Zanzibar: Uhafidhina, Visasi na Miafaka isiyodumu (2)
Joseph Mihangwa Mei 21, 2008
UCHAGUZI wa Januari 1961 uliposhindwa kupata mshindi ilibidi urudiwe Juni 1961 ambapo liliongezwa Jimbo moja la Mtambwe huko Pemba kufanya majimbo ya uchaguzi kuwa 23. Hatua hiyo ililalamikiwa na ASP (kama jinsi CUF ilivyoilalamikia CCM kuongeza majimbo mawili Unguja mwaka 2005) kwamba iliipendelea ngome ya vyama vya ZNP/ZPPP.
Matokeo ya uchaguzi huo uliogubikwa na ghasia yalikuwa kama ifuatavyo:- ZNP/ZPPP viti 13 na ASP viti 10. Hivyo, kwa mara nyingine, matokeo hayo hayakutoa mshindi na machafuko makubwa na ghasia kuzuka ambapo karibu watu 70 waliuawa, zaidi ya 1,000 kujeruhiwa na wengine 1,000 kukamatwa na serikali.
Wakati huo huo, ulizuka mtafaruku na migongano ndani ya chama cha ZNP kati ya viongozi wake wakuu Ali Muhsin, aliyekuwa na kundi kubwa la wafuasi, na Abdulrahman Mohamed Babu, Katibu Mkuu wa chama na mwenye kundi dogo la wafuasi; juu ya mwelekeo wa Zanzibar kuhusu itikadi na sera za uchumi za kufuata baada Uhuru.
Rais wa ZNP (Mwafrika), Vuai Kitoweo, kwa uwezo wake duni kiuongozi hakuweza kuzuia athari za ugomvi huo ndani ya chama. Wakati Muhsin alitetea sera na siasa za mrengo wa kulia za kihafidhina (conservative policies) na utii kwa Sultani, Babu kwa upande wake alikuwa muumini mkubwa wa sera/itikadi za Karl Marx, mbinu za ukomunisti wa China na chuki kwa ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo.
Wakati Muhsin alitetea uchaguzi kwa misingi ya ubaguzi wa rangi kwa maana ya watu kupiga kura kwa kuzingatia asili na utaifa wa mtu (racial compartmentalization), Babu alitaka kura zipigwe kwa kapu moja bila ubaguzi wa rangi au asili na utaifa wa mtu. Wakati huo huo alikitaka ZNP kisisahau asili yake kwamba kilikuwa Chama cha Waafrika wakulima, akashinikiza ateuliwe angalau mmoja wa waanzilishi wake kugombea kiti kwenye jimbo salama kuonyesha mtazamo wa kizalendo. Mapendekezo ya Babu yalikataliwa na viongozi wa ZNP na hivyo Babu na wenzake wawili wakajiengua kutoka chama hicho na kuunda Umma Party.
Umma Party kiliungwa mkono na sehemu kubwa ya jamii ya Kizanzibari kwa mtazamo wake wa kumjali mtu wa chini. Kilipigiwa upatu pia na Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (FPTU na ZPFL ), Umoja wa Waandishi wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari na Wanaharakati wa siasa za mrengo wa kushoto ndani ya ASP.
ABDULRAHMAN Mohamed Babu
Babu mwenyewe aliingia Umoja wa Waandishi wa habari na Wamiliki wa vyombo vya habari kama Mhariri wa gazeti la ZANEWS na aliweza kutoa msukumo na mchango mkubwa ndani ya vyombo hivyo na kuweza kuichonganisha serikali ya ZNP/ZPPP na wananchi. Ingawa Chama cha Babu hakikuweka mgombea /wagombea kwa nafasi yeyote katika uchaguzi wa Julai 1963, lakini kilikuwa mpinzani mkubwa na mwenye nguvu kwa serikali ya ZNP/ZPPP, ambapo kati ya kipindi cha kuundwa kwake 1962, na Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kilikuwa mwiba mkali (kuliko ASP) kwa serikali madarakani kiasi cha Babu kuwindwa na serikali ili akamatwe kwa kosa la uhaini.
Matokeo ya Juni 1961 yaliyowapa ushindi ZNP/ZPPP ndiyo yaliyotumika kama kigezo cha kuitishwa kwa mkutano wa Katiba mjini London (the Constitutional Conference) Machi na Aprili, 1962, ili kupitisha katiba ya Uhuru. Babu alihudhuria mkutano huo kinyemela baada ya kunyanganywa na Serikali hati yake ya kusafiria lakini akapewa hati nyingine na Serikali ya Tanganyika.
Katika mkutano huo, Waingereza walipendekeza iundwe serikali ya mseto Zanzibar ikihusisha vyama vyote, yaani ZNP/ZPPP, na ASP, ambamo ASP ingepewa nafasi tatu kati ya nafasi tisa za uwaziri na kura turufu (casting vote) juu ya maamuzi yote ya Baraza la Mawaziri.
Lakini hata hivyo, ASP walikataa pendekezo hilo, wakataka nafasi za uwaziri zigawanwe nusu kwa nusu, na kwamba uchaguzi mwingine ufanyike kabla ya uhuru, na wakapendekeza uwe katikati ya mwaka 1964. Ombi hilo lilikataliwa na Mkutano ukavunjika.
Baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya London, Serikali ya Uingereza ilimtuma mjumbe wake, Duncan Sandy, Zanzibar kujaribu kwa mara ya mwisho kutatua tatizo hilo la kikatiba kwa njia ya serikali ya mseto. Sandy aliwakutanisha viongozi wa pande zote mbili lakini hakuna maridhiano yaliyofikiwa.
Serikali ya Uingereza iliamua iundwe serikali ya ndani Juni 1963, na kufuatiwa na uchaguzi mwingine wiki mbili baadaye ambao matokeo yake yangetoa picha ya mwelekeo wa uhuru kamili kwa nchi.
Uchaguzi wa Julai 8, 1963, ulifanyika kwa majimbo ya uchaguzi 31 ambapo Muungano wa ZNP/ZPPP walishinda kwa viti 18 na ASP viti 13. Na kwa ushindi huo ZNP/ZPPP walipewa jukumu la kuunda Seikali na Mohamed Shamte wa ZPPP aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Zanzibar.
Kufikia hapo, viongozi wa ASP walifungua mazungumzo na ZNP/ZPPP wakiomba iundwe serikali ya mseto na pia kuona uwezekano wa kugawana kwa usawa nafasi za uwaziri. Ombi hilo lilikataliwa na ZNP/ZPPP kwa madai kwamba nafasi kama hiyo ilitolewa kwenye Mkutano wa Katiba wa London, lakini ASP wakakataa. Kwa kauli ambayo haikutarajiwa, Waziri Mkuu Shamte alijibu kwa jeuri kwamba siasa si kugawana mateka na akatamka Karume avunje ASP na wanachama wake wahamie ZPPP.
Ndani ya ASP nako mambo hayakuwa shwari ambapo kambi tatu ziliibuka na kupingana vikali kuhusu mtazamo na maana ya uhuru kufuatia ushindi wa ZNP/ZPPP na kupewa jukumu la kuunda Serikali, huku viongozi wakilaumiana kila mmoja kwa chama chao kushindwa.
Kundi la kwanza lilitaka ASP ifuatilie kwa nguvu na kwa gharama zozote kuhakikisha kwamba inaundwa serikali ya mseto ikishirikisha vyama vya ZNP, ZPPP, na ASP kama njia pekee ya muafaka wa kisiasa Zanzibar.
Kundi la pili la viongozi, likiongozwa na Rais wa ASP, Abeid Amani Karume, lilipendelea upinzani makini na wa kistaarabu na utii mkubwa bungeni uendelezwe ili kuepuka Serikali kutumia sheria na nguvu za dola dhidi ya chama hicho na wanachama wake.
Hii inamaana kwamba Karume hakutaka matumizi ya ghasia au malumbano na Serikali madarakani nje ya Bunge. Ndiyo kusema kwamba aliitambua Serikali madarakani na kwamba demokrasia ilipaswa kufanyakazi ndani ya Bunge pekee kwa maendeleo ya Wazanzibari
Kundi la tatu la viongozi wa ASP lilitaka kuwapo kwa upinzani wa nguvu na wa wazi wazi dhidi ya Serikali kwa kushirikiana na Umma Party cha Babu, na kwa kutumia mbinu za chini kwa chini kuihujumu Serikali, miundombinu na mipango yake.
Kwa mgawanyiko huu kiuongozi ASP kilidhoofu na kujiendesha kwa kupapasapapasa gizani. Viongozi wake hawakuweza kuzika tofauti zao kuweza kukiokoa nacho kikapoteza morale kisiasa, na hivyo hakikuweza tena kujiratibu kama chama makini na chenye nguvu kuweza kutoa changamoto kwa Serikalil ya ZNP/ZPPP.
Zanzibar ilipewa uhuru kutoka kwa Waingereza Desemba 10, 1963 katika sherehe zilizohudhuriwa na mwana wa Mfalme (Prince) wa Uingereza na Prince Agha Khan. Viongozi wote wa nchi za Afrika Mashariki hawakuhudhuria. Vyama vya ASP na Umma vilihudhuria kama waalikwa na kutoa salaamu za uhuru.
Ni Abdulrahman Babu wa Umma Party, aliyeuacha umma mdomo wazi bila kumwelewa, aliposimama kutoa salamu za chama chake na kusema, Salaam
. Vyama vya ZNP/ZPPP vimeunda Serikali kuingoza Zanzibar bila ridhaa ya waliowengi. . Lakini nawambieni kuwa Wazanzibari, chini ya uongozi wa Chama chao cha Umma Party wanasubiri kunyakua madaraka ya Nchi saa itakapowadia muda si mrefu.
Serikali ya Shamte haikudumu madarakani, kwani ilipinduliwa siku 32 tu tangu ishike madaraka na wanaharakati wa Umma Party wakishirikiana na wanaharakati wa siasa za mrengo wa kushoto walioziasi sera za ASP.
Msomaji, unaweza kuuliza, kuna ukweli gani kwa hilo? Jibu liko wazi. Angalia sehemu mbalimbali Visiwani zilizopewa majina ya Wanamapinduzi wa Kisoshalisti/ Kikomunisti kufuatia mapinduzi kama, Uwanja wa Mao-Tse-Tung, Chuo cha Fidel Castro, Hospitali kuu ya Serikali ya V.I. Lenin, Chuo cha Ualimu cha Patrice Lumumba, n.k
Itakumbukwa pia kwamba, Babu, mwanasiasa mwenye upeo mkubwa wa kuona mbali, wakati akiwa Katibu Mkuu wa Chama cha ZNP aliwahi kupeleka vijana Cuba na China kwa mafunzo ya kijeshi na mbinu za kivita ya msituni, na ambao siku chache tu kabla ya Mapinduzi ndio kwanza walikuwa wanarejea Zanzibar kutoka mafunzoni.
Vivyo hivyo siku chache baada ya Mapinduzi, Mwanamapinduzi na shujaa wa vita vya msituni kwa nchi za dunia ya tatu na mkombozi wa Cuba, Che Guevara, alitembelea Zanzibar kuja kusalimu, ndugu, jamaa na marafiki. Ndugu hao walikuwa kina nani kama si wanamapinduzi wa Zanzibar?. Siku chache tu baada ya kutoka ziara ya Zanzibar, Che Guevara alikamatwa (kwa msaada wa CIA) na majeshi ya Marekani na kuuawa nchini Bolivia.
Yote haya ni kielelezo thabiti juu ya nani, au kina nani waliopanga na kuendesha Mapinduzi ya Januari 12, 1964 Zanzibar. Hili limeelezwa mara nyingi katika makala zangu nyingi zilizopita.
Kama tulivyoona ndani ya makala haya, ni kwamba chaguzi zote Visiwani zimetumika kufufua na kutonesha vidonda vya kale na hivyo kuzua uhasama wa kale. Hapajawa na viongozi makini, wenye busara na hekima kuweza kuwaunganisha Wazanzibari na kuponya vidonda hivyo vya kale. Na ingawa ni Wazanzibari hao hao waliotaka Mwingereza aondoke, wakachagua viongozi wao kuwaongoza hadi leo, ni bahati mbaya kwamba viongozi wanaopata madaraka ni watu wanaoishi jana, wafitini na wenye kutazama nyuma badala ya kutazama na kuona mbele.
Kiongozi makini ni yule anayeweza kufanya maamuzi au kuchukua hatua ambazo si lazima ziwe kwa manufaa kwa chama chake, au zenye kuwafurahisha makada wake, lakini ni maamuzi au hatua sahihi na za manufaa kwa taifa; kwa maana ni taifa kwanza, Vyama vya siasa nyuma. Kushindwa kuelewa ukweli huu ni ulofa na ubinafsi wa hali ya juu.
Tunapenda kuamini kwamba viongozi wa CCM na CUF Zanzibar wataweka mbele maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari, badala ya kuweka mbele maslahi yao binafsi au yale ya vyama vyao vya siasa na marafiki zao.
Ubabe, jeuri na kupotosha historia ili kujijengea umaarufu bandia na Usultani ni sumu kwa demokrasia, utawala bora na kwa maendeleo ya nchi.
0713-526972
jmihangwa@yahoo.com