Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania: Novemba 11

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania: Novemba 11

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Zungu achaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mbunge wa Jimbo la Ilala na aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la 12, Mussa Azzan Zungu, amechaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupata kura 378 kati ya kura 380 zilizopigwa na wabunge akichukua nafasi ya mtangulizi wake Tulia Ackson ambaye katika Serikali hii hakuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo.

Maoni ya wananchi:
Wananchi wengi hawakuonesha kushangazwa na ushindi Zungu hasa ikizingatiwa bunge hilo kuwa na CCM wengi kuliko wapinzani.

Kwa upande mwingine wananchi wameendelea kutolitambua Bunge hilo wakisema hawajawachagua wabunge hao hivyo ni kama hakuna Bunge wakati huu.

Wakili Maduhu: Jumla ya watuhumiwa 641 wamefikishwa mahakamni kwa kesi za uhaini, unyang'anyi wa kutumia silaha na kufanya vurugu wakati wa Uchaguzi
Wakili Maduhu Williams wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) amesema jumla ya watuhumiwa 641 wamefikishwa mahakamani nchini kwa makosa ya uhaini, unyang’anyi wa kutumia silaha na vurugu kutokana na matukio yaliyotokea kwenye uchaguzi Oktoba 29.

Kati yao, 240 wapo Dar es Salaam, 172 Mwanza, 89 Iringa, 45 Mafinga, 32 Dodoma, 11 Kigoma, 9 Njombe, 29 Bunda, na 9 Tarime, huku Tabora ikiwa na watu 5 wanaoshikiliwa na polisi.

Aidha, zaidi ya watu 60 Arusha wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za uhaini.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameendelea kukosoa kamatakamata inayofanywa polisi wakisema ni namna ya serikali kukwepa uwajibikaji huku wakiwaacha wahusika halisi wa mauaji hayo ambao ni polisi.

Heche: Hatujafanya mazungumzo wala maridhiano na yeyote ili kuachiwa huru
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, amesema hakuna makubaliano wala maridhiano yoyote yaliyofanyika kati yao na vyombo vya dola kabla ya kuachiwa, kinyume na madai yanayosambaa mitandaoni.

Heche alitoa kauli hiyo Novemba 11, mara baada ya kuripoti katika Kituo cha Polisi cha Kati jijini Dar es Salaam, akiwa na Wakili Hekima Mwasipu na viongozi wenzake wa CHADEMA akiwemo Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa, Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Boniface Jacob na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema.

Amesisitiza kuwa - kama jinsi walivyokamatwa, ndivyo walivyoachiwa.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameonesha kufurahia kuwa hakuna makubaliano yaliyofanyika wakisisitiza kuwa hawataki maridhiano hadi matakwa yao yatimizwe, ikiwemo kuwachukulia hatua waliowaua raia siku ya uchaguzi mkuu na uchaguzi kufutwa.

Wengine wameendelea kuwasihi na kusisitiza wasije kugeuka na kuwa wasiliti kama jinsi Mbowe alivyofanya.

Askofu Stephano Musomba wa Kanisa Katoliki awaombea waliopoteza maisha wakati wa uchaguzi kwa kupigwa risasi
Askofu Stephano Lameck Musomba wa Jimbo Katoliki Bagamoyo ameongoza Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Moyo Safi wa Bikira Maria, kuwaombea waliouawa na waliojeruhiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29.

Akizungumza wakati wa ibada hiyo, Askofu Musomba alisema maombi hayo yamelenga kuwatakasia waliopoteza maisha kwa kupigwa risasi, kuwaombea majeruhi wapone haraka, na kuomba haki na amani virejee nchini.

Maoni ya Wananchi:
Wananchi wengi wameendelea walipongeza Kanisa Katoliki kwa kuwa na misimamo ya kweli katika imani bila kujipendekeza kwa Serikali kwaajili ya maslahi yao binafsi, na kuwasihi wasikubali kutishwa au kutetereshwa na serikali.

Kamishna Mkuu Haki za Binadamu UN: Tanzania ichunguze mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi, Lissu na wengine waliokamatwa waachiliwe
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ameitaka Serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mauaji na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu uliofanyika wakati wa Uchaguzi wa Oktoba 29, akieleza wasiwasi juu ya ripoti kwamba miili ya watu waliouawa ilichukuliwa na Vyombo vya Usalama kwenda maeneo yasiyojulikana, na hivyo kuzuia familia kuwazika wapendwa wao.

Türk ametoa wito kwa mamlaka kutoa taarifa kuhusu hatima ya watu waliopotea, kurudisha miili ya waliofariki kwa familia zao ili wazikwe kwa heshima, kuhakikisha wale wote waliohusika na ukiukwaji huo wanawajibishwa na kuwaachia viongozi wa upinzani waliokamatwa, akiwemo mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu na wale wote waliokamatwa kiholela tangu siku ya uchaguzi.

Maoni ya Wananchi:
Wengi wamekubaliana na wito wa UN kuhusu uchunguzi huru na kuwawajibisha wahusika ingawa wengi wameonyesha mashaka wa hilo kufanywa na serikali wakisema uchunguzi huru utafanyika tu endapo timu ya wachunguzi wa nje itatumwa nchini, huku wengine wakisema hili linaweza kuisha haraka ikiwa kutakuwa na shinikizo kutoka nchi za Magharibi.

ACT Wazalendo yatangaza kwenda Mahakamani kudai Ushindi Uchaguzi Zanzibar
Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza mpango wa kuchukua hatua za kisheria kudai ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, wakidai mchakato wa uchaguzi uliharibiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho Vuga, Zanzibar, Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Profesa Omar Fakih, alisema chama hicho kilishinda jumla ya majimbo 32 ya Ubunge, Uwakilishi na Udiwani lakini waliporwa matokeo hayo, na sasa kitaenda mahakamani kufuata taratibu za kisheria ili kurejesha haki yao.

Maoni ya wananchi:
Baadhi wahoji kama Sheria za Zanzibar zinaruhusu kupinga matokeo ya uchaguzi, na wengine wakieleza ni makosa yao tangu mwanzoni kwa kushiriki katika uchaguzi ambao walijua fika hautakuwa wa huru na haki, hivyo waache kuzua taharuki!
 
Back
Top Bottom