Kero za Muungano zinapotikisa Umoja wa Kitaifa
Joseph Mihangwa
Aprili 16, 2008
KIASI cha mwaka au hata miwili, kabla ya Uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, alinukuliwa kwenye karamu moja ya chakula cha jioni mjini Dar es salaam akisema maneno yafuatayo kuhusu Zanzibar:
Kama ningeweza kukivuta kisiwa kile mpaka katikati ya Bahari ya Hindi ningefanya hivyo.
Huku akionyesha wasi wasi dhahiri na kukerwa kwake na Zanzibar Mwalimu alisema:
kwa kweli sitanii kuna wasiwasi mkubwa kitatuletea matatizo makubwa huko mbele.
Miaka mitano baadaye Tanganyika na Zanzibar ziliungana kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, April 26, 1964.
Kwa Watanzania, Aprili unabeba matukio matatu makubwa ya kihistoria. Tukio moja ni hili la nchi mbili, (Tanganyika na Zanzibar) kuungana; la pili ni kuuawa kwa mmoja wa waasisi wa Mungano huo, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, mzee Abeid Amani Karume, miaka minane baadaye, Aprili 7, 1972.
Na tukio la tatu ni kufariki katika ajali ya gari kwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine ambaye rekodi yake haijavunjwa, Aprili 12, 1984. Yote haya yaligusa kwa namna moja au nyingine mustakabali wa Muungano.
Miaka 48 ni muda mrefu kwa uhai wa Muungano kama wetu, ikizingatiwa kwamba Muungano kama huu ulijaribiwa na nchi nyingine barani Afrika, kama vile kati ya Senegal na Gambia uliojulikana kama Sene-gambia, na ukafa katika kipindi kifupi sana pengine kutokana na kukosekana kwa utashi madhubuti wa viongozi wa nchi hizo, au kutokana na mifumo ya miungano hiyo kutokidhi matakwa na matarajio ya wananchi walio wengi wa nchi husika.
Vivyo hivyo, licha ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutimiza miaka 48 mwezi huu, hatuwezi kusema kwamba umesafiri kwenye barabara iliyonyooka siku zote kufika hapa ulipo, wala hatuwezi kujitapa kwamba Muungano huu umekidhi utashi (wa viongozi) na matarajio ya wananchi walio wengi kuweza kuitwa Muungano maridhawa asilimia mia kwa mia.
Tumeshuhudia mawimbi na tufani na meli yetu bado inaendelea kusukwasukwa. Tunapoadhimisha miaka hiyo 48 ya Muungano, siku kumi na moja tu zijazo kuanzia leo, yatupasa kutazama nyuma kuona wapi tumejikwaa, wapi tumelegea, wapi tujisahihishe ili tuweze kwenda mbele. Yote haya yataka utashi na uzalendo wa kweli.
Hatutaweza kufanya hivyo bila kutazama nyuma kuona na kubaini ukweli juu ya utashi uliozaa Muungano, misingi na mihimili ya Muungano; utekelezaji wake na mitafaruku iliyojitokeza na kuzua tufani.
Je, kifo cha Karume au kungatuka kwa Mwalimu Nyerere kumebakiza au kumepunguza utashi na usimamizi wa Muungano? Nini hatima ya Muungano?
Aprili 21, 1964 Rais Karume alipokea simu kutoka kwa Rais Nyerere akimwomba wakutane mjini Dar es Salaam kesho yake. Kweli, siku iliyofuata, Karume aliruka kwa ndege kwenda Dar Es Salaam, akakutana na Mwalimu na kuzungumza mengi ambayo hatujapata kuambiwa. Karume alirejea Zanzibar siku hiyo hiyo adhuhuri.
Siku moja au mbili nyuma kabla ya ziara ya Karume, Mwalimu alikuwa amemwagiza Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika, Roland Brown, kuandaa rasimu ya Mkataba wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar bila mtu mwingine kujua.
Naye Karume, aliporejea Zanzibar kutoka Dar Es Salaam, aliwaagiza wasaidizi wake kuandaa mapokezi ya Mwalimu Nyerere aliyetarajiwa kufika Zanzibar (Unguja) kesho yake asubuhi, Aprili 22, 1964. Mwalimu (na ujumbe wake) waliwasili Unguja siku hiyo kama ilivyopangwa akiwa na rasimu ya Mkataba wa Muungano mkononi, na kumkabidhi Karume aupitie na kuutia sahihi Mkataba huo ulioandikwa kwa Kiingereza.
Mkataba huo ulitiwa sahihi siku hiyo hiyo na Nyerere na Karume na kushuhudiwa na wasaidizi wao.
Nyerere alirejea Dar es Salaam siku hiyo hiyo baada ya kutiwa sahihi kwa Mkataba wa Muungano, maarufu kwa jina la Hati ya Muungano au kwa lugha ya kigeni Articles of Union. Mkataba uliofikiwa na viongozi hao wawili ulikuwa na hadhi ya kimataifa. Na ili Mkataba wa kimataifa upate nguvu, utambuliwe na kutumika katika nchi husika ni sharti uridhiwe (to ratify) na mabunge ya nchi husika.
NYERERE na Karume siku ya Muungano
Kwa hiyo, Bunge la Tanganyika na lile la Zanzibar (Baraza la Wawakilishi) yaliitishwa haraka haraka na kuridhia Mkataba huo, Aprili 25, 1964, na Aprili 26, 1964 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitangazwa rasmi.
Tutazame kwa ufupi tu maswali yaliyoibuka juu ya uhalali wa Muungano na jinsi ulivyofikiwa, kero na mitafaruku inayousibu Muungano tangu mwanzo hadi sasa.
Imeelezwa mara nyingi na duru za Muungano kwamba, Nyerere alitoa wazo la Muungano kwa Karume, naye (Karume) akakubali sawia. Kuna ukweli gani kwa taarifa hiyo?
Ni mambo yapi yalikuwamo katika Mkataba wa Muungno? Kuna hoja pia kwamba Mkataba wa Muungano haukuwa na ridhaa ya wananchi; na hivyo si halali. Watetezi wa hoja hii wanakwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa, ili mkataba huo uwe halali, ilitakiwa kura ya maoni (referendum) kama ambavyo mapendekezo ya muafaka wa Zanzibar kati ya CCM na CUF umerejeshwa kwa Wazanzibar kupata kura ya maoni. Hoja hii ni sahihi kiasi gani?
Kumbukumbu zilizopo (na imeandika mara nyingi juu ya hili) zinaonyesha kwamba kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika, kisiwa cha Zanzibar kilimnyima usingizi Mwalimu Nyerere kiasi cha kutamani kukivuta hadi katikati ya Bahari ya Hindi, kama angekuwa na uwezo wa kufanya hivyo; lakini hakuwa na uwezo huo kwa sababu yeye hakuwa Mungu.
Kwa hiyo, pengine njia pekee aliyoona Nyerere inafaa, ni kukidhibiti kisiwa hicho na kukisogeza karibu kwa njia ya Muungano. Hakuna ushahidi kuonyesha kwamba Karume alikubali sawia pendekezo la Mwalimu la Muungano, lakini kuna ushahidi kuonyesha kuwa, mwanzoni Karume alikuwa mzito kupokea au kujadili pendekezo la Mwalimu.
Kwanza, Mwalimu aliwatuma Oscar Kambona na Bibi Titi Mohamed kwenda kumshawishi Karume juu ya nchi zao Kuungana, lakini yaelekea Karume hakuweza kutoa jibu lililonyooka.
Alipowatuma tena Kambona na Bibi Titi Mohamed na kuwatumia pia baadhi ya viongozi wa Zanzibar Kassim Hanga na Salehe Sadallah kumshawishi Karume akubali hapo ndipo Karume alipoanza kuuona mwanga. Hilo ni jibu la kwanza.
Itakumbukwa pia kwamba, wakati Nyerere akijaribu kuzima hofu yake juu ya kisiwa hiki kama alivyosema mwanzo, Marekani nayo ilijawa na hofu kwa kisiwa hicho kuendelea kuserereka kwenda (kutekwa) kambi ya Ukomunisti (Urusi) kifikra na kimahusiano kiasi cha kuitwa Cuba ya Afrika".
Kwa hiyo, wazo la Nyerere la Muungano lilishabikiwa vile vile na Marekani kwa kuamini kwamba kama Zanzibar ingemezwa ndani ya tumbo pana la Tanganyika, harakati za Kikomunisti zikiongozwa na kina Abdulrahman Babu na vijana wengine kama Kassim Hanga, wenye fikra za mrengo wa kushoto, zisingefurukuta. Hilo ni jibu la pili.
Wakati huo huo Karume na Serikali yake alikuwa anakabiliwa na changamoto ndani na nje ya Serikali yake mwenyewe, kwamba alikuwa ameshindwa kutetea na kuendeleza dhana ya Mapinduzi iliyofanikisha Mapinduzi ya Januari 12, 1964, na hivyo alikabiliwa na tishio la kupinduliwa wakati wowote.
Kwa wana harakati wengi, Karume alionekana kuyaasi au kuyauza Mapinduzi. Kwa hiyo, Karume aliingia katika Muungano ili kujiponya mwenyewe na mahasimu wake ndani ya serikali waliomsakama na kutaka kumpindua. Hii ni sababu ya tatu.
Kwa sababu hizo tatu, na ile hofu ya Nyerere juu ya Zanzibar kuwa karibu na Tanganyika, tunaweza kusema kwamba Muungano huu ulifikiwa kwa msukumo wa hofu na kwa pande zote mbili mmoja kutaka kujiponya na tishio lake la kufikirika. Hii haikuwa ndoa ya hiari, bali ilikuwa ndoa ya kulindana (marriage of convenience) na kujiponya.
Chini ya Mkataba wa Muungano, Tanganyika na Zanzibar zilikubali kushirikiana katika mambo kumi na moja tu, ambayo ni Katiba, mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Polisi, Mahakama, hali ya hatari na Uraia.
Mengine ni Uhamiaji, Mikopo na biashara ya nje, utumishi, kodi ya mapato na Bandari. Orodha ya mambo ya Muungano imekuwa ikiongezwa kila mara kwa utaratibu ambao Wanasheria wa mambo ya Katiba wanadai ni kinyume cha Mkataba wa Muungano. Mambo hayo sasa yamefika 22.
Profesa Issa Shivji, katika kitabu chake The Legal Foundation of the Union in Tanzanias Union and Zanzibars Constitution anabainisha kuwa Bunge la Tanzania halina mamlaka ya kuongeza au kupunguza mambo yaliyokubaliwa kwenye Mkataba wa Muungano. Kufanya hivyo ni kukiuka ibara ya 5(i) ya Mkataba.
Msomi huyo anaeleza kuwa marekebisho kama hayo yanaweza kufanywa tu kwa njia ya kura ya maoni (referendum), ambao ndio utaratibu pekee unaojulikana duniani kwa nchi zenye Muungano kama wetu.
Anayosema Profesa Shivji yamefafanuliwa vizuri na Mahakama ya Rufaa ya Canada, katika shauri la A.G of Canada for Nova Scotia Vrs A.G. Canada (1951) S.C.R 31.
Ni maoni pia ya mtaalamu wa Katiba za nchi mbali mbali, K. C Wheare, katika kitabu chake, Modern Constitutions (Edition 1966), London, Oxford University Press Uk. 84, kama alivyoelezea Profesa Shivji.
Kwa hiyo, Bunge, hata kama litakaa kama Bunge la Katiba (Constituent Assembly), haliwezi kubadili Mkataba wa Muungano wa 1964. Huu ndio msimamo na mwongozo wa kisheria (wa mahakama) kama inavyobainishwa na Mahakama ya Mamwinyi ya Uingereza, katika shauri la A.G for Canada Vrs A.G for Ontario: (1973) A.G. 326 (PC); na katika hukumu za Mahakama ya Rufaa ya India, katika shauri la Kesavananda Vrs State of Kerala (1973) S C. 1461; Smt Indira Gandhi Vrs Raj Narain (1976) 2 S.C.R 3475 na katika kesi ya Minerva Mills Vrs Union of India: AIR (1980) SC 1789.
Kitendo cha Bunge la Muungano cha kubadili mambo ya msingi yale 11 yaliyomo katika mkataba kinyume cha utaratibu, kimekuwa ni moja ya sababu za Wazanzibari kurejea hoja ya kutaka kumezwa: na pale wanapojiamlia kutenda watakavyo, kinyume na baadhi ya marekebisho kiasi cha kuitwa wakorofi, serikali ya Muungano imekosa nguvu wala kauli inapobaini hayo; kero za Muungano huibuka, mitafaruku kuzuka, Muungano huyumba na utatuzi huwa mbali kwa imani kwamba suala la Muungano ni nyeti na lisilozungumzika.
Muungano uliofikiwa na waasisi wake, Mwalimu Nyerere na Karume mwaka 1964 ni halali na hauwezi kubatilika kwa sababu tu haukufikiwa kwa njia ya kura ya maoni (referendum) ya wananchi. Utaratibu wa kura ya maoni ni mpya kwa mfumo wa sheria za nchi za Jumuiya ya madola. Ulianza kutumika miaka ya 1970 (1976). Kwa hiyo wakati Nyerere na Karume wanafikia Muungano wa nchi zao walikuwa sahihi walivyofanya kwani Katiba iliruhusu.
Hapa nchini, utaratibu, uhalali na umuhimu wa kura ya maoni ni matokeo ya marekebisho ya Katiba ya 1984 pale Katiba hiyo ilipoingiza ibara ya 8(i)(a) inayosomeka: Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo, wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi. Tangu sehemu hiyo ya Katiba itungwe 1984, ni lazima wananchi watoe maoni yao kwa kura ya maoni, ni muundo gani wa Muungano wanataka.
Mengine yaliyokubaliwa katika mkataba huo ni pamoja na Rais wa Serikali ya Muungano, kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, kuteua Tume ya kupendekeza Katiba ya Muungano na kuitisha Bunge la Katiba ndani ya mwaka mmoja tangu tarehe ya Muungano, kupitisha Katiba ya Muungano.
Itakumbukwa kuwa pia Muungano wetu ulifikiwa haraka haraka bila maandalizi ya kutosha kiasi kwamba serikali ya Muungano ilianzishwa bila kuwa na Katiba ya nchi. Kwa sababu ya uharaka huo aina ya zima moto, ilibidi Katiba ya Tanganyika ya 1962 itumike pia kama Katiba ya Muungano kwa kuifanyia marekebisho madogo, hadi hapo Muungano utakapopata Katiba yake.
Hadi muda wa mwaka mmoja unamalizika, si Tume ya Katiba iliyoteuliwa, wala si Bunge la (kutunga) Katiba lililoitishwa. Ukimya huo ulifuatiwa na kutungwa kwa sheria Na. 18 ya 1965 ya kuongeza muda huo hadi hapo hali itakaporuhusu, huku kero za Muungano zikiibuka kwa kasi.
Mbali na kuongezwa kwa mambo ya Muungano kinyume cha Mkataba wa Muungano, mengine ni pamoja na kufutwa kwa nafasi za Makamu na Makamu wawili wa Rais, kuingizwa kwa mfumo wa chama kimoja ndani ya Muungano, na uteuzi wa Tume ya kupendekeza Katiba mwaka 1976, tofauti na aina ya Tume iliyotajwa ndani ya Mkataba na mengine. Yote haya na mengine yamezidisha badala ya kupunguza kero za Muungano.
Katika sehemu ya pili ya makala haya, tutajibu maswali yafuatayo: kwa nini Rais Nyerere hakuteua Tume ya Katiba wala kuitisha Bunge la Katiba na kusababisha Muungano kuendeshwa kwa Katiba ya mpito kwa miaka 13? Je, Katiba ya 1977 ni halali chini ya mkataba wa Muungano?
Je, kifo cha Karume na kungatuka kwa Mwalimu madarakani mwaka 1985 kuliathiri vipi utashi wa Muungano na kwa kiasi gani? Je, kitendo cha Zanzibar kuwa na bendera yake, wimbo wa taifa na ngao ya taifa ndani ya Muungano ni sehemu ya mkataba? Kwa nini haya yafanyike leo na si wakati wa enzi za waasisi wa Muungano huo?
Itaendelea wiki ijayo.