Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 15, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 15, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Godfrey Mwambe aachiwa kwa dhamana. Anatuhumiwa kupanga njama za kutaka kumuua ‘Mkuu wa Polisi’

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo Jumatatu Desemba 15, 2025 imeyaondoa rasmi maombi Na. 289778/2025 yaliyokuwa yamefunguliwa na Waziri wa zamani Geoffrey Mwambe dhidi ya Mkuu wa Polisi, DPP na ZCO Dar es Salaam, baada ya Wakili wake Hekima Mwasipu kuomba yaondolewe kufuatia mteja wake kupatiwa dhamana, ombi ambalo halikupingwa na upande wa Jamhuri.

Akizungumza na waandishi wa habari, Wakili Mwasipu amesema Mwambe anakabiliwa na tuhuma mbili; uchochezi kupitia mitandao ya kijamii na kupanga njama za kutaka kumuua ‘Mkuu wa Polisi’ ambaye utambulisho wake haukutajwa, na kwamba baada ya kupatiwa dhamana waliripoti Polisi asubuhi ya leo kama walivyoelekezwa, huku upelelezi ukiendelea.

Aidha, katika tukio jingine mlinzi wa Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, Charles Hangaya ameachiwa kwa dhamana baada ya kushikiliwa na Polisi toka Novemba 8, 2025 aliporipotiwa kuvamiwa na watu waliojitambulisha kuwa Polisi na kutokomea naye kusikojulikana.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameendelea kukemea namna ukamataji wa Polisi unavyofanywa nchini bila kufuata sheria, pamoja na ucheleweshaji wa dhamana kwa makosa ambayo mtu ana haki ya kupatiwa dhamana, wakisema mfumo wa haki umeingiliwa na wanasiasa, na ‘haki’ hiyo inapatikana kwa wale waliokuwa upande wa Serikali iliyo madarakani!

Adha, wananchi wameanza kuhamasishana kuhusu kutafuta njia mbadala za kujilinda dhidi ya Polisi, wakidai wanashindwa kuona tofauti yao na majambazi!

Polisi: Mhadhiri UDOM anachunguzwa kwa kuhamasisha maandamano yaliyopigwa marufuku

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP Gallus Hyera, amethibitisha kukamatwa kwa Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Ndaki ya Sayansi ya Jamii, Melchizedek Tunzi Kaijage kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano kinyume na sheria. Kwa mujibu wa kamanda huyo, Kaijage alikamatwa Desemba 9, 2025 akiwa darasani akiendelea na majukumu yake ya ufundishaji.

Kamanda Hyera amesema baada ya kukamatwa, alihojiwa na baadaye aliachiwa huru na kurejea katika shughuli zake za kawaida, huku uchunguzi wa tuhuma hizo ukiendelea.

Ingawa, baada ya taaria za kukamatwa kwake kusambaa, Waziri wa Elimu Sayansi ya Teknolojia, Adolf Mkenda jana Disemba 15 alisema taarifa za awali za kukamatwa kwa Kaijage hazihusiani na maandamano, bali ‘aliitwa kwaajili ya kuhojiwa kwa masuala yaliyofanyika nje ya chuo’.

Mkenda alisisitiza kuwa Mhadhiri akiwa darasani yuko huru kufundisha sababu wanaamini atafundisha kwa weledi na hawatavuka mstari na kwenda kwenye vitu ambavyo vina makosa makubwa na kama kutatokea makosa ya kiuweledi katika ufundishaji au kwa kutoa matamshi kwenye mambo 'sensitive' mfano kwenye musuala ya dini, siasa za vyama na kadhalika, mamlaka yake ya kumshughulikia sio Polisi bali atachunguzwa na mamlaka ya chuo kupitia ngazi za uongozi sababu ni suala la kiutawala katika utendaji wa kazi, labda kama suala hilo litakuwa ni jinai.

Pia, Mkenda alisema Serikali hawataingia na kusikiliza mihadhara yao kwa lengo la kuwaingilia, kwasababu vyuo vikuu haviendeshwi hivyo na hawataviendesha hivyo.

Desemba 12, 2025 chuo kilitoa taarifa ikisisitiza wahadhiri na watendaji wengine wawe makini wawapo darasani, kikieleza kuwa tukio hilo linaashiria uwepo wa ufuatiliaji, huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini hatua stahiki zitakazochukuliwa.

Maoni ya wananchi:
Mjadala umeendelea kuhusu uhuru wa maoni na taaluma ndani ya vyuo vikuu, wakisema uminywaji wa watu kwenye kutoa maoni yao kwa uhuru unaenda kuua elimu nchini na kuendelea kuzalisha viongozi na watendaji wanaowaza kulinda maslahi yao na sio kwenda kuendeleza ustawi wa jamii.

Wengine wametoa angalizo kwa taaluma kuingiliwa na kuendeshwa kisiasa, wakisema itadhoofisha maeneo mengi nchini na hivyo kupelekea kuwa na taasisi dhaifu jambo ambalo ni tishio kwa uchumi na maendeleo ya nchi.

Kwa upande mwingine wananchi wamehoji kati ya Waziri wa Elimu na Polisi nani anasema ukweli? Na ikiwa mhadhiri huyo amekamatwa kwa kuongelea maandamano; hiyo ni jinai toka lini wakati ni haki ya Kikatiba na ukizingatia alikuwa katika mazingira ya kitaaluma?
 
Back
Top Bottom