Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 24, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 24, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Wakfu wa Thabo Mbeki wasema Tanzania Haina Serikali Halali Baada ya Uchaguzi Mkuu, yasisitiza mazungumzo ya wazi

Wakfu wa Thabo Mbeki umetoa taarifa ukieleza kwa masikitiko makubwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29, 2025 haukutimiza kanuni za kidemokrasia, baada ya waangalizi wa SADC na AU kubainisha kuwa uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki na hivyo matokeo ya urais na ubunge yaliyotangazwa na INEC hayakuakisi mapenzi ya Watanzania ikihitimisha kwamba utawala uliopo umewekwa madarakani kupitia mchanganyiko wa nguvu na ulaghai.

Taarifa hiyo, imetoa pole kwa waliopoteza wapendwa wao na kuombea majeruhi wapone haraka, ikieleza kuwa hali hiyo inaacha Tanzania bila serikali inayotambulika kama halali.

Aidha, taasisi hiyo imeitaka Tanzania kuanzisha mazungumzo ya kitaifa, ya wazi, huru na jumuishi ikiamini kwamba hii ndio njia pekee itakayoweza kuleta uponyaji wa kweli, ambapo taifa kwa pamoja linatakiwa kujibu maswali mawili muhimu; Nini kilienda vibaya, na nini kifanyike ili kuirudisha nchi hii inayopendwa na wengi kwenye njia sahihi. Pia imesisitiza umuhimu wa kutimiza wajibu huu kwaajili ya wananchi, Hayati Julius Nyerere na kama mfano wa Waafrika wenzao wote barani.

Maoni ya wananchi:
Wananchi wengi wamesema taarifa ya Wakfu wa Thabo Mbeki umeungana na maoni ya Watanzania wengi kuhusu mambo yaliyokuwa yakipingwa na kutaka yabadilishwe, kukomeshwa na mengine kuboreshwa ili kuleta misingi ya haki, uwajibikaji, uhuru na demokrasia ya kweli nchini.

Wengine wameeleza kuwa mateso, vifo na ukandamizaji uliotokea wakati wa uchaguzi hauwezi kusahaulika bila hatua za haki na uwajibikaji kuchukuliwa, na kusisitiza kuwa hawaitambui serikali iliyopo madarakani, wakitaka mchakato wa Katiba Mpya uanze na uchaguzi mwingine wa huru na wa haki kufanyika.

Aidha, wengine wameonyesha umuhimu wa taasisi za kimataifa kuendelea kushinikiza uwajibikaji ufanyike, kwani hiyo inaweza kuwa namna pekee ya kupata uwajibikaji wa kweli na kurejesha amani nchini.

Wakili aliyekuwa akiwatetea watuhumiwa 93 wa kesi ya uhaini wakati wa uchaguzi mkoani Mwanza afariki ghafla

Wakili Beatus Linda, aliyekuwa akiwatetea watuhumiwa 93 waliokamatwa kipindi cha uchaguzi mkoani Mwanza, amefariki dunia ghafla muda mfupi baada ya kulalamika maumivu ya miguu na tumbo.

Siku chache kabla ya kifo chake, yeye pamoja na mawakili wenzake wa chama cha mawakili - Tanganyika Law Society (TLS) waliweka pingamizi mahakamani kuzuia maombi ya Jamhuri ya kubadilisha hati ya mashtaka ili kuongeza tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha na uharibifu wa mali kwa washtakiwa.

Maoni ya wananchi:
Wengi wameonyesha masikitiko yao na kumwelezea Wakili Linda kama shujaa kwa kuwatetea wananchi waliokuwa wakipigania haki ambao ni dhahiri walipewa kesi za uongo katika jitihada za serikali kukimbia uwajibikaji kutokana mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi. Wanasema kifo chake ni pigo kubwa kwa jamii pamoja na watetezi wa haki za binadamu, huku ikisemakana kilichochukua uhai wake ni sumu.

DPP awafutia mashtaka watuhumiwa 104 wa kesi ya uhaini Dar Es Salaam na Mwanza

Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jijini Dar es Salaam na Mahakama ya Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza zimewaachia huru jumla ya watuhumiwa 104 wa kesi za uhaini waliokamatwa kufuatia vurugu za baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha ombi la kutokuendelea na mashitaka dhidi yao.

Jijini Dar es Salaam, watuhumiwa 47 kati ya 48 walifutiwa mashtaka na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalo huku jijini Mwanza, watuhumiwa 57 wa shauri namba 26641/2025 wakiachiwa huru katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Buswelu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Stella Kiama.

Maoni ya Wananchi:
Wengi wamesema wananchi hao walibambikiwa kesi na serikali ili wauaji wakimbie kuwajibika na hivyo ni sawa kusema serikali haijafanya chochote na hawana sababu ya kuipongeza au kufurahia wananchi wao kuachiwa sababu hawakutakiwa kuwakamata tokea mwanzoni!

Wengine wamesema hii ni mbinu ya serikali kujionyesha ina huruma na inawajali wananchi wake kwa kutengeneza tatizo na kulitatua ili waonekane bora, ikitajwa kama matumizi mabaya ya rasilimali za umma na kuwachelewesha wananchi katika kufanya mambo ya msingi.

Mwigulu: Tume ya Uchunguzi ni kwa Maslahi ya Watanzania, Kanisa la Ufufuo na Uzima lifunguliwe, Sherehe za Uhuru kutofanyika

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema uharibifu wa miundombinu uliotokea wakati na baada ya uchaguzi unapaswa kuwa funzo kwa taifa, akisisitiza kuwa miundombinu hiyo ni matokeo ya kodi na kujinyima kwa wananchi, si mali ya serikali.

Akiwa katika ziara jijini Dar es Salaam Novemba 24, alionya kuwa kuchoma au kubomoa mali za umma ni sawa na kuharibu mali ya wananchi wenyewe na kwamba rasilimali za nchi zitalindwa kwa gharama yoyote.

Aidha, alitangaza kuwa Rais Samia ameagiza Sherehe za Uhuru kutofanyika mwaka huu na fedha zilizopangwa kugharamia sherehe hizo zitumike kukarabati miundombinu iliyoharibiwa wakati wa uchaguzi.

Katika hotuba hiyo, Dkt. Mwigulu alisisitiza pia umuhimu wa tume ya uchunguzi kuhusu matukio ya wakati na baada ya uchaguzi, akibainisha kuwa imeundwa kwa maslahi ya kitaifa, ambapo imejaa ‘wazee wenye heshima na uzoefu mkubwa’.

Aliitaka jamii kutoa ushirikiano kwa tume hiyo kwa kutoa ushahidi na taarifa zitakazosaidia kupata ukweli, huku akimuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani kulifungulia Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima na wapewe masharti ya uangalizi ndani ya miezi sita akisema kukosea kwa taasisi moja hakupaswi kupelekea kufungiwa kwa taasisi zote. Pia, ameagiza taasisi nyingine zilizokuwa na shida zipewe miezi sita ya uangalizi. Kwa taasisi nyingine za dini, Mwigulu ameagiza ziandikiwe kukumbushwa miiko ya ufanyaji kazi na masharti.

Maoni ya wananchi:
Wengi wamehoji wanamsamehe Askofu Gwajima kwani alifanya kosa gani? Je, kuishauri serikali juu ya mambo ya kitaifa imekuwa kosa la mtu kufungiwa makanisa yake yote? Lakini, kama kesi iko mahakamani Waziri Mkuu ana mamlaka gani ya kuingilia na kutoa amri makanisa hayo yafunguliwe? Wakiongeza kuwa hii ni mbinu ambayo serikali inaitumia kwa kutengeneza tatizo na baadaye kuja kulitatua ili waonekane wema.

Kwa upande mwingine, wananchi wamemsihi Gwajima kuendelea kukaa mafichoni wakisema serikali inatumia mbinu ya kufungulia makanisa yake ili ajitokeze waweze kumteka na kutokomea naye pasipojulikana na mbaya zaidi wanaweza wakamuua wakitolea mfano jinsi aliyekuwa Balozi wa Cuba, Humphrey Polepole, alivyotekwa.

Aidha, wengine wamesema nchi haijapata uhuru bado hivyo hakuna haja ya sherehe siku ya Disemba 9, badala yake siku hiyo ndio itakuwa siku ya kweli wa ukombozi wa Tanganyika kwa wananchi kutoka na kuandamana na kuirudisha nchi mikononi wa mwa Watanganyika.

Mtangazaji Clouds TV: Pongezi za Msigwa kwa Waandishi hazinihusu, tuache unafiki!

Wakati wakizungumza kwenye kipindi cha ‘Power Breakfast’, watangazaji wa Clouds walijadili sifa zilizotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Novemba 23, 2025 kwa wanahabari kuhusu kufuata maadili na weledi wa uandishi kwa kutoripoti kusu mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi.

Sam Sasali alisema pongezi hizo hazimuhusu, kwasababu wengi hawakuripoti matukio hayo kwasababu ya uoga akisema yeye binafsi hakuripoti kwasabu ya “Trauma” kutokana na kusababisha chombo hicho kufungiwa kurusha matangazo yao kwa kipindi fulani na kusema asingekuwa anahofia chombo hicho kufungiwa tena au angekuwa nje ya nchi basi angeripoti matukio hayo bila kificho akitania “Ningeweka satelaiti juu” ili aweze kupata matukio yote yaliyotokea kwa uzuri.

Maoni ya Wananchi:
Wananchi wengi wamesema kwa kauli hiyo ya Sam inaonesha hata waandishi wamechoka namna serikali imekuwa ikiingilia uhuru wa habari na kuzuia haki ya wananchi kupata taarifa lakini hawasemi kutokana na hofu ya kupoteza kazi zao, kutekwa na kuuliwa au vyombo vyao kufungiwa hivyo wanajikuta hawana jinsi bali kukaa kimya au kuungana na serikali kuwakandamiza wananchi.
 
Back
Top Bottom