Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Bara, Ester Thomas, ametoa onyo kali dhidi ya vitendo vya kuwahusisha wananchi wanaoiunga mkono ACT Wazalendo na madai ya kufutiwa msaada wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Masewa, kata ya Masewa, jimbo la Bariadi mkoani Simiyu, Alhamisi Novemba 21, 2024, kama sehemu ya kampeni ya chama hicho kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, Ester amesisitiza kuwa fedha za TASAF si mali ya chama tawala, bali ni misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo kwa ajili ya kusaidia kaya maskini nchini.
Ester amesema kuwa si sahihi kwa watu kuogopeshwa kwa hofu ya kupoteza msaada wa TASAF kwa sababu ya kuonesha mapenzi kwa ACT Wazalendo. Ameeleza kuwa mpango huo unalenga kusaidia kaya zenye uhitaji na hautakiwi kutumika kama chombo cha kuwahujumu wapigakura.