haya ni baadhi ya maneno ya wabunge wetu huko zanzibar wakiwa bungeni.
huyu ni mbunge wa DOLE
source:
http://www.parliament.go.tz/bunge/ContrLst.asp?Menu=Contr&PTerm=2005-2010&vpkey=1205&page=2
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kidogo kuhusu uchumi hasa uchumi wa Zanzibar. Kabla sijasema, ninataka nimnukuu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano alipokuja katika Bunge. Alisema hivi: Nitaangalia upya mchango wa Serikali ya Muungano katika maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii ya Zanzibar bila kuathiri haki na mamlaka kamili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mambo ambayo siyo ya Muungano.
Sasa hili nimeliangalia humu, nimekuta ule mgawanyo tu wa misaada kutoka nje, sasa hivi Zanzibar inapata mtihani mmoja, mtihani mmoja uko kwenye Muungano. Lazima unapokuwa katika Muungano, uridhie na mambo ya mwenzio hata kama hayo siyo wewe yanayokufaidisha. Lakini, keshokutwa tunaingia katika Afrika Mashariki. Tunazungumza Afrika Mashariki na kila kitu. Tunasema, Mwalimu alisema kwamba kuna hatari nchi ndogo ikamezwa na kubwa. Lazima tuambiane ukweli, nchi ndogo ikamezwa na kubwa.
Zanzibar hivi sasa hali yake ya uchumi siyo nzuri tukubaliane ndugu zangu. Siyo nzuri, pengine kwa sababu hakuna namna ya kutoka pale, maana kodi zinazowekwa hapa na Jamhuri ya Muungano, ndiyo kodi zinazotumika Zanzibar. Hivi tunaulizana, wananchi wa Zanzibar tuseme wako milioni moja. Kama kuna tajiri anaamua kuleta televisheni milioni moja, basi ina maana kila mmoja lazima anunue moja moja mpaka mchange, zitakazobakia kama milioni mbili atanunua nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tukubali kwamba wananchi wa Zanzibar kwa vyovyote vile uandaliwe mkakati, soko lao liwe Tanzania Bara. Tukubaliane hivyo. La sivyo, viwango vya kodi vya Zanzibar viwekwe vya tofauti, na kama siyo hivyo ujengwe mkakati maalum wa kusaidia. Kwa mfano, Afrika Mashariki kuna mambo mengi hivi sasa yanakuja na yatasadia Jumuiya ya Afrika Mashariki na yatasaidia hao wananchi milioni 30. Lakini hao watu milioni moja ambao wako pale Zanzibar wanasaidiwa vipi? Wanafaidika vipi na Muungano? Maana wananchi wa kawaida hawataki Uwaziri Mkuu hawataki Ubunge, hawataki Uwaziri, wao wanataka kufaidika na maisha yao vizuri. Hali za wale Wazanzibari wale sio nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, njia ya kwanza ambayo ningeomba, Bandari ya Zanzibar iwe bandari huru katika Afrika Mashariki na Afrika Mashariki ikibali kwamba Bandari ya Zanzibar ni Bandari huru ili ifanye kazi ya kupokea mizigo yote ya Afrika Mashariki na baadaye isambae katika Afrika Mashariki. Wazanzibari wale watapata kazi na suala la uchumi litakua na Serikali itajiendesha na mgogoro utakuwa hakuna. Si tunagawana! Wewe, kilimo wewe ardhi yako nzuri, wewe na nini, wewe na soko, lakini na wale nao watapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili sijui limefikia wapi! Nilitaka hilo na lenyewe niliweke hapa ili pengine Serikali itakapofanyia kazi, lifanyiwe kazi. Sio lazima lipatiwe jibu. Mnaweza mkalifanyia kazi huko baadaye, sio lazima mseme msimamie. Semeni nyie ndiyo mliosema. Kwa sababu wadogo hawaambiwi hili kasema fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninataka niliseme ni suala la Utawala Bora. Suala la Mihimili Mitatu:- Mhimili Bunge, Mhimili Mahakama, Mhimili Serikali. Kwa muda wa miaka 40 Bunge, Mahakama, vimetiwa mfukoni na Serikali.
Sasa, Mheshimiwa Rais ana maneno mazuri alisema hapa na nilikuwa namsikiliza na nafuatilia sana. Katika ukurasa wa 22 wa hotuba yake, alisema hivi: Serikali nitakayoiongoza itazingatia na kuendeshwa kwa msingi wa utawala bora, uwazi na uwajibikaji. Tutaheshimu utawala wa sheria na tutazingatia na kuheshimu mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mikuu ya dola yaani Utawala, Bunge na Mahakama. Tutaheshimu uhuru wa Mahakama na Bunge na tutatimiza ipasavyo wajibu wetu na tutawezesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ukitizama wenzetu wa Serikali na Bunge na Mahakama, kweli tuko sawa sawa! Tukubaliane! Wenzetu wa Serikali wanakusanya kodi na kupanga mikakati. Maana yake mpaka hili Baraza la Mipango na kila kitu wanakubaliana huko, sisi tunaletewa hapa tupitishe Bajeti. Lakini vipaumbele wamepitisha wao. Wanatutia mfukoni wenzetu. Sasa hilo ni jambo ambalo linatakiwa kusawazishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, Bunge na Mahakama sio chombo cha kuipigia magoti Serikalini katika kuomba Bajeti yake. Kama mwenzio ana uwezo mkubwa na wewe huna uwezo, uhuru huna. Kama yeye anakusanya kodi na halafu wewe unapiga magoti, maana yake Ofisi ya Spika, Bajeti yake iko chini ya Mkurugenzi ambaye yuko Ofisi ya Waziri Mkuu. Sasa, mtaendeshaje mambo yenu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.