Date::8/18/2008 Wanasheria wapigilia msumari kuwa Zanzibar si nchi Kizitto Noya na Happiness Matanji
WATAALAM wa Sheria wamesema mgogoro wa hadhi ya Zanzibar kuwa nchi hauwezi kutatuliwa kwa kutumia sheria bali busara ya ama kufuta Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) au kuanzisha serikali ya Tanganyika.
Wakizungumzakwa nyakati tofauti jana, wanasheria hao walisema sheria haiwezi kutumika kumaliza mgogoro huo kwa sababu imeshafikia kikomo chake cha maamuzi.
Wakili maarufu wa kujitegemea, Twaha Taslima, alisema sheria ina ukomo katika kushughulikia mambo hasa baada ya Mahakama ambayo ndiyo ya mwisho katika kutoa maamuzi, kupitisha hukumu.
Alisema kuhusu Zanzibar, mahakama ilishatoa hukumu kwamba Zanzibar sio nchi na kuwaachia huru watuhumiwa wa kesi za uhani katika miaka ya hivi karibuni na Katiba pia imeweka bayana kuwa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.
Akinukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema Ibara ya Kwanza imetamka bayana kwamba Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano hivyo sheria ya maandishi haina jibu lingine.
Taslima alisema maelezo hayo na kitendo cha Mahakama Mahakama Kuu kuwaachia huru watuhumiwa wa uhani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ndio mwisho wa tafsiri za kisheria kuhusu suala la Zanzibar na kwamba kilichobaki sasa ni busara ya kawaida kutumika.
Hata hivyo alisema sheria imechangia kuleta utata wa suala hilo kwani ukisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ibara ya nne vifungu vya kwanza hadi tatu utapata picha kwamba, kiutekelezaji Zanzibar ni nchi na kiutendaji sio nchi.
Ibara ya Nne, kifungu cha kwanza hadi cha tatu vinasema: 'Kwa ajili ya utekelezaji bora na mgawanyo wa mamlaka, kutakuwa na mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano', alisema na kuongeza:
''Shughuli zote za Mamlaka zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo vyenye mamlaka ya utekelezaji (SMZ na Serikali ya Muungano) na mamlaka ya kutoa haki itakuwa ya vyombo viwili vya kutoa haki (Mahakama ya Zanzibar na Muungano)''.
Kuhusu mjadala wa ama Mbunge wa Kyela Harrison Mwakyembe alikosea kuwataka mawaziri wa Zanzibar waadhibiwe kwa kupingana na Waziri Mkuu kuhusu hadhi ya Zanzibar, Taslima alisema alikuwa sahihi ingawa pia haikuwa busara kwake kutoa tamko hilo hadharani.
''Mwakyembe angepeleka suala hilo kwenye vikao vya chama ili wakajadili, lakini pia hakukosea kusema mawaziri hao waadhibiwe kwani kimsingi dola ya Muungano ndio yenye nguvu kuliko SMZ na yeye alikuwa anazungumzia masuala ya Muungano,'' alisema
Kauli ya Taslima iliungwa mkono na mtaalam wa mambo ya katiba na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk Sengondo Mvungi, aliyesema kuwa sasa inatakiwa busara itumike kuhusu hoja ya hadhi ya Zanziba.
''Mbona tunasema hamwaelewi, mnataka sheria isemeje? alihoji Dk Mvungi na kuendelea: ''Katiba inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi moja yenye Mamlaka, ukilijua hilo swali kwamba Zanzibar ni nchi au sio halizuka tena, vinginevyo hawa wanaoendeleza mjadala huo watwambie wana maana gani,'' alisema.
Kuhusu suala la Mwakyembe alisema kwa sababu dola ya Jamhuri ya Muungano ndio yenye nguvu, mawaziri wa Zanzibar wanapaswa kumheshimu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ingawa anayeweza kuwaadhibu ni Rais wa Zanzibar.
''Mwakyembe yuko sahihi kwamba mawaziri wa Zanzibar wanatakiwa kumheshimu Waziri Mkuu na ikumbukwe kuwa Pinda alizungumzia suala la Muungano hivyo wadhifa wake bado ni mkubwa na usiopaswa kupingwa hadharani na watendaji wa serikali,'' alisema Mvungi.