Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 18, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 18, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Samia aunda tume Kuchunguza ‘Matukio ya Uvunjifu wa Amani’ wakati wa uchaguzi, itaongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande
Rais Samia ameunda Tume ya Uchunguzi kwa ajili ya kuchunguza ‘matukio ya uvunjifu wa amani’ yaliyotokea nchini Tanzania wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, na kumteua Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.

Wajumbe wengine wa Tume hiyo ni Jaji Mkuu Mstaafu Prof. Ibrahim Hamis Juma, Balozi Ombeni Yohana Sefue, Mwanadiplomasia na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Radhia Msuya, Balozi Mstaafu, Lt. Gen. Paul Meela, Balozi na IGP Mstaafu Said Ally Mwema, Balozi David Kapya, pamoja na Dkt. Stergomena Lawrence Tax, aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa SADC pamoja na Waziri wa Ulinzi katika Serikali iliyopita.

Maoni ya wananchi: Wengi wameonyesha kutokubaliana na uteuzi wa tume hiyo, kutokana na kuwa wajumbe walioteuliwa ni viongozi wa zamani ambao ni sehemu ya mfumo wa serikali, wakisema kuwa mhalifu wa matukio hayo (serikali) hawezi kujichunguza, na kwamba kama kweli wangekuwa na nia ya kufanya uchaguzi kwanza ingesemwa bayana kuwa tume hiyo inachunguza kuhusu mauaji yaliyofanywa na vyombo vya ulinzi na kuteua wadau kutoka sekta mbalimbali, ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha uhuru wa tume hiyo.

Wengine wameonyesha wasiwasi wao wa tume hiyo kuchaguliwa kimkakati ili kuwaangushia lawama za ‘vurugu’ hizo wakati wa uchaguzi, wanaharakati pamoja na asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu kwakuwa zimekuwa mwiba kwa serikali pale inapokiuka haki za wananchi na wakati wa maandamano wamekuwa mstari wa mbele kwenye kukemea ukiukwaji wote wa haki za bnadamu uliotokea.

Baadhi ya wananchi wamesema tume hizi huwa ni geresha tu kuonyesha wanafanya wanataka kubadilika na kushughulikia matatizo yanayotokea nchini lakini kiuhalishia zipo kwaajili ya kuwanufaisha watawala pale wanapohitaji kujisafisha kunapokuwa na chukizo kutoka kwa wananchi wakitolea mfano Tume ya Haki Jinai ambayo ilikuja na mapendekezo mazuri ambayo karibu yote hayajafanyiwa kazi.

Aidha, kuna waliokumbushia mauaji ya raia yaliyofanywa na Polisi wakati wa uongozi wa IGP Said Mwema na wengine kukumbushia kuwa Dkt. Tax alikuwa Waziri wa Ulinzi wakati vurugu zinatokea na yeye kama kada wa chama tawala hatarajiwi kuwa mtu huru katika tume.

Samia: Yalitokea wakati wa uchaguzi yametia doa nchi, hatutategemea sana wahisani, tutawekeza nguvu kwenye vyanzo vya mapato vya ndani
Leo Novemba 18, Rais Samia amewaapisha Mawaziri 27 na Manaibu Mawaziri 29 Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma. Samia amesisitiza kuwa dhamana alizowapa ni jukumu la kazi, si nafasi ya kujivunia, akiwataka kufanya kazi kwa kasi na kuwajibika kwa wananchi kutokana na wingi wa ahadi na uchache wa muda wa utekelezaji.

Pia, amewatahadharisha viongozi hao kuwa vurugu na uharibifu uliotokea nchini wakati wa uchaguzi vimetia doa taswira ya nchi na hivyo vitaathiri katika uwezo wa Tanzania kupata mikopo na misaada kutoka taasisi za kimataifa, akisema rasilimali za taifa ni chache hivyo ni muhimu viongozi kujipanga vizuri kusimamia matumizi ya rasilimali zilizopo ndani ya nchi.

Ameongeza kuwa serikali yake haitasubiri kwenda kuomba fedha na kutumia muda mrefu kushawishi wadau wa maendeleo, bali wataanza kufanya kazi na taasisi hizo ‘zitakapomaliza mapingamizi yao’ wataungana nao katikati ili kuendeleza miradi itakayokuwa inatekelezwa.

Maoni ya Wananchi: Baadhi wamesema maneno yake wameonyesha kiburi na kutojutia hata kidogo mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi akijua fika kuwa hakuna wa kumuwajibisha ikiwemo taasisi nje, jambo linaloongeza hasira na motisha kwa wananchi kushiriki maandamano yanayotarajiwa kufanyika Disemba 9 ili kumuondoa madarakani na kuwawajibisha wale wote waliohusika.

Wengine wamesema kuhamia kwenye vyanzo vya ndani inamaanisha wananchi watabebeshwa mzigo wa kodi ili kuendesha miradi hiyo, na ili waepuke hili, suluhisho ni maandamano ya Disemba 9.

CHADEMA: Polisi waachieni wananchama wetu waliokamatwa kinyume cha sheria
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja na bila masharti wanachama, viongozi na wananchi wanaoshikiliwa kinyume cha sheria, na kutoa ufafanuzi kuhusu mahali walipo wale ambao hawajulikani walipo.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia, CHADEMA imesema mamia ya watu wamekamatwa bila kufuata taratibu za kisheria, bila sababu za wazi, na bila kupewa nafasi ya kuwasiliana na familia au mawakili wao, jambo linalokiuka misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria. Chama hicho kimezitaka jumuiya za kimataifa kufuatilia kwa karibu yanayoendelea nchini ili kuhakikisha haki za raia zinaheshimiwa.

Maoni ya wananchi: Wengi wameonyesha kukasirishwa na hali hiyo wakisema nchi ni kama haina Polisi bali kikundi cha wahuni na wauaji wanaofanya kazi maslahi ya kikundi cha watu fulani ambao hawaitakii mema nchi, jambo linazidi kuzorotesha imani ya wananchi kwa vyombo vya usalama.

Aidha, wengine wamesema haya yote yataisha Disemba 9 (siku ambayo maandamano ya amani yasiyo na kikomo, yanatarajiwa kuanza), ambapo wananchi wanaamini wataondoa mifumo yote kandamizi na kupata mipya inayojali maslahi umma.

RC Chalamila afanya ziara kukagua uharibifu kwenye Mwendokasi Mbagala, huduma kurejea Novemba 20
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amefanya ukaguzi maalum katika eneo la Mbagala kutathmini uharibifu wa miundombinu katika mradi wa Mabasi ya Mwendokasi (BRT) uliotokana na maandamano ya Oktoba 29, akieleza kusikitishwa na vitendo vya uharibifu vilivyoathiri huduma kwa wananchi.

Ametangaza kuwa usafiri wa mwendokasi katika njia ya hiyo itarejea Novemba 20 baada ya matengenezo yanayoendelea kukamilika.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kulinda miundombinu ya umma na kueleza kuwa serikali ya mkoa inaendeleza ushirikiano na vyombo vya usalama ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia.

Maoni ya Wananchi:
Baadhi ya wananchi wamehoji mabadiliko ya kauli za uongozi, wakisema awali kulikanushwa kuwepo kwa maandamano wakisema ni vurugu zinazofanya na vijana kutoka nje ya nchi, lakini sasa serikali inathibitisha uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na waandamanaji nchini! Je, wananchi watawaaminije kuwa miundombinu hiyo imeharibiwa na raia na sio polisi waliotekeleza mauaji?

Polisi: MC Pilipili alikufa baada ya kupigwa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limethibitisha kuwa kifo cha mchekeshaji Emmanuel Mathia, maarufu ‘MC Pilipili’ kimetokana na kupigwa, baada ya kufanya uchunguzi wa mwili wake kwa kushirikiana na madaktari. Kamanda wa Polisi, Gallus Hyela amesema kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na alama zisizo za kawaida zinazoashiria kipigo, hivyo uchunguzi rasmi umeanza ili kubaini waliohusika.

Mwili wa MC Pilipili ulifikishwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na wasamaria wema Novemba 16 majira ya jioni, ambapo ilithibitishwa kuwa tayari alikuwa amefariki. Polisi wameomba mtu yeyote mwenye taarifa za siri kuhusu tukio hilo kujitokeza kusaidia uchunguzi.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameonyesha mshtuko, huzuni na hofu kufuatia tukio hilo kuwa mauaji, wakisema matukio ya ‘watu wasiojulikana’ kuteka na kuua watu yameongezeka kwa kasi nchini kwakuwa hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa kukomesha vitendo hivyo.

Aidha wengine wamehoji, kama polisi wameweza kutoa taarifa za kifo cha msanii huyu na kuanza uchunguzi mara moja, nini kinawazuia kufanya hivyo kwa wananchi waliouawa wakati wa uchaguzi kukiwa na madai kadhaa ambayo yanahitaji majibu ya polisi kujua nini hasa kilitokea?
 
Back
Top Bottom