba 263 zilizobakia zipo tayari kwa ajili ya kupokea kaya ambazo muda wowote kuanzia wiki ijayo zitapelekwa. Nyumba nyingine 1,500 bado ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi ili kufikisha idadi ya nyumba 2,500 zilizopangwa kujengwa.

11. Ingawa upimaji wa viwanja vya nyumba umeshafanyika lakini bado ujenzi wa nyumba zingine 1,500 katika eneo la Kitwai na 1,000 katika eneo la Saunyi haujaanza. Nyumba hizi pia zitajengwa na jeshi.

UHIFADHI NA UTALII NGORONGORO
12. Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro limeendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi kwa kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori aina ya faru ambao ni adimu. Ngorongoro ni eneo maalum kwa faru weusi wakiwa katika mazingira yao ya asili. Vilevile, Mamlaka imeendelea kupambana na kudhibiti mimea vamizi na kuimarisha nyanda za malisho kwa ajili ya wanyamapori katika maeneo mbalimbali.

13. Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro limeendelea kupokea idadi kubwa ya wageni ambapo kati ya mwezi Julai 2023 na Aprili 2024 ilifikia 780,281 ikiwa ni miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha wa 2023/24 haujaisha. Mapato yaliyopatikana ni sh. 188,519,361,412/- na kuvuka lengo la shilingi bilioni 155.4. Idadi hii imeshazidi ya mwaka 2022/23 uliopata wageni 752,000. Haya ni matunda ya filamu ya Tanzania: The Royal Tour iliyoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

MKAKATI WA UELIMISHAJI, UHAMASISHAJI NA UANDIKISHAJI
14. Ili kufanikisha mpango huu wa kuwahamisha wananchi kwa hiari na kwa kujali haki za binadamu, Serikali na NCAA ziliamua kuweka mkakati maalum wa uelimishaji, uhamasishaji na uandikishaji ukijumuisha viongozi na watendaji wa serikali za mitaa ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

15. Mkakati huu unafuata maeneo yaliyogawanywa katika kanda tano za kaskazini, kusini, mashariki, magharibi na kati mwa tarafa ya Ngorongoro ili kuhakikisha kata zote 11 na vijiji vyake na vitongoji zinafikiwa. Wilaya nzima ina kata 28 ambapo tarafa ya Loliondo ina nane na Sale kata tisa.

16. Timu ya uelimishaji, uhamasishaji na uandikishaji inashirikiana na wataalamu wa ustawi wa jamii kutoka Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru na imeshawafikia wananchi wengi wanaohusika na uhamaji wa hiari kwa kutembelea nyumba za ibada, minada, mikutano ya hadhara na kukutana na baadhi ya viongozi wa kimila, watu maarufu na wenyeviti wa vitongoji na vijiji.

17. Lengo la mikakati yote hii ni kuhakikisha wananchi wanauelewa mpango huu wa uhamaji wa hiari unaojali haki za binadamu, umuhimu wa uhifadhi, sababu zake, faida na utekelezaji wake ili kuondoa hofu na mashaka kwa wananchi wa Ngorongoro, nchi yetu na jumuiya ya kimataifa.

18. Uandikishaji wa wananchi wanaohama kwa hiari hufanywa kwa kuzingatia nani ni mkuu wa kaya na idadi ya wategemezi; mali na maendelezo yaliyofanywa na kaya; idadi ya mifugo; na utambulisho wa makazi kwa kutumia nukta za kijiografia. Taarifa zote hizi huwekwa katika vishikwambi vyenye mfumo uliobuniwa na wataalamu wetu wa Tehama uitwao Ngoromso.

19. Awamu ya pili ya uhamaji wa hiari imefanikiwa vema kwani tangu mwezi Aprili 2023 hadi Aprili 2024 kaya 793 zimeandikishwa katika takriban kata na vijiji vyote vya tarafa ya Ngorongoro. Vijiji ambavyo vimekuwa na mwamko mkubwa ni Olpiro na Masamburai kwenye kata ya Eyasi pamoja na Naiyobi na Kapenjiro kwenye kata ya Naiyobi. Hadi sasa ni kaya 160 tu zilizoandikishwa ndizo bado hazijahama ambapo 67 kati ya hizo zinasubiri uthamini na 93 zinakamilishiwa taratibu za kuhama.

UTHAMINISHAJI NA MALIPO YA STAHIKI
20. Wakati kazi ya uandikishaji ikiendelea, timu ya wataalamu huendelea pia na kazi ya uthaminishaji ambapo wakuu wa kaya huoneshwa fidia wanayostahili kulipwa mbali ya fedha za ziada ambazo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliekeleza kila kaya ilipwe, yaani shilingi milioni 10.

21. Uhamaji hufanyika baada ya malipo ya fidia kukamilika; kuvunja makazi au maendelezo na kuchagua mali wanazotaka kuhama nazo. Hapo ndipo usafirishaji wa watu, mifugo na mali zao hufanyika kwa hiari na kwa kuhakikisha wasafiri wanapata huduma zote safarini hadi kufika Msomera au popote pengine wanapochagua kuhamia. Kwa wanaohamia maeneo mengine ya nchi mbali ya usafiri wa kuhamia, hulipwa pia shilingi milioni 15 za ziada kwa kila kaya badala ya sh. milioni 10.

22. Kwa wananchi wanaohamia sasa Msomera, na baadaye itakuwa Kitwai na Saunyi, maandalizi huenda sambamba na uandaaji wa hati za nyumba ya vyumba vitatu iliyo katika eneo lenye ukubwa wa ekari 2.5 na shamba binafsi la ekari tano. Hati hizi hukabidhiwa wakuu wa kaya wakati wa kuagwa wakiwa bado Ngorongoro chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya, Mhe. Kanali Wilson Sakulo.

23. Wananchi wanaohamia Msomera hupewa chakula magunia mawili ya mahindi kwa kila miezi mitatu kwa kaya kwa muda wa kipindi cha miezi 18 wakati wakiandaa mashamba; malisho, majosho na maji ya mifugo yao; kujengewa shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, mnada wa kisasa na vituo vya kuuzia maziwa; miundombinu ya maji, barabara, umeme, posta na mawasiliano; huduma za usalamana uangalizi wa serikali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Albert Msando.

MAELEKEZO YA SERIKALI KWA WANANCHI
24. Baada ya Serikali kujiridhisha kwamba hamasa ya wananchi kuhama ni kubwa, inapenda kushauri na kusisitiza kwamba, wale wote wanaotaka kwenda katika kijiji cha Msomera wafuate taratibu zote za kuhamia huko ili kuepuka usumbufu. Rai hii ni kutokana na kupatikana kwa taarifa kwamba baadhi ya watu kutoka Ngorongoro huenda Msomera kusalimia ndugu na jamaa zao na wakiona mazingira ni mazuri huamua kubaki huko na kuleta changamoto ya makazi na huduma zingine.

25. Serikali inawashauri wananchi wanaopatwa na changamoto zozote wawasiliane na serikali za vijiji ili wahudumiwe. Serikali inaendelea kuboresha makazi mapya na kuhamasisha uhamaji wa hiari.

PIA, SOMA:
-
Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi kuzungumza na Waandishi wa Habari leo 26/5/2024 7:30 mchana
- Juliana Mwakang'ali: Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Ifutwe
- Wamasai waliohama Ngorongoro walalamika zoezi hilo kuzungukwa na udanganyifu, wasema watarudi
 

Attachments

  • IMG-20240526-WA0083.jpg
    IMG-20240526-WA0083.jpg
    142 KB · Views: 5
  • IMG-20240526-WA0084.jpg
    IMG-20240526-WA0084.jpg
    152.4 KB · Views: 4
  • IMG-20240526-WA0085.jpg
    IMG-20240526-WA0085.jpg
    156.5 KB · Views: 5
  • IMG-20240526-WA0082.jpg
    IMG-20240526-WA0082.jpg
    428.8 KB · Views: 10
Eneo la kuchungia mifugo litakuwa wapi? Hawa ni wafugaji ndio kazi yao. Tanga mbona ni kukame? Ndio sababu wako morogoro mpaka mbeya wakifuata malusho na maji. Hatua ya pili iwe kuwawekea eneo la mifugo ikiwa na maji. Hapo msonera serikali ifanye mpango wa ugani wFuge kisasa kwa vike eneo la kufugia holela linazidi kuwa finyu. Wamasai wanaelejea nchi za kusini na mifugo yao. Walitokea kaskazinj wanazidi kuelekea kusini.
 
Eneo la kuchungia mifugo litakuwa wapi? Hawa ni wafugaji ndio kazi yao. Tanga mbona ni kukame? Ndio sababu wako morogoro mpaka mbeya wakifuata malusho na maji. Hatua ya pili iwe kuwawekea eneo la mifugo ikiwa na maji. Hapo msonera serikali ifanye mpango wa ugani wFuge kisasa kwa vike eneo la kufugia holela linazidi kuwa finyu. Wamasai wanaelejea nchi za kusini na mifugo yao. Walitokea kaskazinj wanazidi kuelekea kusini.
Mkuu zingatia uandishi basi hili jukwaa siyo la vilaza
 
Unawahamisha watu Kwa nguvu na mitutu halafu unasema hiari, na vipi mbona sijaona kesi yeyote kupinga huu uonezi wanaofanyiwa wananchi, mahakama zetu sio perfect na zina mahakimu wengi wanafanya kazi Kwa uchawa, lakini mara nyingi mahakama Kuu kesi ikifika kwao wanajitahidi kutoa hukumu ya haki
 
Back
Top Bottom