Na Ndimara Tegambwage
SITAKI Zanzibar itumbukie katika mgogoro mwingine mkubwa, mpana na mzito kuliko yote iliyowahi kushuhudiwa Tanzania kutokana na ukaidi wa wachache wasiopenda mabadiliko.
Kamati ya Rais Jakaya Kikwete imekamilisha kazi ya kuleta makubaliano kati ya vyama viwili vikubwa vya siasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Tayari Baraza Kuu la CUF limekubaliana na mapendekezo ya kamati iliyofanya kazi kwa miaka miwili ikiwa na wajumbe kutoka vyama hivyo viwili.
CCM ilitarajiwa kuridhia makubaliano hayo jana au leo katika kikao chake cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kinachoendelea katika viunga vya Butiama, kijiji alikozaliwa Mwalimu Julius Nyerere.
Lakini hapa katikati kumezuka vineno. Hivi vinahusu tarehe ya kuanza kutekelezwa kwa muafaka mpya, unaolenga kuundwa kwa serikali ya umoja kati ya vyama vikubwa ambavyo ni CCM na CUF; na baadaye vyama vingine kwa mujibu wa marekebisho ya katiba na sheria husika.
Hadi jana, hakukuwa na taarifa yoyote juu ya tarehe ya kuanza kutekelezwa kwa muafaka mpya unaoleta serikali ya umoja. Taarifa zilizopo ni kwamba baada ya CCM kuridhia kazi ya Kamati ya Rais, basi kamati itaketi tena kuweka utaratibu, ikiwa ni pamoja na tarehe ya kuanza utekelezaji.
Habari kutoka Zanzibar zinasema utawala wa CCM visiwani Unguja na Pemba umeanzisha kampeni ya kutaka muafaka huu utekelezwe baada ya uchaguzi mkuu wa 2010.
Hoja zimeanza kujitokeza kwamba wakati rais anaweza kuendelea kuwa yuleyule kutoka CCM, Waziri Kiongozi wa sasa atapoteza nafasi yake. Hili, hoja hizo zinasema, litamdhalilisha Waziri Kiongozi na ofisi yake.
Hoja hizo zinadai pia kwamba, baadhi ya mawaziri waandamizi huenda wakapoteza nafasi zao katika serikali ya umoja, jambo linaloelezwa kuwa litawaondolea utukufu wa kisiasa waliokwishachuma.
Ni hoja hizohizo ambazo zinadai kuwa kuja kwa serikali ya umoja kutadhalilisha baadhi ya viongozi wa CCM ambao kwa ushabiki wa siasa za kitoto, wamekuwa wakitunisha vifua na kutambia CUF kwa kauli: Ikulu mtaisikia kwenye redio na kuiona kwenye televisheni
hamtakanyaga kule!
Hizi ni hoja za woga. Zinaletwa alfajiri wakati kazi pekee iliyo mbele yao kwa siku hii ni kuwa na serikali ya ushirika au serikali ya ubia, kabla haijaanza kuitwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Hatua ya CUF ya kukubaliana haraka na mapendekezo ya Kamati ya Kikwete inaweza kueleweka haraka pia. Kwamba wamechoka na biashara ya maneno kati ya chama chao na CCM.
Kwamba wamechoka kupokonywa ushindi au hata kunyimwa ushirika katika utawala wakati wana wanachama, wapenzi na wafuasi wengi katika Unguja na Pemba.
Kwamba wamechoka kutawala wakiwa kivulini; sharti sasa watambuliwe na katiba na sheria za Zanzibar, na jumuiya ya kimataifa.
Hili la kuwa watawala kivulini limeipa shida kubwa Serikali ya CCM Visiwani, kwani imeshindwa kujiamini; imekalia tako moja kwa woga; imeshindwa kupeleka huduma palipostahili, ama kwa kutaka kukomoa au kushindwa kupenya ngome ya wapinzani.
Kwa CUF kukubaliana haraka na mapendekezo ya Kamati ya Kikwete, inaonyesha imechoka kupigwa rungu na risasi; wafuasi wake kuuawa na wengine kuwa wakimbizi nchi za nje; na kuishi maisha ya woga siku hadi siku.
Lakini muhimu pia ni kwamba, CUF imeona hakuna sababu ya kuendelea kuwanyima wananchi wa Unguja na Pemba, fursa ya kujitawala, hata kama ni kwa ushirikiano na waliokuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40 sasa.
Kingine muhimu ni kwamba, CUF imetambua kuwa hakuna sababu ya kuchelewa kuasisi utamaduni wa maridhiano kisiasa ili kuweka msingi wa siasa za uvumilivu kwa vitendo.
CUF pia imejifunza na sasa imehitimu. Inaelewa vema kwamba siasa za kukaa na kulalamika, au kwenda mahakamani; au kusubiri mkono wa binadamu udondoke ndipo fisi auokote, hazitaweza kuifikisha mbali.
Kwa ufupi imekubali na kutamka: Tutawale pamoja. Nchi ni yetu sote. Kwa yeyote aliyekuwa anafuatilia vituko vya serikali katika chaguzi zote Visiwani, tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi, atakubali kuwa CUF imekubali kumeza ndoana, lije na lijalo!
Viongozi wa CUF waliona CCM ndio serikali na wakapata fursa ya kukaa na serikali kupitia CCM. Leo kuna muafaka wa kuwa na serikali ya ubia kati ya CCM na CUF. Nani anasema serikali hiyo isije leo?
Hatua sababu yoyote ile ya kutaka kuchelewesha utekelezaji wa makubaliano kupitia Kamati ya Kikwete, kwa visingizio vya Waziri Kiongozi na baadhi ya mawaziri kupoteza hadhi, ni adui mkubwa wa amani na usalama wa nchi hii.
Kwamba wafadhili wametishia kusita kutoa misaada kwa Zanzibar katika bajeti ya mwaka huu hadi muafaka wa sasa utekelezwe, si hoja kubwa sana ya msingi.
Wafadhili wana malengo yao na wanatumia miwani tofauti; kwani wamekuwepo kwa miaka yote na uchafu huu umefanyika mbele ya macho yao mwaka hadi mwaka.
Inabidi watawala wafikie mahali wachoke kutenda jinai na uhalifu mwingine, hata bila kuambiwa na wafadhili au yeyote kutoka nje. Katika hili, kusubiri ni kujidhalilisha.
Sitaki kusikia Serikali ya Kikwete ikikubali mawazo ya kuahirisha utekelezaji wa muafaka mpya hadi 2010. Kufanya hivyo ni kukiri utoto kisiasa. Ni kuomba wananchi waiondoe madarakani kwa ukosefu wa uwezo. Ni kuleta mgogoro mwingine mkubwa.