Date::8/14/2008
Mbunge: Shamuhuna adhibiwe, suala Zanzibar si nchi laibuka tena Bungeni
Na Tausi Mbowe, Dodoma
Mwananchi
MBUNGE wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe, ameitaka serikali kumuadhibu Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Ali Juma Shamuhuna, kwa kuonyesha utovu wa nidhamu wa kumkosoa hadharani Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusiana na kauli yake kuwa Zanzibar si nchi bali ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya Pinda kutoa msimamo huo kuwa Zanzibar si nchi, Shamuhuna alidai katika tamko lake ndani ya Baraza la Wawakilishi, Zanzibar ni nchi huku akibeza wale wanaodai tofauti.
Dk. Makyembe ambaye jana alikuwa akichangia hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2008/09, alisema kitendo kilichoonyeshwa na kiongozi huyo wa juu wa serikali ni utovu wa nidhamu na kimeonyesha fedheha kubwa kwa serikali.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe ambaye hakutaja moja kwa moja jina la kiongozi huyo ambaye hivi karibuni alisimama na kupingana na Waziri Mkuu Pinda kuhusu hadhi ya Zanzibar, alisema kwa waziri kupingana na tamko la Waziri Mkuu ni utovu wa nidhamu wa kupindukia.
Alisema kilichotokea ni fedheha kwa serikali kwa kuwa Waziri Mkuu alishatoa tamko bungeni, lakini kichekesho kinakuja pale waziri anasimama na na kumkejeli.
Pia Dk. Makyembe alihoji serikali ipo wapi na usiri wa serikali ikiwa ni pamoja na vyombo vya mawasiliano kama vimeenda likizo kwa kushindwa kumshughulikia waziri huyo ambaye alionekana wazi kumkejeli Waziri Mkuu ambaye amekuwa akifuata katiba na tayari alikwisha agiza wanasheria wa pande zote mbili kulishughulikia suala hilo.
"Waziri wa Zanzibar kumkosoa Waziri Mkuu ni utovu wa nidhamu kwa viongozi wetu, mimi hapa sioni kama kuna mgogoro wowote wa kikatiba ninachoona ni fedheha kubwa kwa serikali yetu, baadhi ya viongozi wa serikali. Ninachoomba adhibiwe, asipoadhibiwa mimi sioni ajabu siku moja Rais akinyooshewa kidole machoni," alionya Mwakyembe.
Alisema endapo Waziri Mkuu ambaye ndiye kiongozi wa Baraza la Mawaziri akiamua jambo na kulitolea ufafanuzi, hairuhusiwi kwa waziri yoyote kupinga maamuzi hayo, kwani kwa kufanya hivyo ni kutoheshimu kiongozi huyo na ni utovu wa nidhamu.
Mjadala wa Zanzibar si nchi au la umezidi kuchukua sura mpya kila kukicha.
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge Samuel Sitta, jana tena alimuokoa tena Waziri Mkuu Pinda, kutumbukia katika mjadala wa ama Zanzibar ni nchi au la, baada ya kuweka msimamo kwa kutaka wabunge wasiulize tena hoja hiyo katika Bunge linaloendelea.
Sambamba na hilo, Spika Sitta alijikuta akilazimika kujibu maswali ya wabunge waliokuwa wakionekana kuendeleza hoja hiyo ya Zanzibar ni nchi au la, huku pia akimtaka Katibu wa Bunge, asirudie kupanga wabunge wengi kutoka visiwani Zanzibar katika orodha ya wabunge wanaotaka kumuuliza waziri mkuu, maswali ya papo kwa papo.
Aliyeibua tena mjadala huo alikuwa ni mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Sulemain Khalifa, ambaye alitaka kauli ya serikali kuhusu azimio la mkutano wa 16 lililoazimia pamoja na mambo mengine, kuundwa kwa serikali ya Tanganyika lililotolewa mwaka 1993 na kuomba alisome lote, jambo aliloruhusiwa na spika.
Hata hivyo, badala ya kumruhusu Waziri Mkuu Pinda ajibu swali hilo, spika Sitta alisimama na kusema:, "Mimi nalitafsiri hili ni kama njia ya kwenda katika hoja ya kwanza ya Zanzibar si nchi au la, wakati Waziri Mkuu ameshalitolea maamuzi jambo hili lisingestahili kwa wakati huu, hapana silikubali hata kidogo, mheshimiwa Waziri Mkuu wala usijibu hili,"alisisitiza Sitta na kuongeza:
"Zanzibar kuna serikali, kuna Rais, kuna Baraza la Mawaziri, hivi hii hoja ya Zanzibar si nchi ina kitu gani kwa Wazanzibari? Kutaka serikali ya Tanganyika basi suala hili litoke kwa Watanganyika wenyewe, leo Wanzanzibari wanataka serikali ya Tanganyika kwa nini, kuna kitu kinajificha hapa, hawa wenzetu wana hoja gani hasa wanayoimaanisha," alihoji Spika Sitta.
Mara baada ya Spika kujibu hoja hiyo, Mbunge wa Mkanyageni, (CUF) Habibu Mnyaa, alisimama na kutaka kuuliza swali, lakini kabla ya kufanya hivyo, aliuulizwa, na wewe unaenda huko? na kisha Mnyaa akamjibu kuwa hapana yeye alikuwa akiuliza swali lingine.
Hata hivyo, hali haikuwa kama alivyoahidi kwani alionekana kutumia ujanja kwani baada ya kupatiwa nafasi, alihoji ni chombo gani kinatambulika kisheria kinachounganisha Muungano, jambo lilofanya ukumbi mzima kutamka kuwa ni 'yaleyale'.
Kufutia swali hilo, Sitta alisimama kwa mara nyingine na kulazimika kutoa ufafanuzi tena na kusema katika utaratibu kama hoja ikishajibiwa na kutolewa maamuzi katika mkutano unaoendelea, haistahili kujadiliwa tena.
Sitta alisema ni dhahiri kabisa jibu lililowazi Makamu wa Rais anatoka Zanzibar ambaye ndiye mwakilishi wa Zanzibar, kwani hata wakati Rais anaposafiri yeye ndiye anamkaimu hivyo kuendelea kuhoji suala hilo haileti maana.
Mara baada kujibu hoja hiyo, wakati huo Waziri Mkuu akiwa amesimama katika eneo lake la kujibia maswali, Spika alimwita mbunge mwingine, Dk Tarab Ally Tarab, mbunge wa Konde (CUF), ambaye aliuliza swali lililofuata na kushangazwa jinsi Katibu wa Bunge alivyopanga orodha hiyo ya wabunge wanaotakiwa kumuuliza maswali Waziri Mkuu, kwa jinsi wote walivyotoka visiwani Zanzibar.
"Leo katibu amewapanga wale wale, kweli usirudie mchezo huu, hoja hii imeshajadiliwa, lakini hawa wenzetu bado wanaturudisha nyuma," alisisitiza Spika na kuhoji kama Wanzanzibari hao wana hoja gani iliyojificha ndani yao mpaka wakashupalia suala hilo la kuundwa kwa serikali ya Tanganyika badala ya kuwaachia Watanganyika wenyewe.
Dk Ally alimuuliza Waziri Mkuu Pinda, atawahakikishia vipi wananchi wa Zanzibar kila raia mwenye sifa za kupiga kura atapatiwa haki hiyo na kudai kuwa yeye kama mbunge alinyimwa haki yake ya kupiga kura mwaka 2005 katika uchaguzi mkuu baada ya kushindwa kuona jina lake katika daftari la wapiga kura.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alishindwa kujibu swali hilo na kusema kuwa swali hilo linaleta utata kwa kuwa ukilitazama tu unagundua halina maana kwa kuwa muuliza swali alionekana wazi kuficha baadhi ya vitu ambavyo aliamini ni kutokana na Spika kukataza hoja ya Zanzibar isijadiliwe hivyo kumtaka muuliza swali aliweke vizuri swali lake.
Naye Mbunge wa Chambani (CUF), Salimu Hamisi, alimuuliza Waziri Mkuu kwa nini viongozi wa siasa wanaingilia matokeo ya uchaguzi na kutoa mfano wa Tume ya Uchanguzi Zanzibar (ZEC), kuwa ilishawahi kukiri inaingiliwa katika matokeo yake, je, serikali inasemaji kuhusina na hilo na Waziri Pinda alimjibu kuwa inaonekana muuliza swali kuna kitu ameshindwa kusema kwa kuwa hana hakika mbunge huyo alikuwa anataka kusema nini hasa.
Kwani serikali ya Zanzniaba ina tume yake ya Uchaguzi na kama imekiri kuingiliwa basi zipo njia za kupeleka malalamiko hayo huko.
Hata hivyo, mara baada ya kipindi hicho cha maswali ya papo kwa papo kuisha, Mbunge wa Mkanyageni, Habibu Mnyaa alisisimama na kuomba muongozo wa Spika kwa kutumia kifungu namba 68 (7), na kusema kwa kuwa si kazi ya Spika kujibu maswali ya wabunge inakuaje mbunge aulize swali na kujibu Spika? na kwamba hakuridhishwa na majibu hayo hivyo kuomba muongozo afanyaje ili maswali yao yaweze kujibiwa na mtu anayestahili.
Sitta alisimama tena na kumjibu mbunge huyo kuwa ni kweli kazi ya spika si kujibu maswali ya wabunge, lakini inapotokea hoja imeshatolewa ufafanuzi na spika akaona kuna baadhi ya watu wanaendeleza usumbufu, kiti alichokalia ni imara hivyo hataruhusu mambo hayo yatendeke.
''Kiti ni imara na tutaendelea na msimamo huo huo, nawaomba wenzangu akiwemo Naibu Spika, Wenyeviti, Job Ndugai, Zuberi Maulid na Jenista Mhagama, wote tuwe na msimamo huo huo,'' alisistiza Spika Sitta.
Mjadala kuhusu hadhi ya Zanzibar uliibuka katika mkutano wa Bunge unaondelea baada ya Pinda, kusema Zanzibar haiwezi kujiunga na Jumuiya za kimataifa kama ile ya Kiislam (OIC) au Afrika Mashariki (EAC), kwani si nchi.