Yesu,
Inaelekea wewe ni mgeni katika jukwaa hili.
Itakuwa tabu kujibu yote uliyosema.
Nitakueleza historia ya babu yangu Salum Abdallah:
BABU YANGU SALUM ABDALLAH POPO
Ikiwa umemsoma babu yangu Salum Abdalah na kigoma chake cha daku utakuwa umeona kuwa alipata kuwekwa kizuizini mwaka wa 1964.
Hayo hapo chini yatakusaidiwa kumwelewa mtu huyu.
Ilikuwa mwaka wa 1965 babu yangu Salum Abdallah katoka jela ya Uyui Tabora alikowekwa kizuzini mwaka wa 1964 baada ya maasi ya Tanganyika Rifles tarehe 20 Januari 1964 hana kazi yuko nyumbani.
Mwaka wa 1953 akiwa na taarifa kutoka Dar es Salaam kuwa kuna harakati za kuunda chama cha siasa yeye na wenzake Tabora wakawa wanafanya mikutano ya siri kila Jumapili Town School ambako Abubakar Mwilima alikuwa mwalimu na yeye Mwalimu Abuu kama walivyopenda kumwita ndiye aliyekuwa akiwafungulia darasa moja kukutana na kupeana habari kutoka New Street Dar es Salaam, Makao Makuu ya TAA.
Hii ailikuwa baada ya kumtuma Katibu wa TAA Western Province, Germano Pacha kwenda Makao Makuu ya TAA kuwapa taarifa kuwa Tabora inataka kuunda chama cha siasa.
Germano Pacha alipokelewa Dar es Salaam na Abdul Sykes na akamwambia arudishe salamu Tabora kuwa wafanye subira.
Tufupishe kisa kwani kuna mengi.
TANU ikaundwa mwaka wa 1954 babu yangu akiwa mmoja wa wanachama wa mwanzo.
Mwaka wa 1955 babu na Kassanga tumbo wakaunda Tanganyika Railway African Union (TRAU) babu akiwa President na Kassanga Tumbo Secretary.
Babu yangu Salum Abdallah ana historia ya uzalendo ya kusisimua ambayo hutochoka kuisikiliza kila inapohadithiwa kwa kuwa mkasa una kuwa ndani ya mkasa mwingine visa vikiunganishwa kama ushanga katika uzi.
Mwaka wa 1965 baba akanifungia safari niende Tabora kumwangalia babu baada ya kutoka kifungoni.
Babu yangu jina lake alililopewa na baba yake Abdallah Mwekapopo (naweza kwenda vizazi saba hadi kwa waliokuwa Belgian Congo) ni Rashid lakini katika ujana wake akiwa mfanyakazi wa Tanganyika Railways katika miaka ya 1930 alimpiga Mzungu akafungwa na alipotoka jela akabadili jina lake akawa Salum Abdallah.
Kisa gani akampiga Mzungu?
Huyu Mzungu alikuwa mbaguzi, mnyanyasaji Waafrika kwa hiyo babu siku moja akaamua kumshughulikia.
Hili lilikuwa kosa kubwa sana wakati wa ukoloni.
Hukaa nikafikiri yule Mzungu alikuwa katika hali gani baada ya kuingia katika mikono ya babu kwani alikuwa kapanda juu futi sita ana kifua kipana ile mitambo, yaami maumbo makubwa ya Kimanyema.
Kwa ajili ya umbo hili akiwa kijana Waingereza walimfunza kazi ya kufua chuma, yaani ‘’foundry,’’ kazi ngumu katika moto na joto kali.
Hii ‘’foundry ’’ ilikuwa ndani ya karakana ya Tanganyika Railways.
Humo ndani ya karakana wanaume wako vifua wazi na nyundo nzito ni kelele za chuma kikigonga chuma cheche za moto zikiruka na miaka ile hakuna vifaa mfanyakazi atavaa kuzuia kelele.
Hii karakana ndiyo ilikuwa ikachonga spea za treni.
Wenyewe kwa wenyewe ndani ya karakana wakizungumza kwa sauti za juu.
Labda ndiyo sababu babu hata akizunngumza hata katika mazungumzo ya kawaida sauti yake siku zote ilikuwa juu.
Hii karakana ilikuwa ndani ya eneo la Tanganyika Railway lakini jirani na Arab Street hivi sasa Mtaa wa Nkrumah na ndiko lilipokuwa lango kuu la wafanyazi wa Tanganyika Railways wakiingilia na kutokea katika miaka ile ya 1930.
Babu akiishi Mtaa wa Kipata.
Nyuma aliyokuwa akiishi ilikuwa inatazamana na nyuma ya Kleist Sykes ambae yeye alikuwa Accounts Clerk (Karani wa Mahesabu) Tanganyika Railways.
Nafasi kubwa sana wakati ule kwani hio kazi wakifanya Wahindi.
Lakini babu yangu juu ya ubabe wake na haya yote alikuwa mtu karimu sana mimi nimeshuhudia kwa macho yangu na labda huu ukarimu alimrithisha baba yangu kwani mara nyingi nikipisha wageni chumbani kwangu nami kwenda kulala ‘’sitting room,’’hadi waondoke.
Hii Karakana ya Railway ikahamishwa Dar es Salaam mwaka wa 1947 kupelekwa Tabora na babu yangu akahamanayo kwenda huko.
Hakurudi tena Dar es Salaam.
Lakini mwaka huo huo alipofika Tabora akaongoza mgomo wa Railway ulioenea nchi nzima na akafanya hivyo mwaka wa 1947, 1949 na tena mwaka wa 1960 miezi michache kabla ya Tanganyika kupata madaraka.
Huu mgomo wa mwaka wa 1960 ulidumu kwa siku 82 na kuweka rekodi kushida mgomo wa Kenya ulioongozwa na Makhan Singh uliodumu kwa siku 62.
Baada ya mgomo huu wa mwaka wa 1960 Nyerere ilimhidhihirikia kuwa mtu huyu atakuja kumpa shida katika Tanganyika huru akawa sasa anamtazama kwa macho mawili.
Picha: Kulia ni Salum Abdallah na anaefuatia ni Kassanga Tumbo na viongozi wa TRAU, Tabora.
View attachment 3043143