Nimepata kukutana na marafiki zangu kadhaa na wamekuwa wakidai kuwa, wao hawapendi kabsa kutumia kondomu wakiwa kwenye faragha zao, huku wakidai kuwa mafuta au vilainishi vilivyomo ndani ya Kondomu zinawafanya wapate upele pamoja na miwasho.
Naomba kuuliza, Je ni kweli matumizi ya Kondomu yanaweza kumletea mtu kupata mzio (allergy)?
Naomba kuuliza, Je ni kweli matumizi ya Kondomu yanaweza kumletea mtu kupata mzio (allergy)?
- Tunachokijua
- Kondomu ni zana inayotumika kujikinga dhidi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo Maambukizi ya VVU pamoja na ujauzito. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ikiwa itatumika kwa usahihi, Kondomu ya kiume huzuia ujauzito kwa 98% huku kondomu ya kike ikiwa na uwezo wa kuzuia ujauzito kwa 95%.
Kondomu zinaweza kugawanywa kwenye makundi matatu kutokana na aina ya malighafi yanayotumika. Zinaweza kuwa za latex (Mpira), plastiki au kondomu zilizotengenezwa kwa kutumia ngozi za wanyama (Lambskin).
Kondomu na Mzio (Allergy)
Mzio hutokea pindi mwili wa binadamu unapokumbana na vitu kwenye mazingira ambavyo haviwadhuru walio wengi. Vitu hivyo vinaweza kuwa chakula, vumbi, vinywaji n.k ambavyo kwa watu wengine huwa mara nyingi huwa havina madhara yoyote.
Baadhi ya dalili za kupatwa na mzio ni wekundu wa ngozi, miwasho, vipele, wekundu wa macho na kuvimba kwa midomo.
Sasa swali la msingi linasalia kuwa, ni kweli kondomu inaweza kusababisha mzio kwa mtumiaji?
Ufuatiliaji wa JamiiCheck umebaini uwepo wa uwezekano wa kupatwa na mzio baada ya kutumia kondomu.
Kwa mujibu wa taasisi ya Mayo Clinic, malighafi ya latex (mpira) yanaweza kusababisha mzio kwa binadamu. Aidha, mafuta na vilainishi vingine vinavyowekwa kwenye kondomu vinaweza kusabanisha mzio.
Kwa mujibu wa tafiti, 80% ya kondomu zote zinazotengenezwa duniani hutumia malighafi ya latex (Mpira). Kwakuwa malighafi haya yanaweza kusababisha mzio, kondomu zake zinaweza kusababisha mzio pia.
Ukubwa wa tatizo upoje?
Kwa mujibu wa taasisi ya Planned Parenthood, takriban 6% ya binadamu duniani wanakabiliwa na changamoto ya kuwa na mzio unaotokana na mpira (latex).
Watu wenye mzio wa aina hii ya kondomu hushauriwa kutumia aina nyingine ya kondomu isiyotengenezwa kwa malighafi ya mpira ili kujiepusha na changamoto zinazoweza kuathiri afya yao.