Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 22, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 22, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Mbeya: Polisi wakiri kumshikilia Clemence Mwandambo kwa tuhuma za Uchochezi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema limemkamata mtengeneza maudhui mtandaoni na Mwalimu wa Shule ya Awali ya Mtakatifu Clemence, Clemence Kenani Mwandambo, mkazi wa Uzunguni “A”, kwa tuhuma za kutoa na kusambaza maneno ya uchochezi na uchonganishi kupitia akaunti zake za Facebook na Instagram. Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, Mwandambo alikamatwa jana, Novemba 21, 2025 saa 5:20 asubuhi, na uchunguzi wa Polisi unaendelea ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Awali taarifa zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Mwandambo alichukuliwa nyumbani kwake na watu waliojitambulisha kuwa Polisi wakiwa na silaha za moto, wakamuingiza kwenye gari na kutokomea naye kusikojulikana.

Kabla ya kukamatwa na Polisi, Mwandambo amekuwa akitengeneza maudhui mbalimbali mtandaoni ambayo mengi yanaikaosoa serikali na kuitaka iwajibike. Siku chache zilizopita, alikwenda ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kusajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na kukadiriwa kama mfanyabiashara wa mtandaoni.

Katika mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi, Mwandambo amekuwa mmoja wa watu waliokemea kwa wazi vitendo hivyo na kutaka wote waliohusika wawajibishwe.

Maoni ya Wananchi:
Wananchi wengi wamekosoa mtindo wa ukamataji wa Polisi wakidai unafanana na ule wa watekaji ambao humchukua mtu wakiwa na silaha za moto bila ya kuwa na utambulisho rasmi. Wananchi wamesema pia kuwa Polisi wamekuwa wakitumia nguvu kupita kiasi wakati wa ukamataji, jambo linalofanya waamini kuwa wanaotekeleza matukio ya utekaji huenda ni vyombo vya ulinzi.

Aidha, wengine wamelalamikia ubaguzi unaofanywa na Polisi kwa kukamata watu wanaokosoa serikali na kuwaacha wale wanaoonekana kutenda makosa lakini wakiwa wameelekea upande wa serikali au chama tawala. Wanatolea mfano Sheikh aliyesema watawakata vichwa watakaotoka kuandamana, ambapo wananchi wanadai kama angekuwa ni mpinzani au mwananchi anayekosoa serikali, angematwa haraka na hata kupewa kesi ya uhaini.

Bodaboda na Machinga Dar: Desemba 9 hatufungui biashara
Shirikisho la Vyama vya Madereva Bodaboda na Bajaji pamoja na Uongozi wa Machinga mkoa wa Dar es Salaam wametangaza kutofanya kazi Disemba 9, wakisema wamepata taarifa kuwa wanaotaka kufanya maandamano watatumia maeneo yao ya biashara pamoja na makundi yao kisha wawasingizie machinga na bodaboda kuhusika na maandamano hayo.

Msimamo huo umetolewa katika ‘kongamano la kupongeza hotuba ya Rais Samia aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge la 13 jijini Dodoma’, wakisisitiza kuwa bodaboda, bajaji na machinga wanataka amani na utulivu nchini, kwani vurugu zinazofanywa zinaathiri biashara pamoja na uchumi wao.

Maoni ya Wananchi:
Wengi wameonyesha mashaka kama waliotoa kauli hiyo kweli ni bodaboda, wakisema kama viongozi hao sio CCM, basi wamepewa maagizo na viongozi wa CCM ili kuwatisha wananchi wanaotaka kuandamana Disemba 9. Wanadai kundi hilo (madereva bodaboda na bajaji pamoja na machinga) limekuwa likitumika vibaya na wanasiasa kueneza proganda za wanasiasa inapotokea kuna upinzani kutoka kwa wananchi ili kuonyesha watu wengi kwenye jamii wana maono sawa na serikali.

BoT: Wananchi kuweni makini, kuna ongezeko la fedha bandia
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi kuongeza umakini kutokana na ongezeko la matukio ya ukamataji wa fedha bandia kwa asilimia 32.4 (kutoka 105 mwaka 2023 hadi 139 mwaka 2024), ikisema watengenezaji sasa wanatumia mbinu za kisasa.

Ikumbukwe kuwa, wakati wa kampeni zilizuta taarifa kuwa BoT wamechapisha pesa nyingi kwaajili ya chama tawala kutumia fedha hizo kuwahonga wananchi ili wamchague Samia pamoja na wagombea wengine wa CCM, madai ambayo yalikanushwa na BoT.

Maoni ya Wananchi:

Wengi wamesema huenda madai ya pesa kuchapichwa kwa makontena yalikuwa ya kweli, na fedha hizo zilizochapishwa ndio hizi ambazo sasa wanasema ni bandia. Hii imepelekea wananchi kusema mbali na kuchapisha fedha hizo bandia, huenda walifanya kosa jingine la kuzisambaza mtaani na sasa wamekuja kugeuza maneno kuwa ni wahalifu ndio wamefanya hayo!
 
Back
Top Bottom