Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,985
- 10,840
Simulizi : MTAMBO WA MAUTI
Mwandishi : BEN R. MTOBWA
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
Sehemu ya 1
W 1 X
HILI lilianza kama tamthiliya, tena tamthiliya yenyewe nyepesi tu, ya mapenzi. Kama waigizaji katika tamthiliya hiyo, si Joram Kiango kwa upande mmoja;
wala msichana huyu, kwa upande wa pili, alipata angalau kuhisi tu kuwa mwanzo wa tamthiliya hiyo ulikuwa sawa na kuanza kwa mkasa mzito kama mkondo wa mto unaopita katika majanga ya nchi yenye kila aina ya ukatili na unyama usiomithilika.
Dar es Salaam ikiwa imefurika wasichana warembo kupindukia, wengi wao wakiwa wameuongeza urembo wao wa asili maradufu kwa vipodozi lukuki vilivyofurika madukani, msichana huyu, machoni mwa Joram alikuwa wa kawaida kabisa. Hata hivyo, baada ya kumtazama kwa makini zaidi alibaini kuwa alikuwa na ziada moja juu ya urembo wake. Si ile ngozi yake ya maji ya kunde, la hasha. Ilikuwa ngozi ya kawaida ingawa weusi wake uliifanya imeremete na kushawishi kuigusa. Si lile tabasamu lake la mara kwa mara. Hilo pia ni jambo la kawaida katika nyuso za wasichana wa kileo na lingeweza kununuliwa kwa fedha tu iwapo mwenyewe angejali kujiunga na chuo kimojawapo cha usanii na kuhitimu. Hali kadhalika, ziada hii haikutokana na macho yake maangavu, pua yake iliyochongoka; wala meno yake meupe yaliyojipanga kikamilifu kinywani mwake kama mistari miwili ya punje za
mahindi kwenye kibunzi.
Alikuwa na ziada!
Lakini ziada hii ilikuwa ipi? Joram alijiuliza akimtazama kwa hila mrembo huyo aliyeketi kando. Macho yao yakagongana. Yale ya msichana yalihimili kwa sekunde moja dhidi ya yale ya Joram, sekunde ya pili yakawa yameangukia chini huku lile tabasamu lake likigeuka kuwa katika sura nyingine. Ni hapo Joram alipobaini ile ziada iliyomvuta katika sura na umbile la msichana huyu.
Haya!
Alikuwa msichana mwenye haya! Mmoja kati ya wasichana wachache kabisa duniani waliobakia na haya. Wengi wao, toka walipoanza kuvaa suruali kama wanaume, huku wakienda kazini na kurudi jioni kama wanaume, kile kirusi kinachoitwa ‘haya’ kilitoroka zama za kale katika maumbile yao na, hivyo, kuwaacha wakavu kama wanaume.
Akiwa amevutwa na hilo, kwa mara ya kwanza Joram Kiango alijikuta akimtilia maanani na kuamua kumsikiliza, badala ya kuishia kumsikia tu.
“Umesema unaitwa nani vile bibie?” alimuuliza. “Mona.”
“Mona?” “Mona Lisa.”
Joram alipata kuziona mara nyingi nakala za ule mchoro maarufu duniani wa Mona Lisa. Aidha, aliwahi kuiona nakala halisi ya mchoro huo katika jumba moja la kumbukumbu za Sanaa nchini Ufaransa. Mchoro huo ulichorwa na msanii maarufu aliyeishi mwaka 1452 hadi 1519 huko Italia, Leonardo da Vinci, akimwigiza mrembo huyo Mona, aliyezaliwa kati ya mwaka 1503 na 1506; mchoro ambao mtu mmoja, Vincenzo Peruggia aliwahi kuuiba toka katika jumba hilo na kuuficha kwa kuamini kuwa ulikuwa umeibiwa na Napoleon wakati wa vita vilivyoifanya Ufaransa iitawale Italia kwa muda mrefu. Lakini mchoro huo ukakamatwa na kurejeshwa tena Ufaransa mwaka 1913, baada ya kibaka huyo kujaribu kuuza.