Na Salim Said Salim
KWA kawaida binaadamu yoyote yule mwenye akili timamu huwa hapendi kupoteza kiungo chake chochote kile, iwe cha mguu au mkono. Lakini hufika wakati mtu huyo huyo huridhia kwa tabasamu na kusisitiza kiungo chake kimoja kinachomsumbua kikatwe haraka.
Wakati mwingine mtu huyo anakuwa tayari kiungo hicho kikatwe hata kama hapana sindano ya ganzi, kama kufanya hivyo kutamsaidia kunusuru maisha yake ambayo yapo hatarini.
Ni kutokana na hali kama hii ndio wazee wetu wakasema na kutunasihi kwamba baadhi ya wakati Lisilo budi hutendwa.
Hivi sasa pamezuka jambo baada ya kusikika kauli za kutaka uchaguzi wa Zanzibar uliopangwa kufanyika Oktoba, usogezwe mbele ili kujenga mazingira sio tu ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki, bali wa amani ya kweli na utaokuwa hauna mauaji, watu kupigwa mapanga na nondo na kuwa vilema.
Wengine wengi katika chaguzi ziliopita za vyama vingi walibakwa, nyumba zao ziliporwa na wengine walilazimika kukimbia nyumba zao na kuishi msituni au kwenda nje ya nchi kuwa wakimbizi na wengine hivi leo wapo Somalia kwa vile wanaona huko kuna afadhali kwao kuliko waliyoyashuhudia visiwani.
Hakuna mtu aliyefikishwa mahakamani kwa kuhusika na orodha ya maovu yote haya. Sijui mambo kama haya yangefanyika Kisarawe, Mzee Pius Msekwa angelisemaje.
Baada ya kikao cha kihistoria cha miezi miwili iliyopita kati ya Rais Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, watu wa Zanzibar wameanza kupumua na kuona ipo kheri usoni. Hata hivyo, wapo pia walionuna.
Ni kwa kutaka hali hii ya amani iendelee na pajengeke mazingira yatakayoyafanya yaliopita kuwa sehemu ya historia na sio kurudiwa baadhi ya watu, hasa kutoka bara, nasisitiza kutoka bara, wanaoonekana hawapendi na wamekasirishwa na kuwa watetezi wakubwa wa Katiba ya Zanzibar.
Sijui watu hawa walikuwa wapi na kushindwa kutetea Katiba pale suala la mafuta lilipoingizwa katika orodha ya mambo ya Muungano bila ya ridhaa ya Zanzibar na hatukuwaona kutetea maslahi ya Zanzibar na watu wake?
Kichekesho ni kwamba aliyekuwa Spika wa Bunge, Pius Msekwa, na sasa Makamu Mwenyekiti wa CCM alikuwa kimya wakati mabadiliko mengi ya Katiba yalipofanywa akiwa Spika, lakini leo ndio kawa mtetezi mkubwa wa kutaka Katiba ya Zanzibar iheshimiwe na isirekebishwe wakati alikuwa kimya Katiba ya Muungano ilipoongezwa kiraka kimoja baada ya chengine.
Zipo hisia hapa Zanzibar kuwa labda Msekwa na wengine kama yeye wangelielewa uchungu wa mauaji kama waliouawa na kuwa vilema ni watu wa kisiwa cha Kisarawe na sio Pemba.
Baadhi ya waandishi wa habari wa Dar es Salaam ambao hata Zanzibar hawajafika na kuona harakati za uchaguzi ambapo watu kutoka Bunju, Kawe, Bagamoyo huja kupiga kura wamekuwa wataalamu wa masuala ya Zanzibar.
Ni vyema wakaelewa wanapaswa kufahamu kilichotokea kinachoendelea na kinachopangwa kutokea visiwani kabla hawajawa na ujabari wa kuzungumzia habari za Zanzibar.
Ukweli ni kwamba mazingira ya kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu ni machafu na ya hatari. Zaidi ya nusu ya watu wenye haki ya kupiga kura wamenyimwa haki hio, hasa katika sehemu ambazo ni ngome za chama cha CUF, kama Mji Mkongwe, ingawa takwimu zinaonyesha ni zaidi ya asilimia 90 ya wapiga kura wameandikishwa.
Takwimu za Tume ya Uchaguzi hazitoi sura yoyote ile isipokuwa kuonyesha namna uwongo unavyoshadidiwa ili ukubalike kuwa kweli. Kama Tume ya Taifa Uchaguzi Zanzibar (ZEC), inasema kweli, basi ingeacha kuendesha shughuli zake kwa siri na kuliweka hadharani daftari la wapiga kura ili wale walioandikishwa zaidi ya mara moja wakaeleweka.
Huu mchezo mchafu wa maelfu ya watu kunyimwa haki ya kupiga kura, ndio unaoleta wasi wasi juu ya uchaguzi ujao.
Zipo taarifa za kuandaliwa kambi za vijana wanaoitwa Janjaweed na maeneo yanayotajwa kuwepo kambi hizi ni kama Tungu na Pangatupu, Unguja.
Waliofanya vijana hawa katika chaguzi ziliopita na Jeshi la Polisi kuonekana halikuwa na habari za matukio ya watu kupigwa mapanga na nondo katika vituo vya uchaguzi.
Matukio kama haya, kutokana na mazingra yaliopo yanaonekana kutaka kurejewa katika uchaguzi ujao. Hii ni hatari ambayo akina Msekwa wanafaa waione na waelewe kuwa maisha ya watu wa visiwani nayo yana thamani kama ya ndugu zao wa bara.
Kwa ufupi hali ya kisiasa kuelekea uchaguzi ujao Zanzibar ni mbaya na inatisha, lakini inaoenkana baadhi ya wakubwa bara huenda wakawa wanafurahia vurugu hizi zilizoshuhudiwa Zanzibar.
Kama wanawapenda ndugu zao wa Zanzibar kwa nini wasifurahie maelewano haya na kuona amani ni muhimu kuliko uchaguzi?
Linalonishangaza ni kuwa kinachojadiliwa ni Katiba ya Zanzibar na sio ya Muungano. Kwa maana nyingine hili ni suala la Wazanzibari na sio la bara au Muungano. Au tunataka kuambiwa Wazanzibari hawana haki ya kujiamulia mustakbali wao au Zanzibar ni mali ya CCM na sio ya wananchi wake?
Wazanzibari wamekuwa wakijizuia kujadili kasheshe za Richmond, EPA na nyingine kwa vile masuala haya hayamo katika orodha ya Mambo ya Muungano.
Sijuwi wapi baadhi ya viongozi wa bara wamepata ujabari wa kutaka kuwaamulia watu wa Zanzibar mambo yao. Labda walitakiwa ushauri na kama ni hivyo ni nani hao waliowapa kazi hiyo?
Ninachowasihi ndugu zangu wa bara waliachie suala hili liamuliwe na Wazanzibari ambao wamechoshwa na mauaji na kuona askari wanaletwa kwa mamia kutoka bara wakati wa uchaguzi.
Ni kweli katiba haifai kuchezewa, japokuwa Katiba ya Muungano ina historia ndefu ya kuchezewa na ndio maana sasa imejaa viraka. Lakini inaonekana kutaka kubadili Katiba ya Zanzibar ndio nongwa. Maajabu haya.
Hili ni suala la Zanzibar na kinachotaka kufanywa na Wanzibari na lile niliolieleza kama lisilo budi hutendwa, kama kukubali mtu kukatwa kiungo ili anusuru maisha yake.
Lakini pia tukumbuke mtu ambaye hajala pili pili hastahiki kudai inamuwasha, yaani pilipili usioila wewe inakuwashiani? Katiba ya Zanzibar haiwahusu watu wa bara sasa kwa nini hawawaachii watu wa Zanzibar kuamua wanachotaka au hawana haki hiyo?
Kama viongozi wa Bara walishindwa kuwasaidia watu wa Zanzibar kuelewana walipokuwa wanakwaruzana sasa wasifunge njuga kuwarejesha walipotoka. Wanaokufa ni watu wa visiwa vya Unguja na Pemba na sio Mafia au Kisarawe na wanaopata vilema ni watu wa Mji Mkongwe na sio Nguvumali, Tanga.
Suala la kama Rais Karume aongezewe muda ili astawishe mazingira ya amani au la, waachiwe Wazanzibari kuamua na wenye haki kwa niaba ya watu wa visiwani kulifanyia maamuzi ni Baraza la Wawakilishi na sio Msekwa, Makamba na wenzake au Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Katiba ya Zanzibar ni ya Wanzibari wenyewe na tuiachie ibaki hivyo kwa maslahi ya Zanzibar na ya Muungano. Tuache dhana potofu ya kusema Wazanzibari wanapotaka umoja basi lengo lao kuu ni kuvunja Muungano. Hii ni hoja ya kipuuzi.
Kama Wazanzibari hawataki Muungano hawataona taabu kueleza hivyo na mara kadhaa walipokerwa walitamka hivyo. Hakuna anayeogopa kusema hivyo.
Hata Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati mzee Abeid Amani Karume, aliweka wazi kwamba Muungano ni kama koti. Ukiona linakubana sana na huwezi tena kulivaa, unalivua na kutafuta jengine.
Sio vizuri kuburuzana na kutishana.
Kama Wazanzibari wanafanya makosa kwa kutafuta maelewano, kuachana na siasa za chuki na uhasama na kuwa na mshikamanao waachieni wafanye hivyo.
Kama wanakosea huko usoni watakuja kujuta wenyewe na historia itawahukumu kwa kosa hilo. Kama wanayoyafanya yana maslahi na wao na vizazi vijavyo historia itatuonyesha siku za mbele.
Lakni jambo lingine la kuzingatia ni kwamba kinachoonekana Zanzibar sasa ni historia kujirudia. Katika mwaka 1964 mzee Abeida Karume na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nerere, walifanya mazungumzo wao wawili na kuunganisha Zanzibar na Tanganya na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivi sasa mwanawe, Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad, wamekutana watu wawili kwa lengo la kuwaunganisha Wazanzibari. Sasa kwa nini mkutano wa watu hawa wawili uwe nongwa?
Vile vile, baadhi ya viongozi wa Serikali ya Zanzibar na ya Muungano wanataka Baraza la Wawakilishi lisifanye uamuzi wowote wa masuala ya Katiba na badala yake waachiwe wananchi kuamua.
Hapa tujiulize kazi ya Baraza ni ipi na kama ni wananchi kuamua mbona mambo mazito huamuliwa bila ya wao kushirikishwa moja kwa moja?
Mungu inusuru Zanzibar na watu wake na iwakinge na wale wasioitakia mema na iwabariki wote wanaoitakia kheri.