Inadaiwa kuwa kuna mawingu yamedondoka huko Morogoro kutokana na mvua kubwa zinazonyesha.
Wataalam, imekaaje hii?
Wataalam, imekaaje hii?
Video ikionesha kile kinachodaiwa kuwa ni Mawingu yaliyodondoka, Morogoro
- Tunachokijua
- JamiiCheck imefuatilia madai yanayotolewa kwenye video hiyo yenye sekunde 29 yakidai mawingu yamedondoka ardhini na kubaini kuwa hayana ukweli.
Kinachoonekana kwenye video hii ni mapovu yaliyotengenezwa baada ya kudondoka kwa gari iliyobeba kemikali zinazotumika kutengenezea sabuni kwenye Kata ya Tungi, Manispaa ya Morogoro.
“Ni kata ya Tungi, gari kubwa la mizigo lilimwaga kemikali inayotumika kutengeneza sabuni barabara kubwa ndio ikatengeneza povu kubwa. Watu ambao hawakuona kilichotokea wakajua kuna kitu kimedondoka kutoka juu, ilikuwa hali ya kushtua watu wengi lakini baada ya muda hali ya hewa ikakaa sawa na wakaliondoa gari ila hakufanikiwa kupata picha kutoka kwa wahusika”Mkazi mmoja wa eneo hilo aliiambia JamiiCheck.
Hata hivyo, video hii iliwekwa pia kwenye Mtandao wa X (Zamani Twitter) na Sophia Kessy akiomba ufafanuzi kutoka kwa wataalam.
Watu waliochangia mjadala huu walikuwa na maoni tofauti, lakini mchangiaji mmoja kwa jina la Moseleoh alisema “Hapa 88 Moro, kuna roli lilimwaga chemical pipa sita sasa nadhani hiyo ndio sababu. Na maeneo yenye mapovu kama hayo ni 88, Tungi, Tubuyu, Mfuruni kwa sababu mkondo wa maji ni mmoja”
Mamlaka zinazungumziaje suala hili?
Akizungumza na Gazeti la Mwananchi, Januari 21, 2024, Ofisa Afya Manispaa ya Morogoro, Ndimile Kilatu alisema maofisa wa idara hiyo walifika eneo la tukio (Tubuyu B) kufutilia chanzo cha mapovu katika korongo linalopitisha maji wakati wa mvua na kuyapeleka Mto Ngerengere na kubaini chanzo ni malighafi ya kutengenezea sabuni iliyomwagika Januari 17, mwaka huu kwenye maegesho ya malori ya Dar kuelekea DRC Congo au Zambia katika eneo la Nane Nane.
"Mua iliyonyesha siku mbili hizi imesafisha mabaki ya kemilikali hiyo na kuipelekwa kwenye vyanzo vya maji katika Mto Ngerengere na kutokana na maporoko ya maji, imezalisha povu. Tunafanya uchunguzi wa kimaabara tutatoa majibu," alisema Kilatu.
Kwenye video hiyo, mwanaume mmoja anasikika akisema sehemu hiyo ni Morogoro, Tanzania. Anaendelea kufafanua kuwa inasemekana mawingu yemetua nchi kavu, na yanaonekana yakielea na kuondoka.