Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 2, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Disemba 2, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Samia: Vurugu za Oktoba 29 walitaka kuangusha Dola. Tunapoambiwa tulitumia nguvu kubwa, nguvu ndogo ni ipi? Wanatupa maelekezo kwani wao ni kina nani hasa?

Rais Samia amezungumza na Taifa kupitia mkutano maalum na ‘Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam’, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ambapo amegusia mambo mbalimbali yaliyotokea wakati wa uchaguzi pamoja na kujibu hoja zilizokuwa zikitolewa na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Katika hotuba yake, Rais Samia amezungumzia vurugu zilizojitokeza wakati na baada ya uchaguzi, akisema hayakuwa maandamano ya kawaida bali ni vurugu zilizotengenezwa kwa lengo la kuangusha dola. Amedai kuwa watu wenye nia ovu kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wakifanya kila wawezalo kuporomosha taswira ya Tanzania kwa manufaa yao binafsi. Ameongeza kuwa Serikali imeanza utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, ambapo asilimia 90 ya mageuzi ya muda mfupi na wa kati yamekamilika, huku suala la Katiba Mpya likipangwa kutekelezwa kwa taratibu.

Kuhusu vyombo vya dola kutumia nguvu kubwa wakati wa maandamano, amesema Serikali ilitumia nguvu kwa mujibu wa mazingira ya tukio huku akihoji wanaokosoa nguvu kubwa iliyotumika, nguvu ndogo ni ipi kwa watu ambao walikuwa wakifanya jaribio la mapinduzi?

Pia ameeleza kuwa vijana wa Tanzania si wazalendo, na hawana elimu ya uzalendo ndiyo maana Serikali yake imeamua kuunda Wizara ya Vijana ili kushughulikia matatizo yao, akisema hawakuwa na sababu ya kushiriki kufanya uharibifu.

Samia amewambia wazazi badala ya kulia watoto wao kuumizwa miguu au wamekufa kwa “Bahati mbaya”, kwanini hawakuwazuia kutoka na kwenda kufanya vurugu? Amewataka wazazi wasikubali kuona watoto wao wakitumiwa kama “Kafara za kisiasa” na kuwasisitiza kuwa sehemu ya ulinzi wa amani na kutekeleza jukumu lao la malezi na usimamizi wa vijana badala ya kulalamika baada ya madhara kutokea.

Aidha, amekosoa baadhi ya taasisi za dini kwa kutoa matamko yanayovuruga umoja, akisisitiza kuwa Serikali haiendeshwi kwa misingi ya madhehebu wala kwa kuamrishwa kufuata maelekezo fulani. Amesema hakuna dini moja inayoweza kuiendesha Serikali na wakitoa tamko basi linatakiwa kufuatwa. Akililenga Kanisa Katoliki, amesema toka ameingia madarakani Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) limetoa matamko 8. Amewaasa Watanzania wasivurugwe kutokana na milengo yao ya siasa, dini pamoja na mingine na kutolewa kwenye misingi yao ya amani, umoja, mshikamano na utulivu.

Rais amesema pia waratibu wa vurugu zilizotokea wanaoishi nje ya nchi kuwa ni watu wanaokabiliwa na ugumu wa maisha na hivyo kutumia mitandao kueneza taharuki ili kujipatia kipato. Ameongeza kuwa demokrasia haimaanishi vurugu na kwamba ikiwa hawampendi kiongozi aliyekuwa madarakani wanatakiwa kustahimili, muda wake ukiisha ataondoka na watapata kiongozi mwingine!

Akiwazungumzia viongozi wa baadhi ya vyama vya upinzani, Samia amesema wamekuwa wakipandikiza misimamo ya uchochezi licha ya kuwasaidia kurudi nchini kwa amani na kufutiwa kesi zao na kupewa uhuru wa kufanya siasa. Amesema migogoro ya ndani ya vyama, makundi na kukosa umoja kumesababisha viongozi hao kushindwa kuona mbele, na hivyo kugeukia uchochezi kwa wananchi.

Kuhusu maandamano yanayotarajiwa kufanywa Disemba 9, amesema Serikali imepata taarifa hizo pamoja na kusikia kutoka kwa waandaaji wa nje wakishauri kuyasogeza mpaka katika sherehe za Krismasi, Disemba 25 kwakuwa wakati huu Serikali imejipanga. Samia amewajuza kuwa sio siku ya Krismasi pekee, wakati wowote watakapoamua kufanya maandamno Serikali imejipanga vilivyo kuwakabili.

Akiwajibu vijana waliotoa masharti ili maridhiano yaweze kufanyika huku wakiungwa mkono na baadhi ya wanasiasa pamoja na wanaharakati, Rais amesema hayo (kuipa Serikali masharti) yanatokea ndani ya nyumba baina ya mume na mke wakikorofishana au kwenye Serikali ya wanafunzi, lakini sio kwa Serikali huru, yenye kujielewa na kuendesha mambo yake. Amehoji wale wanaosema wanawawakilisha Watanzania wanamuwakilisha nani hasa, kwani wananchi walishaamua kwa kuichagua CCM kwa 97.66% kuendelea kushika dola, na hilo liliwezekana sababu wapinzani wao wakubwa hawakushiriki kwenye uchaguzi.

Akihitimisha hotuba yake, alizikosoa vikali jumuiya za kimataifa pamoja na mataifa ya nje kwa kile alichokiita kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania, akihoji; wanatoa maelekezo ya vitu kufanyika kwa namna fulani kwani wao ni kina nani hasa? Je, wanadhani wao ni mabwana wa Tanzania? Akisisitiza kuwa wanafanya biashara ili pande zote mbili zifaidike na kwamba hata hivyo fedha wanazotoa ni chache na wakati huu hazipo!

Maoni ya wananchi:
Wengi wameonyesha kukasirishwa na hotuba hiyo wakisema imejaa dharau na kiburi badala ya kuwa hotuba waliyotarajia ingelenga kuliponya taifa na kuanza upya watu wakiwa hawana majeraha. Wanasema kupitia hotuba hiyo, Rais Samia ameonyesha wazi hajutii madhara waliyopata wananchi na hana mpango wa kuwajibika kutokana na mauaji yaliyotokea. Wanadai inaashiria vitendo vinavyokiuka haki za binadamu ikiwemo matukio ya utekaji, yatandelea kufanyika na kuongezeka kwani Rais ametoa baraka zake.

Wengine wamesema hakuna haja ya kutafuta zaidi ushahidi wa nani alitoa amri ya wananchi kuuliwa na vyombo vya dola, kwani Rais ameonyesha wazi ilikuwa ni kwa maagizo yake.

Pia, kuna walioona hali hii kama chachu ya mahusiano ya kidiplomasia kuzidi kuporomoka, wakisema wengine watafuata nyayo za EU na kusababisha hali ya uchumi kuyumba na wananchi kuzidi kutumbukizwa kwenye dimbwi la umasikini. Hata hivyo, baadhi walisema huenda Serikali imeshajipanga kubadilisha uelekeo wa wafadhali kwenda kwa mataifa ya Asia, Urusi na Uarabuni na hivyo kutojali sana ikiwa mataifa ya magharibi yatafunga milango yao kwa Tanzania.

Kwenye upande wa kauli za chuki zinazochochea udini, baadhi wamesema ni dhahiri Rais ndiye alielekeza viongozi wa kiislamu kuleta hoja za udini kwa wananchi ili waache kujadili kuhusu maandamano na uwajibikaji kwa wote waliosababisha mauaji wakati wa uchaguzi. Hii ni kufuatia mashambulizi yake kwa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) walioshauri vile walivyoona inafaa, huku akiacha kukemea kabisa kauli za masheikh zilizokuwa na chuki za kidini.

Aidha, baadhi wamechukulia hotuba hiyo kama chachu ya kushiriki kwenye maandamano na kuhakikisha wale wote wanaotakiwa kuwajibishwa, akiwemo Rais, wanawajibishwa na utawala unaofuata sheria na misingi ya haki unarejeshwe.

Wahadhiri wa Kiislamu wamjia juu Padri Kitima, wataka Serikali ianzishe uchunguzi dhidi ya kauli zake

Wahadhiri wa Kiislamu wameiomba Serikali kumchukulia hatua za kisheria Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, wakidai kuwa kauli zake za hivi karibuni zimeleta taharuki katika jamii.
Wakizungumza na Vyombo vya Habari, walisema kauli za Kitima kuhusu matukio ya Oktoba 29 zimeibua maswali na kuashiria mwelekeo wa uchochezi, wakimtishia Kitima kwa kusema wanayo mengi ya kusema kuhusu Wakristo lakini wamekaa kimya, “Kitima, huu muziki wa Waislamu huuwezi! Damu itamwagika, tunayo mengi ila tumekaa kimya kuhusu Wakristo.”

Pia, wamesema baadhi ya hoja zilizotolewa na Kitima, ikiwemo madai kwamba Polisi waliagiza majeruhi wasitibiwe bali waingizwe mochwari, zilipaswa kupelekwa kwenye Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29 au kutolewa mbele ya Waziri Mkuu, ambaye Padri Kitima alikutana naye siku chache kabla ya kutoa kauli hizo.

Aidha, wamewashutumu (wakatoliki) kwa kuleta udini nchini wakisema wanataka nafasi za juu Serikalini wapate wao pekee, walitolea mfano uteuzi wa Baraza la Mawaziri lililoteuliwa hivi karibuni wakidai Wakatoliki wanaonekana kuwa wengi wakisema hivyo ndivyo wanataka iwe.

Wanazuoni hao, pia wamelituhumu Kanisa Katoliki kuhusika katika kile walichokiita ‘uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29’, wakisistiza kuwa hawatashiriki maandamano mengine yanayotarajiwa kufanyika Desemba 9. Wametoa onyo kwa watakaoshiriki kuwa cha moto watakiona huku wakikanusha kauli inayodaiwa kutolewa na mmoja wa Masheikh kuhusu ‘kukata waandamanaji vichwa’, wakisema haikuwa na maana ya uasi.

Maoni ya wananchi:
Wananchi Wengi wamesema tamko hilo linaonekana kulazimisha hoja ya vita ya kidini ilhali chanzo halisi cha maandamano ni utekaji, mauaji, kesi za uonevu na wizi wa uchaguzi - mambo ambayo hawajayaongelea kabisa na kusisitiza kuwa wanapotosha kwa makusudi ili kupunguza nguvu ya madai ya msingi ya wananchi.

Wengine wamesema viongozi hao wa kidini wameagizwa kufanya mkutano huo ili kupunguza athari zilizotokana na hotuba ya Rais Samia ambapo wanasema hakuonesha chembe ya kujutia yaliyotokea wala kuwa tayari kwa uwajibikaji; jambo lililoongeza hasira kwa wananchi.
 
Back
Top Bottom