Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 14

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 14

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Rais Samia afungua Bunge la 13, atoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhaini, aahidi marekebisho ya Katiba na kutoa wito wa Maridhiano
Rais Samia akihutubia Bunge la 13 leo Novemba 14, 2025, ameanza kwa kutoa pole kwa majeruhi na familia zilizopoteza wapendwa wao katika matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29. Amesema Serikali itatoa msamaha kwa washtakiwa wa kesi za uhaini - waliojikuta wakiandamana ‘kwa mkumbo’.

Pia, ametangaza kuwa ndani ya siku 100 Serikali yake itaanza mchakato wa marekebisho ya Katiba na kuunda Tume ya Maridhiano na Upatanishi, baada ya uchunguzi kubaini chanzo cha vurugu zilizotokea wakati wa Uchaguzi.

Ameongeza kuwa, Tanzania inapenda kuheshimiwa kama inavyoyaheshimu mataifa mengine, na kwamba maridhiano yatafanyika kwa kufuata mila, destruri na tamaduni za Tanzania na sio kwa shinikizo (toka kwa mataifa mengine).

Amewasihi vijana kutotumia njia za vurugu ili kupata majibu ya wanayotaka, akisema kama wao wazazi wangetumia njia hizi basi Tanzania isingekuwa na hali nzuri (neema) kama ilivyo wakati huu.

Pia, Samia ametangaza kuundwa kwa Wizara ya Vijana pamoja na washauri wa masuala ya vijana katika Ofisi ya Rais, huku akisisitiza kulindwa kwa uhuru wa Vyombo vya Habari ili wananchi wapate haki ya taarifa.

Aidha, Rais Samia alisema Watanzania walijitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, na urahisi wa mchakato wa upigaji kura uliwapa waangalizi taswira isiyo sahihi ya mwamko wa wananchi. Amesisitiza kuwa, Tanzania inapenda kuheshimiwa kama inavyoyaheshimu mataifa mengine.

Maoni ya wananchi:
Wengi wa wananchi mitandaoni wameiona hotuba hiyo kama kejeli kwa kutozungumzia suala la uwajibikaji kwa Polisi waliotekeleza mauaji wakati wa maandamano hata kama hotuba imewagusa vijana mpaka kuahidi kuanzisha Wizara mpya kwa ajili yao, wakisema wameikataa pole yake pamoja na wito wake wa maridhiano.

Wananchi wengine wametafsiri hotuba hiyo kama muelekeo mzuri wa kufanikisha kuiondoa serikali wanayodai hawajaichagua madarakani, wakisema imeonesha kuwa Serikali inahangaika kuwatuliza vijana kwa kuangalia namna bora ya kuwashawishi kwa kutoa nafasi za kazi na kuanzisha Wizara ili waonekane wanasikiliza.

Kwa upande mwingine, wapo wananchi walioonesha kusikitishwa kwao kwa kuwa suala la utekaji halikuongelewa kabisa na Rais, wakisema hii inamaanisha suala hilo limepewa baraka na Rais mwenyewe jambo linalowapa sababu zaidi ya kufanya maandamano Disemba 9 ili kuiondoa Serikali ya CCM.

BAKWATA na taasisi za kiislamu zampongeza Rais Samia kwa kushinda Uchaguzi, walaani vurugu
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), likishirikiana na taasisi mbalimbali za Kiislamu, limelaani vikali machafuko ya Oktoba 29, 2025, na kuitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo na wahusika wa vurugu zilizosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Viongozi hao wamesema walihimiza amani kabla ya uchaguzi na kusisitiza kuwa kudai haki hakupaswi kuhatarisha Usalama wa Taifa. Wameiomba Serikali kuwa na huruma kwa waathirika, lakini pia kuchukua hatua dhidi ya waliochochea vijana kuingia kwenye vurugu na kusababisha vifo.

Aidha, wametoa wito wa suluhu na maridhiano kwa maslahi ya taifa bila kuwalinda wahalifu, huku wakimpongeza Rais Samia kwa ushindi wake na kumtakia heri katika majukumu yake.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameonyesha kukasirishwa na tamko hilo wakihoji ina maana BAKWATA hawajui waliosababisha mauaji ya raia mpaka waseme waandamanaji ndio wamesababisha mauaji. Wengine wameikataa hoja ya maridhiano ikiwa wale wote waliosababisha mauaji ya wananchi hawajawajibishwa.

Kwa upande mwingine, wengi wameendelea kutupa lawama kwa viongozi wa dini ya kiislamu wakisema wamekuwa wadini na kumtetea Rais Samia sababu ya uislamu wake badala ya kuangalia taasisi anayoisimamia na kama anawajibika kama Rais ama lah.

Rais Samia amuapisha Waziri Mkuu Mwigulu, amsihi kuepuka vishawishi
Rais Samia amemuapisha Waziri Mkuu Mteule, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Novemba 14, Ikulu-Chamwino Dodoma, ikiwa ni siku moja baada ya uteuzi wake kupitishwa na Bunge akichukua kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Kassim Majaliwa Kassim.

Rais Samia alimtahadharisha kuwa kazi hiyo ni nzito isiyokuwa na nafasi ya urafiki au upendeleo na kumsisitiza kuepuka vishawishi, akitilia mkazo kuwa nafasi aliyo nayo ni kwaajili ya wananchi wote.

Maoni ya Wananchi:
Suala la kumwambia Dkt. Mwigulu aepuke vishawishi limewashangaza wengi huku wakijiuliza je, ni nani atakuwa analengwa kwenye ujumbe huo?

Aidha jambo lingine lililozua mjadala mkubwa ni wimbo wa msanii Mrisho Mpoto (maarufu kama Mjomba) ambao ulikuwa ukisifia ushindi wa Samia, kuwa amepata ushindi wa kishindo na wa heshima Afrika nzima, ambapo wananchi wamehoji ushindi wa heshima kivipi ikiwa wananchi hawakujitokeza kupiga kura na wengi wameuawa wakipinga uchaguzi huo kufanyika?

BBC yathibitisha video za mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania
Shirika la Utangazaji la Uingereza, British Broadcasting Corporation (BBC) limethibitisha baadhi ya video zilizosambaa mitandaoni kuhusiana na mauaji yaliyotokea wiki ya uchaguzi nchini Tanzania baada ya kutumia picha za satelaiti na kulinganisha maeneo husika.

Video hizo zinaonyesha miili ya watu waliopigwa risasi, majeraha katika sehemu mbalimbali za miili yao na vikosi vya usalama vikilenga raia huku madaktari wakithibitisha kuwa hospitali zilizidiwa ambapo. Imeelezwa kuwa baadaye Polisi walikwenda hospitali mbalimbali kuchukua miili ya waliofariki na kwenda nayo kusikojulikana katika wiki ile ya uchaguzi ambako maandamano yalifanyika katika maeneo mbalimbali nchini. Mtangazaji wa BBC amenukuliwa akisema naye aliyashuhudia hayo Namanga, katika mpaka wa Kenya na Tanzania ambapo alikuwa akifuatilia matukio ya uchaguzi.

Hata hivyo, juhudi za BBC kupata mamlaka nchini ili watoe majibu kuhusu tuhuma zilizomo kwenye ripoti hiyo hazikuzaa matunda na wameeleza kuwa wanaendelea kuwatafuta wenye mamlaka kupata upande wao.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameipongeza BBC kwa uthubutu wake kuwasaidia Watanzania kuonyesha ukweli wa yale yaliyotokea wakati wa uchaguzi jambo ambalo vyombo vya ndani vimeshindwa kufanya.

Wengine wameendelea kuihoji serikali pamoja na vyombo vya ulinzi – Je, wataendelea kukana kuwa walioshiriki kwenye maandamano na waliofariki kwenye maandamano sio Watanzania wakati kila siku vithibitisho vinazidi kuwekwa bayana? Wataziba masikio na kufumbia macho haya mpaka lini?
 
Back
Top Bottom