Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 20, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 20, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Samia azindua Tume ya Uchunguzi wa ‘Matukio ya Uvunjifu wa Amani’ wakati wa Uchaguzi, ataka uchunguzi kauli za upinzani, ushiriki wa NGO na madai ya vijana kulipwa kufanya vurugu
Rais Samia amezindua rasmi Tume ya Uchunguzi wa ‘Matukio ya Uvunjifu wa Amani’ wakati na baada ya Uchaguzi, akisema imeundwa kwa mujibu wa sheria inayompa mamlaka ya kuanzisha tume maalum kuchunguza masuala nyeti ya kitaifa. Amesema lengo ni kufanya uchunguzi wa ndani kabla ya kuhusisha timu za nje.

Katika hotuba yake Ikulu Chamwino, Dodoma, Novemba 20, Rais Samia ametaja maeneo makuu ya uchunguzi, yakiwemo: chanzo hasa cha vurugu, madai ya vijana waliotoka barabarani, kauli za vyama vya upinzani, ushiriki wa asasi za kiraia (NGOs) za ndani na nje pamoja na tuhuma za vijana kulipwa na NGO hizo kabla ya maandamano na uhusiano kati ya vyama vya upinzani na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Rais amesema kazi ya tume hiyo ndiyo itakayoweka msingi wa Maridhiano aliyoiahidi ndani ya siku 100 tangu aingie madarakani, na mapendekezo yatakayotolewa yataongoza hatua zitakazofuata. Amebainisha kuwa uchunguzi wa awali unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu, ingawa muda unaweza kurekebishwa kulingana na mazingira.

Maoni ya wananchi: Wengi wamesema kinachoitwa ‘uchunguzi’ ni kama umeshafanyika kutokana na hadidu za rejea alizotoa Rais Samia zikitaja maeneo yote ambayo tume wanatakiwa kuchunguza, kwa maelekezo hayo inamaanisha hawatakiwi kutoka nje ya maelekezo hayo, na kuonyesha tume iliundwa kwaajili ya kukamilisha ratiba na sio kufanya uchunguzi.

Baadhi wamesema, Rais anataka kuua NGO's kubwa nchi ambazo zimekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wananchi na kuhakikisha haki zao za binadamu zinalindwa kwa kusema waandamanaji walilipwa ili kufanya vurugu wakati ni uongo kwani wananchi walitoka kuandamana kupinga mambo kandamizi yanayokiuka misingi ya haki za binadamu na uchaguzi huru.

Aidha, wengine wamehoji ukweli ni upi juu ya kauli ya serikali kuhusu walioandamana? Mwanzo walisema ‘waliofanya vurugu’ ni raia kutoka nje, baadaye wakasema waliokufa ni raia kutoka nje, wakaja kusema walioandamana wengi walifuata mkumbo, na sasa wanasema vijana walilipwa kwaajili ya kufanya vurugu!

Wananchi wanadai hiki ni kiburi kutoka kwa Rais na serikali yake kwa kupuuza na kutosikiliza malalamiko ya wananchi na badala yake wanaamua kutunga uongo ili kusambaratisha malalamiko hayo.

Bunge la Ulaya kuanza mchakato wa kupinga ufadhili wa Tanzania kwa mwaka 2026
Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ulaya, imepitisha uamuzi wa kuanza mchakato wa kupinga mpango wa ufadhili wa Umoja wa Ulaya kwa Tanzania kwa mwaka 2026, baada ya wajumbe 53 kuunga mkono kufuta ufadhili huo (2 wakupinga na 1 akujizuia kupiga kura).

Mwenyekiti wa kikao, David McAllister, alisema kuwa Tanzania imedorora katika kuheshimu haki za binadamu, uhuru wa msingi, demokrasia, utawala wa sheria, utawala bora na uhuru wa kiraia. Alibainisha kuwepo kwa ongezeko la ukandamizaji, kukamatwa kiholela, mashambulizi na vitisho dhidi ya upinzani, watetezi wa haki za binadamu na asasi za kiraia. Alisisitiza kuwa hakuna nchi inayopaswa kupokea ufadhili wa EU wakati inakiuka makubaliano iliyoingia na Umoja wa Ulaya, na kwamba kutoa ufadhili wakati vyombo vya dola vinatumia nguvu kubwa dhidi ya waandamanaji na vitisho vya adhabu ya kifo kwa sauti za upinzani ingekuwa “ishara chanya” isiyostahili kwa Serikali ya Tanzania.

Maoni ya Wananchi: Wananchi wengi wameunga mkono hatua za EU za kusitisha ufadhili kwa Tanzania kutokana na ukandamizaji wa haki za binadamu, ukiukaji wa demokrasia, matukio ya utekaji na watu kuuliwa pamoja na ukandamizaji wa upinzani. Wanananchi wameongeza kuwa baada ya Bunge la Ulaya kuonyesha mfano, huenda wengine watafuatia na inaweza kusaidia kuongeza msukumo kwa Samia na Serikali yake kuwajibika kutokana na matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi.

Baadhi wameonyesha hofu ya kupoteza misaada kutoka Ulaya na nchi nyingine za Magharibi, kupungua kwa mapato ya serikali ambayo itawaathiri zaidi wananchi wa kawaida na kuongeza ugumu wa maisha kwani huenda Serikali ikaja na kodi zitakazokuwa mzigo kwa mwananchi wa kawaida.

Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu yalaani vurugu za uchaguzi. Yawataka vijana wa kiislamu kutoshiriki maandamano ya Disemba 9
Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini ambazo zipo chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) imelaani vikali matukio ya vurugu yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi, ikisema yameleta majonzi na hasara kwa familia, jamii na taifa. Katika tamko lililotolewa Novemba 20 jijini Dar es Salaam ikiwasilishwa na Sheikh Mussa Kundecha, wamesema upigaji kura ulianza kwa amani katika maeneo mengi kisha vurugu zilijitokeza katika baadhi ya maeneo.

Sheikh Kundecha amesema wanaiunga mkono agenda ya maridhiano ya kitaifa iliyoletwa na Rais Samia, lakini akasisitiza maridhiano yasiwe njia ya kuficha uhalifu; wote waliohusika na vurugu wabainishwe na wasio na hatia wapewe ulinzi. Pia, wamehimiza Watanzania kudumisha mshikamano na kuepuka maneno au vitendo vinavyoweza kuchochea mgawanyiko.

Aidha, wamewataka vijana wa kiislamu kukaa nyumbani Disemba 9 na kufanya ibada badala ya kujihusisha na mikusanyiko yenye hatari ya kuzua fujo, na Watanzania kwa kutumia taratibu za kusheria kudai haki zao pale wanapolazimika kufanya hivyo.

Maoni ya wananchi: Wengi yanaonyesha hasira na kukosoa tamko la jumuiya hiyo wakiwatuhumu kutumika na chama tawala pamoja na serikali kuzuia maandamano, wakisisitiza kuandamana ni haki yao ya kikatiba na hawawezi kuwazuia wakitaka kufanya hivyo.

Wengine wanasema matamko ya viongozi wa dini yamekuwa mengi kupita kiasi na inaonekana kama “kampeni”, wakisema hii ni baada ya serikali pamoja na chama tawala kuona hawawezi kuwatumia wasanii kufikisha ajenda zao kutokana na hasira ya wananchi kwao, jambo ambao lihatarisha usalama wa nchi kwa kuzua migogoro ya kidini.

Aidha, wengine wameona tamko hilo kama njia ya kuwapoza wananchi baada ya Wahadhiri wa Kiislamu kusema watawakata vichwa wananchi watakaotoka kuandamana Disemba 9, wakionyesha chuki kubwa ya kidini dhidi ya Wakristo na hasa Wakatoliki.

Kwa upande mwingine wananchi wameendelea kuelimishana na kuhamasishana kutokukubali kuingia kugawanywaa na kuingia kwenye migogoro ya kidini, kwani hilo ndio hasa serikali, Rais na chama tawala wanataka kitokee ili wakwepe uwajibikaji kwenye mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi.

Waziri Mkuu akutana na kufanya mazungumzo na Padri Kitima
Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam, Novemba 20 huku lengo la mazungumzo hayo likiwa halijawekwa wazi.

Maoni ya wananchi: Wengi wamejaribu kukisia kuhusu madhumuni ya mkutano huo, baadhi wakisema serikali imemuita kiongozi huyo ili kusawazisha mvutano wa viongozi kidini unaoendelea kwani unaweza kusababisha madhara makubwa.

Aidha, wengine wamesema huenda jitihada za kufanya maridhiano zimeanza kwa kuwatumia viongozi wa dini wenye ushawishi, wakisisitiza TEC ni watu wa msimamo kuwa hakuna amani bila haki na haki haiji bila uwajibikaji.

CAF yamtunukia Tuzo Rais Samia
Rais Samia ametunukiwa Tuzo Maalum na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kutambua mchango wake katika mchezo wa soka. Tuzo hiyo imekabidhiwa Novemba 19 jijini Rabat, Morocco ilipofanyika hafla ya Tuzo za CAF 2025. Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa serikali, Gerson Msigwa ndio amepokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais.

Maoni ya wananchi: Wengi wameonyesha kejeli juu ya tuzo hiyo wakisema Samia hastahili kupata tuzo hiyo kwa kuwa amekuwa akitumia michezo na hasa soka kushawishi umaarufu wake kwenye siasa ili mashabiki wa michezo wampigie kura. Pia wanasema vitendo vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini vinathibitisha hakustahili tuzo hiyo.

Wawili watekwa katika nyakati tofauti Arusha. Mmoja ni kada wa CHADEMA
Kumetokea matukio mawili ya utekaji katika Jiji la Arusha yakihusisha watu waliovalia kiraia wakiwa wamebeba silaha. Katika tukio la kwanza, Victor Ndibalema (mwanachama wa CHADEMA) alitekwa na watu waliomuondoa kwa nguvu katika gari aina ya Land Cruiser wakidai wanampeleka Kituo Kikuu cha Polisi (Central), lakini alipofuatiliwa na familia pamoja na viongozi wa CHADEMA, hakupatikana katika kituo chochote cha Polisi.

Katika tukio la pili, kijana mwingine alitekwa eneo la ‘Stendi ya Mtei’, jijini Arusha, na watu wenye silaha za moto. Kijana huyo hakupatikana jina lake mara moja.

Maoni ya wananchi: Wengi wamelalamika kuwa wahuni wenye silaha za moto wanateka watu kwa uhuru, huku vyombo vya dola, hasa Polisi, vikishirikiana au kutofanya lolote la kuzuia matukio hayo. Hali hii inaelezwa kuanza kuchukuliwa ya kawaida dhidi ya wananchi na kuifanya Tanzania izidi kuonekana sio sehemu salama tena.

Wengine wamehoji kuhusu vyanzo vya silaha nzito ambazo watekaji wamekuwa wakionekana nazo, wakisema huenda madai ya kontena la sihala kuingizwa nchini na mtoto wa Rais, (Abdul) kwaajili ya ‘kushughulika’ na wakosoaji wa serikali, zilikuwa za kweli.

Aidha, baadhi wametoa wito kwa wananchi kushirikiana kutokomeza matukio haya kwa kuwahsambulia watekaji pale wanapojaribu kuondoka na mtu, badala ya kukaa pembeni na kuangalia wenzao wakitekwa, kwani hakuna aliye salama.

Mpoki: Nilitegemea wakati tunazika, waliomuua MC Pilipili wangekuwa jela
Msanii wa vichekesho, Mujuni Sylivery (maarufu Mpoki), ameishutumu Polisi kwa kwa kutokamata watuhumiwa wa mauaji ya MC Pilipili hadi wakati wanazika.

Mpoki alieleza masikitiko yake kwamba alitarajia watuhumiwa wangekuwa jela wakati wa mazishi, akisema hilo linawezekana kwani imeshashuhudiwa wengine wakikamatwa ndani ya siku moja tu. Ameshangaa kwanini iwe ngumu kwa waliomuua MC Pilipili wakati kuna mtu aliyempigia simu wanayeweza kuanzia uchunguzi kwake!?

Aidha, Mpoki alisisitiza kuwa baadhi ya viongozi walionekana kutokuwa karibu na wasanii wakati wa changamoto akielezea jinsi walivyomkwepa MC Pilipili wakati alipowatafuta kuomba msaada wao. Amewashauri viongozi kupokea simu kutoka kwa wasanii na kutoa msaada badala ya kukaa mbali kwani ni wao (wasanii) waliowasaidia mpaka wamepata nafasi za uongozi walizo nazo.

Maoni ya wananchi: Watu wengi wamemsifia Mpoki kwa ujasiri wa kusema hayo mbele ya umma na kuungana naye kwenye kushangaa kutokamatwa kwa watuhumiwa wa mauaji ya MC Pilipili. Wananchi wameonyesha kutoridhishwa na uwajibikaji wa vyombo vya usalama kwenye matukio ya utekaji na mauaji ya raia wakisema huenda kuna ushiriki wa vyombo hivyo kwenye matukio hayo.

Aidha, wengine wamesema wasanii wanatakiwa kukemea matukio hayo wakati wote na sio tu wakati msanii mwenzao akifanyiwa vitendo hivyo, kwani hakuna aliyekuwa salama hata kama wamekuwa wakitumiwa na serikali kuwashawishi wananchi kuwakubali wasasiasa kwani hata wao wanaweza kutekwa ama kuuliwa ikiwa hawatokuwa na maana tena kwao.

Katika jambo lililowashangaza wengi, ni uwepo wa aliyekuwa Spika wa Bunge, Tulia Ackson kwenye msiba huo. Tulia alisema msiba wa Pilipili umewashtua wengi na kwamba ni funzo kwa watu kuishi vizuri na wengine katika jamii kwani hujui nani atakusindikiza katika safari yako ya mwisho. Wengi wamehoji, hapo ndio Tulia ameshtuka, lakini hakushtuka wakati Polisi walipoua vijana wakati wa uchaguzi? Ameweza kwenda kwenya msiba wa Pilipili lakini kwanini ameshindwa hata kukemea mauaji yaliyofanywa na Polisi wakati wa uchaguzi?
 
Back
Top Bottom