Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania -Novemba 17, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania -Novemba 17, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Lissu aiomba Mahakama Kuu aunganishwe kama mdaiwa kwenye kesi ya Mgawanyo wa Mali za Chama
Mkurugenzi wa Mambo ya Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA, Gaston Shundu Garubindi, kupitia mtandao wa X amesema kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Tundu Lissu, ameomba kuunganishwa kama mdaiwa kwenye shauri namba 8323/2025 kesi ya mgawanyo wa mali za chama kati ya Bara na Zanzibar, lililofunguliwa na Said Issa Mohamed na wenzake dhidi ya Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa chama wakidai kuwa maslahi ya Zanzibar hayapewi kipaumbele ndani ya CHADEMA.

Lissu anataka kuunganishwa kwa kuwa kesi hiyo ilisababisha chama kuzuiwa kufanya shughuli zake za siasa na kutumia rasilimali zake, na maombi hayo tayari yameshasajiliwa huku wito kwa wajibu wa maombi ukisubiriwa ili usikilizaji uanze rasmi baada ya kuwasilishwa Novemba 10, 2025.

Maoni ya Wananchi: Wananchi wamepongeza juhudi za Mwenyekiti wa chama, wakidai kuwa licha ya kuwa gerezani akiwa na kesi ya uhaini, bado anataka kukipambania chama. Wananchi wanaiona hatua hii kuwa inaonyesha dhamira yake ya kutetea maslahi ya chama bila kujali changamoto alizonazo binafsi. Wengine wanasema Lissu ni kiongozi anayejaribu kuonyesha mfano wa uwajibikaji.

Samia atangaza Baraza jipya la Mawaziri. Amteua mwanaye na mkwe wake
Rais Samia ameteua Baraza la Mawaziri na Manaibu Waziri lenye Wizara 27, likiwa na Mawaziri 27 pamoja na Naibu Waziri 29, akifanya jumla ya viongozi 56 waliopewa dhamana za kisekta katika Serikali ya Awamu ya Sita.

Katika uteuzi huo, Rais pia amemteua mwanaye, Wanu Hafidh Ameir, kuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, huku mumewe (mkwe wa Rais) Mohamed Mchengerwa akiteuliwa kuwa Waziri wa Afya. Ridhiwani Kikwete, mtoto wa Rais wa Awamu ya Nne, ameteuliwa kuwa Waziri wa Utumishi na Utawala Bora (inayosimamia Idara ya Ujasusi nchini), huku Paul Makonda (aliyegubikwa na kashfa mbalimbali nchini wakati wa Serikali ya Awamu ya tano hadi kupelekea kupigwa mafuruku kuingia Marekani) akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Pili wa Wizara ya Habari.

Kwa upande mwingine baadhi ya sura maarufu zilizotegemewa kutinga kwenye baraza hilo zimeangukia pua, huku kukitokea minong’ono ya sababu za kuachwa kwao. Miongoni mwao ni aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu na pia Waziri wa Nishati, Doto Biteko, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa (ambaye wakati wa vurugu za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ndiye alikuwa msimamizi wa Polisi na aliyeshiriki kufungia Kanisa la Askofu Gwajima), Hussein Bashe, ambaye alikuwa Waziri wa Kilimo; Dkt. Damas Ndumbaro ambaye alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Jenista Mhagama ambaye alikuwa Waziri wa Afya na aliyekuwa hakosekani katika nafasi za uwaziri kwa kipindi kirefu; Selemani Jafo, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, na Pindi Chana aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Katika hali iliyowashtua wengi, mjumbe wa Kamati Kuu, Ng'wasi Damas Kimani, Binti liyeshawishi wajumbe kumpitisha Samia kuwa mgombea pekee CCM, ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi.

Maoni ya Wananchi: Wengi wamekosoa uteuzi huo wakisema limekuwa baraza la familia badala ya kuteua kwa kufuata vigezo vya kitaaluma na uzoefu wa mtu kwenye nafasi husika kutokana na uteuzi wa mwanaye, mkwe wake (Mchengerwa) pamoja na mtoto wa Rais Mstaafu Kikwete, huku wakikumbushia jinsi nafasi mbalimbali za wabunge zilivyojaa watoto na ndugu wa viongozi.

Wengine bado wameshikilia msimamo wa kutoitambua Serikali hii kutokana na uchaguzi kutokidhi vigezo vya kidemokrasia na kwamba uteuzi huu hauzingatii matarajio ya wananchi.

Aidha, wengine wamesema baraza hili linaweza kuwa baraza la ovyo kati ya yaliyowahi kuundwa kutokana na wengi walioteuliwa kuonekana kutokuwa na vigezo vya kushika nafasi ya uwaziri au unaibu waziri, na kwamba wameteuliwa sababu hawana ‘sauti’ mbele ya Rais.

Mijadala ya udini yaongezeka kwa kasi. Viongozi wa kiislam wailaumu TEC kwa kuikosoa Serikali kuhusu maandamano wakati wa uchaguzi
Mijadala ya kidini imeendelea kushika kasi mitaani na kwenye mitandao ya kijamii baada ya Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na viongozi wengine kutoka dini hiyo kutoridhika na msimamo wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) pamoja na viongozi wa Kanisa Katoliki juu ya Maandamano na vifo viliyotokea wakati wa uchaguzi.

Viongozi hao wa Kiislamu wameikosoa TEC na Kanisa Katoliki wakidai hawana mamlaka ya kuielekeza serikali kufanya jambo lolote huku wengine wakioneshwa kukasirishwa na viongozi hao kuita hali ile iyotokewa wakati wa uchaguzi ‘Maandamano’ badala ya ‘vurugu’ kutokana na uharibifu wa mali uliotokea na vifo wanavyodai vimechochewa na vurugu hizo.

Maoni ya wananchi: Kwa ujumla, TEC imeonekana kupata uungwaji mkono na wananchi kwa kiasi kikubwa kutokana na kuonekana kuwa upande wao pamoja na msimamo wake thabiti unaosisitiza kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana bila haki huku katika upande mwingine viongozi wa dini ya kiislamu wakikosolewa kwa kulifanya suala hili kuwa la kidini badala ya utu na kupigania haki za Watanzania bila kujali imani zao.

Aidha baadhi ya wananchi wamesema ineonakana viongozi wa dini ya kiislamu ni kama wamelipwa ili kusambaza chuki za kidini na kuwatoa wananchi kwenye jambo la msingi la kudai uwajibikaji juu ya mauji yaliyofanyika ili kuwaingiza kwenye vita ya kidini, wakisema hili linathibitishwa na ukimya wa serikali kwenye kuzungumzia suala hili na kukataza uchochezi wa chuki za kidini unaondelea.

Chakwera, ateuliwa na Jumuiya ya Madola kuongoza mazungumzo ya maridhiano nchini Tanzania kufuatia matukio yaliyojiri wakati wa uchaguzi
Rais wa zamani wa Malawi, Lazarus Chakwera, ameteuliwa na Jumuiya ya Madola kuwa Mjumbe Maalum nchini Tanzania kuongoza mazungumzo ya maridhiano kufuatia matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29. Dkt. Chakwera ataongoza juhudi za kupunguza mvutano wa kisiasa na kusaidia katika mazungumzo ya kitaifa, akilenga kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa.

Ziara yake imepangwa kufanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 18 hadi 21 Novemba, 2025. Katika muda huo, Dkt. Chakwera atafanya mashauriano na maafisa wa serikali, viongozi wa vyama vya siasa, makundi ya kijamii, viongozi wa dini pamoja na wawakilishi wa kidiplomasia, ili kuhakikisha mazungumzo yanayolenga suluhisho la pamoja yanafanikiwa.

Maoni ya Wananchi: Wengi wameona kuwa jitihada hizo hazitasaidia chochote kwani wanaamini hakukuwa na uchaguzi wakiamini suluhisho la kumaliza hali hii ya mvutano nchini ni kuundwa kwa ‘Serikali ya mpito’ itakayosimamia mchakato wa Katiba Mpya na kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, ambapo atakayeshinda aongoze nchi, lakini pia kuhakikisha wale wote waliosababisha mauji ya raia wanawajibishwa.

Lema: CCM kutumia dini kutetea makosa yenu si sahihi, nchi inaweza kutuingiza katika mgogoro mkubwa wa kidini
Mjumbe wa Kamati Kuu wa CHADEMA, Godbless Lema, kupitia ukurasa wake wa X ameonya kuwa CCM kutumia dini kutetea makosa yao ni hatari na haiwezekani kuficha uovu nyuma ya dini, akisisitiza kuwa endapo vitendo viovu vitapuuzwa, nchi inaweza kuingia katika mgogoro mkubwa wa uhasama wa kidini, na kuongeza kuwa ni mtu mpumbavu tu ndiye asiyefahamu kinachoendelea nchini.

Maoni ya Wananchi: Wengi wamekubaliana na Lema huku wakionya viongozi wa dini kutumika na wanasiasa katika masuala ya Haki, wakisema hatua kama hizo zinaweza kuleta mgogoro mkubwa wa kidini na kuchanganya jamii badala yake viongozi wa dini wanapaswa kuwa kielelezo cha umoja na heshima na sio kuwatenganisha wananchi.
 
Back
Top Bottom