Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania: Novemba 7, 2025

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania: Novemba 7, 2025

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
Watanzania 463 Wakabiliwa na Mashtaka ya Uhaini, Unyang’anyi kwa kutumia silaha - akiwemo Mfanyabiashara Jenifer Jovin (Niffer)

Jamhuri imewafungulia kesi Watanzania 240 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Ijumaa Novemba 7, 2025, wakikabiliwa na mashtaka matatu ya uhaini; la kwanza likiwa ni kudaiwa kupanga njama za kutenda uhalifu wa uhaini, la pili (ukimtoa Niffer) ni kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025 na kufanya vurugu zilizosababisha uharibifu wa mali za umma na shtaka la tatu likiwa linamhusu Niffer pekee akidaiwa kuhamasisha watu kuvuruga uchaguzi huo na kuwahimiza kununua barakoa za kuzuia mabomu ya machozi kutoka dukani kwake.

Aidha washitakiwa wengine 172 ni kutoka Mwanza, 42 wapo katika mkoa wa Dodoma na watu 9 wakitoka Makambako mkoani Njombe huku idadi hiyo ikisemekana inaweza kuongezeka kama na mikoa mingine ambako maandamano yalifanyika itajumuishwa pia.

Maoni ya wananchi
Wananchi wengi wameonyesha harisa yao na kutoridhishwa na hatua hiyo ya serikali, ikionekana kwa vijana hao wanatumika kama njia ya kukwepa uwajibikaji na kuwaacha wale waliofanya mauji huru kuendelea kutekeleza unyama wao.

Wengine wamesema kosa la Uhaini sasa linachukuliwa kiwepesi tu kiasi kwamba hata mtu akiiba kuku anaweza kupewa kosa hilo mradi maoni yake yanakinzana na serikali.

Aidha wengine wamesema kwa jinsi serikali na polisi wanakabiliana na suala la maandamano inaonekana dhamira yao ilikuwa ni kuua raia wasio na hatia ambao wamekuwa wakiweka upinzani kwa serikali kwa lengo la kuendelea kubaki madarakani.

Jeshi la Polisi latangaza msako mwingine wa waliohusika na maandamano; yumo Askofu Gwajima pamoja na Viongozi Waandamizi wa CHADEMA

Jeshi la Polisi limeendelea na operesheni yake ya kukabiliana na watu wanaodaiwa kuandaa na kutekeleza vurugu, uharibifu wa mali na uvunjifu wa amani wakati wa maandamano yalifanyika Oktoba ambapo mbali na vijana waliokamatwa katika mikoa mbalimbali limetoa taarifa ya kufanya msako mkali kuwakamata Askofu Josephat Gwajima (CCM), na viongozi waandamizi wa CHADEMA; John Mnyika, Brenda Jonas Rupia, Godbless Lema, Machumu Kadutu, Deogratius Mahinyila, Boniface Jacob, Hilda Newton, Award Kalonga, na Amaan Golugwa.

Polisi imewataka waliotajwa kujisalimisha mara moja katika vituo vya polisi vilivyo karibu na kuonya kuwa yeyote atakayepanga au kutekeleza vitendo vya uhalifu hawatasita kuchukuliwa hatua za kisheria.

Maoni ya wananchi
Wengi wameonyesha hasira yao na kukosa imani na taasisi za dola, wakidai kuwa hatua ya polisi kuanza kukamata viongozi wa upinzani badala ya kuwachunguza waliotumia nguvu kupita kiasi na kuua wananchi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 2,000 ni kuendeleza ukandamizaji huku wengine wakisema hali hii inaashiria kurudi nyuma kwa misingi ya haki na demokrasia kwa kukamata waandamanaji badala ya kuchukua hatua dhidi ya walioua raia.

Baadhi ya wananchi wamesema serikali inatafuta ‘wachawi nje ya genge la wachawi,’ wakimaanisha kuwa inatupa lawama kwa wapinzani ilhali vyombo vya usalama ndivyo vilivyosababisha vifo vya raia.

Wengine wamekosoa kutajwa kwa Gwajima kwenye orodha hiyo, wakiona kama ni jaribio la kuonyesha usawa wa kisiasa usiokuwa wa kweli ukizingatia Gwajima mara zote amekuwa akiishauri serikali juu ya uthabiti na kujitegemea kwa vyombo vya dola ili kufanya maamuzi ambayo yatakuwa hayaingiliwi na Rais na kukomesha matukio ya utekaji na ukatili wa polisi. Kauli nyingi zimebeba kejeli, hasira na masikitiko, huku wachache wakionya kuwa hatua hii inaweza kuchochea zaidi hasira za wananchi na kusababisha maandamano mapya.

Vilevile, baadhi wameeleza kuwa serikali inajaribu kutengeneza hofu ili kuzuia maandamano yanayoratibiwa na vijana (Gen Z), na kwamba kesi za uhaini na uhalifu zimekuwa silaha ya kisiasa dhidi ya wakosoaji.

Mwananchi Enock amshauri RC Mtaka aishauri Serikali kuacha kupuuza haki na madai ya Watanzania ili kurejesha amani na kuponya mioyo

Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Enock, mkazi wa Makambako mkoani Njombe, katika mkutano wa wafanyabiashara na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, uliofanyika Novemba 6, 2025, ameitaka Serikali kutokupuuza haki na madai ya Watanzania ili kurejesha amani na kuponya mioyo ya waliopata changamoto wakati wa uchaguzi.

Amesisitiza umuhimu wa kuandaliwa mazingira bora kwa vijana, akilaani vifo vya vijana vilivyotokea wakati wa maandamano, na kuonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya Haki, Amani na Uhuru, hivyo ana haki ya kuzungumza kwani hajatukana, huku akionya kuwa kupuuza malalamiko ya wananchi kunadhoofisha amani na kuathiri mustakabali wa vijana.

Maoni ya Wananchi
Wengi walimpongeza Enock kwa ujasiri wake wa kusema ukweli mbele ya Mkuu wa Mkoa na kwa hoja nzuri ambazo waliziunga mkono wakisema amewawakilisha vema vijana na kuwa sauti ya wengi walioathirika kwenye maandamano.

Ingawa wengie walionyesha hofu juu ya usalama wake hata kama Mkuu wa Mkoa aliwataka wananchi kwenye mkutano huo kuongea kwa uhuru na kuhahakisha kila mtu kuwa salama. Hii ikitokana na mwenendo wa matukio ya utekaji na watu kupotezwa hata kama serikali na vyombo vya ulinzi kuhakikisha kuna usalama.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ajiapiza kumkamata Mange kwa kuchochea Maandamano ya Oktoba 29

Mwanasheria Mkuu Mpya wa Serikali ya Tanzania, Hamza Johari, amesema serikali inajipanga kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwanaharakati anayeishi Marekani, Mange Kimambi, kwa kile alichodai kuwa ni matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika kuchochea maandamano nchini.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa, Novemba 5, jijini Dodoma, Hamza alimwambia Muendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) waangalie kama kuna Mkataba (Extradition Agreement) na Marekani ili Mange arejeshwe nchini akisema hawezi kuwa anatamba baada ya kusababisha maafa nchini kutokana na maandamano.

Maoni ya wananchi
Kauli hii imechukuliwa kwa hasira na wananchi wengi ambao wamesema kuwa kama taifa hilo suala la Mange halipaswi kuwa kipaumbele kwani kuna mambo mengi ya msingi ya kufanya, huku wakibainisha mashaka yao na uteuzi wakisema Hamza hana elimu rasmi ya uwakili ya kumfanya awe Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hoja nyepesi anazotoa zinazidi kuthibitisha kuwa hafai kushika nafasi hiyo.

Waangalizi wa Uchaguzi wa Kimataifa na Kikanda wakosoa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, wasema haukuwa Huru na Haki, wapendekeza mabadiliko

Ripoti za waangalizi wa kimataifa na kikanda (AU, SADC, EU, EAC, EFC-SADC) zimekosoa uchaguzi mkuu wa Tanzania uliofanyika Oktoba 29, zikieleza kuwa haukufuata misingi ya kidemokrasia na kubainisha kasoro mbalimbali walizoziona kama vurugu, vitisho, masuala ya utekaji, vifo, uminywaji wa mitandao ya kijamii na intaneti, ukosefu wa uwazi, na upendeleo kwa chama tawala.

Waangalizi hao walibainisha pia ukandamizaji wa upinzani, ukosefu wa uhuru wa vyombo vya habari, na changamoto kwa waangalizi wenyewe katika kupata taarifa, wakitoa wito wa mageuzi ya kisiasa yatakayohakikisha uchaguzi huru na haki.

Maoni ya wananchi
Wananchi wengi hawakuwa tofauti na kile kilichoripotiwa na waangalizi hao, wakieleza huenda huu ni uchaguzi mbaya kabisa kuwahi kufanyika nchini mpaka sasa kutokana na kugubigwa na mauji na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kilichowashangaza sana wengi ni ushindi wa Rais Samia wa 98% huku maeneo mengi nchini wakiwa wamejitokeza kwa uchache au kutotokea kabisa kupiga kura. Wengine wamehoji, ripoti za wasimamizi wote wa nje zimekosoa uchaguzi huo, bado serikali itaendelea kupuuza na kuhalalisha uchaguzi huo?

Tulia Ackson ajiondoa kugombea Uspika wa Bunge, atabariwa kuwa Waziri Mkuu

Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Tulia Ackson, ametangaza rasmi Novemba 7, 2025, kujiondoa katika kugombea nafasi hiyo ingawa sababu za kujiondoa kwake hazijawekwa wazi.

Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, Tulia alikuwa kwenye nafasi hiyo ya Uspika wa Bunge baada ya Hayati Job Ndugai kujiuzulu, Tulia akiwa Naibu Spika.

Maoni ya wananchi
Wananchi wamekuwa na maoni tofauti, baadhi wakisema kuna uwezekano anaenda kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu na wengine wakisema moyo unamsuta kutokana na yaliyotokea kwenye maandamano yaliyofanyika kwenye uchaguzi yakionesha kuwa chama hiko na yeye kama mgombea hawakubaliki na wananchi.

Aidha, wengine wamesema anenda kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kutokana na uzoefu wake kwenye masuala ya kidiplomasia na baadhi wakihisi huo ni mkakati wa kuwafanya wananchi waache kujadili masuala ya msingi yanayoendelea wakati huu.

Musiba: Malalamiko yote ya Tundu Lissu na CHADEMA kuhusu uchaguzi ni sahihi
‘Mwanaharakati huru’ Cyprian Musiba, aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Mwibara mkoani Mara kupitia ACT-Wazalendo, amesema malalamiko yote ya Tundu Lissu na chama cha Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu changamoto za kwenye chaguzi ni sahihi, akisisitiza kuwa mfumo wa sasa wa kikatiba unafanya iwe vigumu kwa vyama vingine kushinda dhidi ya chama tawala.

Akizungumza Novemba 07, 2025, Musiba alisema kwamba bila mabadiliko ya kikatiba, itakuwa vigumu kuiondoa CCM madarakani kwa njia ya ushindani wa haki, na akahimiza uwazi katika majadiliano ya mabadiliko ya Katiba yanayoweza kuimarisha demokrasia.

Maoni ya wananchi
Wananchi wamekuwa na maoni tofauti juu ya hili. Baadhi wamesema mwanaharakati huyo ni mnafiki, wakihoji kwani alipokuwa CCM hakuona changamoto za uchaguzi? Kwanini hakusema wakati huo na aje kusema sasa wakati mfumo umemtema? Wengine wameona kama ni maigizo ya kuwatoa wananchi kwenye mambo ya msingi. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameonyesha matumaini kuwa Watanzania siku za usoni wataanza kuongea kwa lugha moja na kupelekea mabadiliko ya kweli.
 
Back
Top Bottom