Hivi karibuni, Msimu wa Kutangaza Tamthilia na Filamu za Beijing Afrika ulianza jijini Dar es Salaam, Tanzania. Tukio hilo lililoandaliwa na Ofisi ya Redio na Televisheni ya Mji wa Beijing, lilifungua ukurasa mpya wa mawasiliano ya kitamaduni kati ya China na Afrika, na kukuza uhusiano wa kina kwa njia ya simulizi za sauti na kuona.
Tamasha hilo kwa sasa linaadhimisha miaka 10 ya ushirikiano thabiti kati ya Beijing na nchi za Afrika kupitia maonesho ya filamu bora, huku likiendelea kuimarisha na kukuza uhusiano wa Sanaa na wasanii.
Kwenye sherehe hizo za uzinduzi zilizopambwa kwa shamrashamra nyingi, viongozi mbalimbali walihudhuria wakiwemo wawakilishi kutoka Idara ya Televisheni na Redio ya Beijing, Bodi ya Uendelezaji wa Filamu ya Tanzania, Baraza la Sanaa la Tanzania (Basata), makampuni ya Kichina barani Afrika, watengenezaji filamu wa Tanzania na wadau wengine mbalimbali wa sekta ya filamu kutoka pande zote mbili.
Kupitia lenzi za kamera, sasa Watanzania wanaweza kujionea kwa macho yao changamoto, ushindi, na mafanikio mbalimbali kwenye tamthilia na filamu za Beijing zilizozinduliwa siku hiyo, na hivyo bila shaka kutaibua hisia za ukaribu na mshikamano kupitia filamu hizo. Hatua hii pia itasaidia zaidi kukuza ujuzi unaoongezeka wa wataalam wa filamu, viongozi, mameneja, vikundi vya michezo ya kuigiza na waigizaji wengine wa filamu nchini Tanzania.
Akielezea safari ya tamasha hili iliyoanza miaka 10 iliyopita, wakati lilipozinduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Televisheni na Redio ya Beijing, Dong Dianyi, amesema tamasha hili limejenga daraja muhimu la mawasiliano ya kiutamaduni kati ya China na Afrika, na sasa limekuwa alama ya urafiki wa kweli kati ya watu wa pande hizi mbili. Pia amesema wanatazamia kuendelea kuimarisha ushirikiano huu katika miaka ijayo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Bodi ya Filamu ya Tanzania, Emmanuel Ndumukwa, amesema kuwa tamasha hilo limechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuzaji wa sekta ya filamu nchini Tanzania. Akitolea mfano wa mafanikio ya Tamthilia kama vile Karibu Kijiji cha Milele, ambayo ilitafsiriwa kwa Kiswahili na lugha nyingine, na hata kushinda “Tuzo maalum ya kuchangia urafiki kati ya China na Tanzania, Bw. Ndumukwa amesema tamasha hili limeleta filamu mpya zenye maudhui mbalimbali, yakiwemo yanayosimulia safari ya ushirikiano kati ya China na Afrika, na filamu ya katuni ya Shuke na Beta itakayovutia watoto wa Afrika.
Kwa upande mmoja Tamasha la Kutangaza Tamthilia na Filamu za Beijing Afrika, linahakikisha linakidhi ladha za watazamaji wa rika zote na kuongeza uelewa wa tamaduni mbalimbali na pia kuonesha uchangamfu wa jamii ya kisasa ya China, na kwa upande wa pili linabeba jukumu muhimu la kukuza Kiswahili katika jukwaa la kimataifa na kuhimiza mawasiliano ya kitamaduni. Kupitia masimulizi ya pamoja na juhudi za ushirikiano, uhusiano kati ya mataifa haya mawili utaendelea kustawi, ukichochea ushirikiano na nia njema kwa vizazi vijavyo.
Tangu mwaka 2014, tamasha hili limewafikia watu katika nchi 13 za Afrika, zikiwemo Kenya, Nigeria, na Afrika Kusini, ambapo limeonesha filamu 148 kwa lugha kama Kiswahili, Kiingereza, Kihausa, Kireno na Kifaransa.
Mbali na maonesho ya filamu, tamasha hili pia limeleta matukio kama vile mashindano ya utiaji sauti wa filamu na tamthilia, maonesho ya sanaa ya mapigano yaani Kungfu, na shughuli za katuni kwa watoto, likisogeza karibu utamaduni wa China katika nchi za Afrika kwa njia ya kuvutia na shirikishi.