KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba ameomba kukutana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad wazungumze kuhusu hatima ya mwafaka wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Habari zilizothibitishwa na baadhi ya viongozi waandamizi wa makao makuu ya CCM, jijini Dar es Salaam, zinaeleza kuwa Makamba ameomba suala hilo kupitia barua yake ya Aprili 25, mwaka huu, aliyomwandikia Maalim Seif.
Vilevile, Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF Taifa ambaye pia ni Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Ismail Jussa, wamelithibitishia gazeti hili jana kuhusu chama chao kupokea barua hiyo na kusema kuwa, wamekwishaijibu tangu jana.
Hatua hiyo ya Makamba imefikiwa ikiwa ni siku mbili, baada ya kukaririwa na gazeti hili Jumanne wiki hii, akipinga kufanya mawasiliano yoyote mapya na CUF kuhusu mwafaka huo.
Katika barua hiyo, Makamba amemuomba Maalim Seif wakutane wazungumze ili wapate kuzikutanisha kamati za mazungumzo ya mwafaka za vyama vyao ili waendelee na mazungumzo hayo.
Kwa mujibu wa Jussa, barua hiyo ya Makamba iliandikwa Aprili 25, mwaka huu, lakini ikapokelewa na Katibu Mkuu wa CUF juzi.
Hata hivyo, Hamad na Jussa kwa nyakati tofauti jana, waliliambia gazeti hili kuwa, barua hiyo ilijibiwa jana kwa CUF kulikataa ombi hilo la Makamba.
''Ni kweli tumeipokea barua hiyo. Ni ya tarehe 25, lakini ilipokelewa jana (juzi). Haina chochote cha maana. Tumeijibu leo (jana),'' walisema.
Hamad alisema wamelikataa ombi hilo la Makamba kwa vile mazungumzo kuhusu mwafaka wa kisiasa Zanzibar, yalishaisha muda mrefu na walishafikia makubaliano mbalimbali kati yao na CCM, ikiwamo kuundwa kwa serikali shirikishi, maarufu kama ''Serikali ya Mseto,'' visiwani humo.
Alisema sababu nyingine ya kukataa ombi hilo la Makamba, inatokana na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kushindwa kutekeleza agizo lake alilolitoa mbele ya umma katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Aprili 4, mwaka huu, kwamba atamwagiza Makamba awaandikie CUF makubaliano waliyofikia katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC-CCM), uliofanyika Butiama, mkoani Mara, Machi 29-30, mwaka huu.
Hamad alisema pamoja na CUF kuiandikia barua CCM zaidi ya mara mbili kuomba makubaliano hayo, hadi sasa CCM hawajafanya hivyo.
Alisema sababu nyingine ya kukataa ombi la Makamba, inatokana na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa katika ukumbi huo iliyoonyesha kutoheshimu na kuthamini mamlaka na maamuzi ya Makamba kama Katibu Mkuu wa chama.
Alisema katika mkutano huo wa Diamond Jubilee, Rais Kikwete alikaririwa akisema saini ya Makamba na Maalim Seif hazitoshi kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na kamati za mazungumzo ya mwafaka za vyama hivyo.
''Hivyo, sisi hatuwezi kukaa na mtu ambaye hana 'mandate' (mamlaka) kwa chama chake na asiyekuwa na uwezo wa kukwamua matatizo. Sisi Katibu Mkuu wetu ana 'mandate' katika chama na maamuzi yake tunayaheshimu na kuyathamini,'' alisema Hamad.
Jussa na Hamad walisema njia pekee iliyobaki hivi sasa, ni Rais Kikwete kuwakutanisha Maalim Seif na Rais Aman Abeid Karume, kama alivyofanya Kenya kwa kuwakutanisha Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga na Rais Mwai Kibaki wa PNU, ili kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo visiwani humo.
Jumatatu wiki hii, Makamba aliliambia gazeti hili kuwa wanasubiri majibu kutoka CUF kuhusu suala hilo na kwamba, haoni sababu ya kujibu barua aliyoandikiwa na Maalim Seif kukataa kuendeleza mazungumzo yaliyoitishwa upya na CCM.
"Tulitoka Butiama, tukawaandikia barua kuwaomba turejee katika mazungumzo. Wao wakatuandikia kuwa hawataki. Sasa unataka niwajibu nini? Mimi ndiye nangoja majibu kutoka kwao," alisema Makamba kwa njia ya simu juzi.
Kauli hiyo ya Makamba, ilitolewa siku hiyo saa chache baada ya Hamad, kuliambia gazeti hili kuwa CCM hawajajibu barua yao.
Katika barua hiyo yenye Kumbumbuku namba CUF/AKM/CCM.II/2008/007 ya Aprili 14, 2008 iliyosambazwa kupitia mtandao wa intaneti, Maalim Seif alisema CUF haiko tayari kushirikiana na CCM kuwahadaa Watanzania kwa kuendeleza mazungumzo yasiyo na mwisho na yaliyokosa nia njema.
Nakala ya barua hiyo ya Maalim Seif, ilipelekwa pia kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Rais Amani Abeid Karume na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Wengine, ni Mwenyekiti Mwenza wa Mazungumzo ya Mwafaka kutoka CUF, Hamad Rashid Mohamed na Mwenyekiti Mwenza wa Mazungumzo hayo kutoka CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru.
Maalim Seif alisema pendekezo la kufanya kura ya maoni akiita kuwa ni kiini macho chenye lengo la kuchelewesha utiaji saini na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa, halikubaliki kwa CUF.
Source: Gazeti Mwananchi