Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania: Novemba 9

Muhtasari wa Matukio Muhimu Tanzania: Novemba 9

JF Summary

Senior Member
Joined
Jul 3, 2015
Posts
163
Reaction score
109
ACT Wazalendo: Serikali ya Rais Samia imekosa uhalali wa kisiasa kuendelea kuongoza Tanzania
Chama cha ACT Wazalendo, kupitia kikao chake cha Kamati ya Uongozi Taifa kilichofanyika Oktoba 7, kimelaani vikali Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, kikisema ulikuwa na udanganyifu, vurugu, na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kimeituhumu Serikali ya Rais Samia na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kupanga matokeo, kukandamiza wapinzani, na kuhusika katika mauaji ya wafuasi wake, ikiwemo kifo cha mgombea udiwani Dafroza Jacob wa Tarime.

ACT imeitaka Serikali kuwaachia huru wote waliokamatwa, kuunda tume huru ya kuchunguza uchaguzi huo na matukio yaliyosababisha vurugu, pamoja na kuanzisha Tume ya Maridhiano ya Kitaifa kwa ajili ya kudumisha umoja wa taifa. Pia imetaka mageuzi ya Katiba na Tume huru ya Uchaguzi ili kuhakikisha uhuru wa kisiasa na haki kwa vyama vyote.

Maoni ya wananchi
Wengi wamehoji imekuaje ACT wameshindwa kulinda kura mbali na kuwa na kauli mbiu ya ‘Linda kura’ waliyoahidi kuwa ingefanya kazi? Wengine wamedai tangu awali chama hicho kilikosa muelekeo ilipoamua kushiriki uchaguzi wa 2025

Diaspora wa Watanzania Canada na Sweden waandamana, wataka uwajibikaji kwa mauaji yaliyotokea Oktoba 29
Diaspora wa Watanzania walioko Toronto, Canada pamoja na Gothenburg, Sweden wameandamana Novemba 8 kama jitihada za kupigania haki za binadamu kufuatia vifo vya mamia ya Watanzania vilivyoripotiwa baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, ambao umegubikwa na mauaji makubwa ya raia.

Waandamanaji hao wametaka Humphrey Polepole, Tundu Lissu, John Heche, Niffer na wengine waliotekwa ama kukamatwa kwenye maandamano hayo waachiwe huru. Pia Rais Samia na serikali yake kujiuzulu kwani uchaguzi haukuwa huru na haki.

Maoni ya wananchi
Wananchi wengi wanaunga mkono suala hili, wakiamini kuwa kuendelea kwa mashinikizo kutoka ndani na nje ya nchi kunaweza kusaidia haki kupatikana na kusaidia familia za waathirika wengi pamoja na kuiondoa serikali ya Samia wanayodai iliingia madarakani kwa udanganyifu.

‘Bongo Zozo’ ajiuzulu Ubalozi wa Utalii Tanzania kufuatia mauaji ya raia Oktoba 29
Mtengeneza maudhui na Balozi wa Hiyari wa Utalii wa Tanzania, Nicholas Reynolds (maarufu kama Bongo Zozo) raia wa Uingereza, ametangaza kujiuzulu rasmi nafasi yake akieleza kuwa uamuzi huo umetokana na hali ya uvunjifu wa amani na kupotea kwa utu nchini.

Kupitia taarifa yake, Bongo Zozo amesema amesikitika kuwaangusha Watanzania na kumshukuru aliyemteua, Hamisi Kigwangalla.

Ametoa shukrani kwa wote waliomuunga mkono, akibainisha kuwa kutokana na maumivu makubwa aliyo nayo, hawezi kuendelea kutekeleza majukumu yake hadi pale atakapopata utulivu wa moyo na kuona amani ikirejea nchini.

Maoni ya wananchi
Wengi wamempongeza Bongo Zozo kwa msimamo wake wa kujiuzulu, wakimwona kuwa ni mzalendo wa kweli. Wamesema uamuzi huo unaonyesha msimamo wa taifa kwa sasa, hasa kutokana na vifo vya raia wasio na hatia, na wanahimiza viongozi wengine kufuata mfano wake katika kudumisha amani, haki na utulivu nchini.

Mwenyekiti UVCCM Taifa: Wanalipwa kuchochea vurugu, nchi yetu wameichoma moto
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mohamed Ali Kawaida, amesema kuwa matukio yaliyotokea Oktoba 29 hayakuwa maandamano halali, bali ni vurugu zilizoendeshwa na baadhi ya vijana waliorubuniwa kupitia mitandao ya kijamii na watu wanaoishi nje ya Tanzania ambao wanalipwa kufanya kazi hizo.

Aidha, amesema vijana walioumizwa katika vurugu hizo walishindwa kupata matibabu kwa kuwa zahanati nyingi zilikuwa tayari zimechomwa, hali iliyosababisha wengine kupoteza maisha kwa makosa yao wenyewe.

Maoni ya wananchi
Wengi wamekosoa kauli yake kwa kuzungumzia uharibifu wa mali bila kutaja raia waliouawa wameuawa na nani, huku wakipinga kuhusu hospitali kuchomwa kwani hakuna mahali popote ambapo waliripoti hospitali kuvamiwa au kuchomwa na waandamanaji.

Baadhi wasema kauli zake zimejaa kiburi na kuzidi kuleta chuki miongoni mwa wananchi.

Kampuni ya Lake Oil yakanusha kumilikiwa na wanasiasa
Kampuni ya Lake Oil imesema kuwa haimilikiwa na mwanasiasa kama inavyodaiwa mitandaoni, bali inamilikiwa na Mtanzania anayeitwa Ally Adha Awadhi, ambaye ndiye mwanzilishi na mmiliki halali wa kampuni hiyo.

Akizungumza na vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Lake Oil Group, Stephen Mtemi, amesema vurugu zilizotokea Oktoba 29 zimesababisha uharibifu mkubwa wa vituo vya mafuta na miundombinu ya kampuni hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema jumla ya vituo 38 vimeharibiwa au kuchomwa moto, hali iliyosababisha zaidi ya wafanyakazi 300 kupoteza ajira kwa muda baada ya kupewa likizo bila malipo.

Maoni ya wananchi
Wameitaka mamlaka na mmiliki wa kampuni hiyo azungumze mwenyewe, huku wakionyesha kutokuwa na imani na umiliki wa kampuni, wakihoji kwamba inamilikiwa na mmoja wa watoto wa rais mstaafu, Ridhiwani Kikwete.
 
Back
Top Bottom