Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 28, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania - Novemba 28, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Ridhiwani Kikwete: Nipo tayari kuhojiwa kuhusu tuhuma za vituo vya Lake Oil. Wenye ushahidi wapeleke

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Ridhiwani Kikwete amesema yuko tayari kuhojiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufuatia tuhuma zinazoelekezwa kwake kuhusu umiliki wa vituo vya mafuta vya Lake Oil.

Akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo juzi tarehe 26 Novemba 2025, Ridhiwani alisema kuwa ni muhimu taarifa za viongozi wa umma ziwe wazi ili panapotokea sintofahamu pawepo na uchunguzi wa wazi kwa maslahi ya umma. Alisema malalamiko dhidi ya Maadili ya viongozi yamekuwa mengi, akitolea mfano maandamano ya Oktoba 29 ambapo vituo vya Lake Oil, vinavyodaiwa kumilikiwa na mtu aitwaye Ally Edha Awadh, vilichomwa moto kwa madai kwamba ni mali yake Ridhiwani. Ameishauri tume hiyo kumuita na kumhoji bila hofu, na kupendekeza ifanye uchunguzi wa awali kisha iitishe mkutano na waandishi wa habari ili kutoa taarifa rasmi na kukusanya ushahidi wa ziada kutoka kwa wananchi.

Maoni ya wananchi: Wengi wamesema hayo ni maneno tu ili ajionyeshe kuwa ana nia ya kufanyiwa uchunguzi lakini ukweli ni kwamba hawezi kuruhusu hilo lifanyike, wakisema kama angekuwa na hata chembe ya maadili basi angemwomba Rais Samia radhi kuwa hawezi kuapa kuwa Waziri Mtendaji wa Maadili na Utawala Bora ilhali akiwa mtuhumiwa.

Wananchi wanasema alitakiwa kupisha uchunguzi wa Tume ya Maadili ufanyike, ikibidi hata watu kutoka nje ili kuondoa mgongano wa kimaslahi, yeye kubaki kama Waziri huku wa chini yake wakitakiwa kumchunguza inazua maswali mengi, kuwa kitakachofanyika hapo ni kukamilisha ratiba tu tena kwa nia ya kutaka kujisafisha kupitia tume.

Aidha, wengine wamejadili kuhusu sintofahamu kwenye takwimu za vituo vya mafuta vilivyoathirika ambapo Ridhiwani amenukuliwa akisema mmiliki wa vituo vya Lake Oil alimwambia zaidi ya vituo vyake 90 vilichomwa moto, huku katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kampuni hiyo ikitaja vituo 38, wakati Umoja wa Wamiliki wa Vituo ya Mafuta Tanzania (TAPSOA) kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wa TAPSOA, Novemba 07 akizungumza na waandishi wa habari alisema kwamba vituo 41 (Lake Oil 38) viliathirika kwa kuchomwa moto nchi nzima!

Wananchi wanaona kuwa huenda serikali inapika takwimu ili kuangusha lawama kwao kwa lengo la kukwepa uwajibikaji na kuyapa maandamano picha mbaya ili kuwa na sababu ya kuyazuia kabisa siku za mbeleni.

Serikali: Tanzania haitakufa njaa kwa kukosa fedha za EU

Baada ya Bunge la Ulaya kupitisha azimio la kusitisha kuipatia Tanzania Tsh. Bilioni 400 zilizotarajiwa kufadhili miradi ya maendeleo mwaka 2026, Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, imesema inafuatilia suala hilo kupitia Balozi wake aliyehudhuria mjadala huo nchini Ubelgiji na kwamba itatoa kauli rasmi baada ya kupokea taarifa kamili, huku akisisitiza kuwa Watanzania hawatakufa wala kukumbwa na tatizo lolote kubwa, akibainisha kuwa nchi ina bajeti yake na vyanzo vingine vya mapato.

Amesema, Tanzania hailazimiki kutekeleza maagizo ya Bunge la Ulaya kwa kuwa uhusiano unasimamiwa na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, na amewataka Watanzania kupuuza taarifa zinazoonesha azimio la Bunge la Ulaya kama masharti ya lazima. Wizara hiyo baadaye ilitoa msimamo wa nchi, ambao haukuwa tofauti na kile alichokisema Waziri, ikisisitiza kuwa Tanzania hailazimiki kutelekeza maagizo ya Bunge hilo kwani kila upande una mipaka wa wigo wa mamlaka yake.

Aidha, Serikali ilikutana na Jumuiya ya Wanadiplomasia wanaowakilisha mataifa na taasisi na kuwahakikishia ushirikiano wa Tanzania na mashirika wanayowakilisha. Kupitia mkutano huo, Serikali ilitoa pia maelezo kuhusu zoezi la uchaguzi, ‘vurugu’ zilizotokea na hatua zilizozofuata ikiwemo kuunda Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais Samia kubaini chanzo cha vurugu na kupata mapendekezo ya kuimarisha mifumo ili yaliyotokea yasijirudie.

Maoni ya Wananchi: Wengi wamekosoa kauli hiyo wakisema imejaa kiburi na kejeli, na kuonyesha kuwa Tanzania haina mpango wa kuwajibika kwa yaliyotokea wakati wa uchaguzi ndio maana hawajishughulishi kurekebisha mahusiano na nchi nyingine huku ikitafuta kuungwa mkono na nchi nyingine ambazo hazijaonyesha kushtushwa na yaliyokea.

Wengine wameshangaa uelewa wa viongozi wanaoendesha Wizara pamoja na wanaomshauri Rais, kwa kushindwa kuchukulia azimio la Bunge la Ulaya kama kengele ya hatari inayoweza kuathiri Tanzania vibaya ikiwa nchi nyingine zitafuata nyayo zao. Wanasema huu ni mwanzo tu, maazimio zaidi kutoka nchi na taasisi nyingine yanaweza kuja huku taswira ya nchi ikizidi kuharibika na kuwa chanzo cha kuwakosesha wananchi fursa za kimataifa na hivyo kuongeza umasikini na hali ngumu ya maisha.

Kesi ya Viongozi wa CHADEMA kuidharau amri ya Mahakama yatupiliwa mbali

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya Said Issa Mohamed aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar na wenzake wawili dhidi ya viongozi waandamizi wa CHADEMA akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Bara, John Heche, wakidai kukiukwa kwa amri ya Mahakama Kuu ya Juni 10, 2025 katika kesi ya madai namba 8960/2025 inayohusu marufuku ya chama kujihusisha na shughuli za kisiasa na kiutendaji.

Jaji Awamu Mbagwa, akitoa uamuzi, amesema Mahakama imekubaliana na pingamizi la upande wa utetezi likisema Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo kwa kuwa yaliwasilishwa nje ya muda kisheria; ameeleza kuwa waleta maombi wanadai Heche alihutubia Juni 17, lakini maombi ya kudai kudharau amri yamewasilishwa Oktoba 03 siku 106 baadaye ni kinyume na sheria inayotaka maombi ya aina hiyo kuwasilishwa ndani ya siku 60.

Maoni ya wananchi: Wengi wameona hili kama namna ya mahakama kuwapoza wananchi kwa kuonyesha kuwa wanatenda haki na hivyo kupunguza ari ya wananchi kushiriki kwenye maandamano mengine, wakisema hawadanganyiki. Aidha wengine wameichukulia kesi hiyo kama mbinu ya kuendelea kukipotezea muda chama cha CHADEMA kisifanye mambo ya msingi pamoja na kupata nafasi ya kuwashawishi wananchi kudai haki.
 
kwa watanzania ni haya yafuatayo;
1.Ni nani aliagiza watu wapigwe risasi na kuuawa vile?
2.Wapigaji risasi wale ni wakina nani na wapo wapi?
3.Ni kwanini uchaguzi ufanyike kwa namna OVU kwa kiwango kile?
4.Watu waliokufa wapo wapi?
5.Wataongozaje taifa la watu wasiowataka?
6.Ni nani anayeteka na kuua watanzania?
Waliotekwa wapo wapi?

Haya maswali wayatafakari na wayazingatie

"MAMAA AMKA, AMKA MAMAAA" sauti hii ikinijia machozi yanashuka.
Eeee Mungu shusha pigo lako.
 
Back
Top Bottom