Tumaini CN-CNB
Member
- Feb 13, 2021
- 5
- 5
Mvuto wa Mlima Taishan
Mount Taishan Attracting Visitors
Mohamed Mwinyi Mohamed
BAKITA TANZANIA
Mount Taishan Attracting Visitors
Mohamed Mwinyi Mohamed
BAKITA TANZANIA
Mlima Taishan wenye historia ya miaka mingi ni mojawapo la machimbuko ya utamaduni wa kale wa China. Kwa misingi hiyo mnamo mwaka 1987 serikali ya China ilipendekeza uingizwe kwenye orodha ya urithi wa kiutamaduni duniani inayosimamiwa na Shirika 1a Elimu, Sayansi na Utamaduni 1a Umoja wa Mataifa (UNESCO).
Tangu wakati huo makundi mengi ya wageni yamekuwa yakifurika ili kujionea wenyewe umaarufu na mvuto wa mlima huo. Lakini umaarufu wake haukuanzia mwaka huo wa 1987 kwa kuingizwa kwenye orodha ya kimataifa bali kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kwamba wafalme 72 wa enzi mbalimbali waliwahi kuitolea Mbingu sadaka kwenye mlima huo. Wasomi, washairi na watu maarufu wengine wa kale walidiriki kupanda mlima huo, kuusifu na kuuandikia makala. Mwanafikra na mwanaelimu wa kale wa China Confucius pia aliwahi kuupanda Mlima Taishan zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.
Tarehe 15 Septemba, 1990 nilipanda mpaka kileleni mwa Mlima Taishan. Kama usemi unavyosema, “kusikia si kuona”, safari hii, niliweza kujionea mwenyewe umaarufu wa mlima huo. Kwa jumla tunaweza kusema kuwa ni mlima mrefu wenye vijito safi, mabonde matulivu na misitu iliyosongamana, aidha ukiwa kwenye kilele chenye kimo cha mita 1,545 juu ya usawa wa bahari utaona kama kwamba upeo wa macho umeifanya dunia ionekane finyu sana.
Siku hiyo ndiyo Harakati ya Nne ya Upandaji Mlima Taishan ya Kimataifa na ya China Nzima ilipofanywa. Wapandaji mlima zaidi ya 600 kutoka nchi na maeneo 30 duniani walishiriki katika harakati hiyo. Mimi na baadhi ya wafanyakazi wa gazeti letu tulipata bahati ya kupiga picha ya pamoja na washindi watatu wa kwanza wa mashindano hayo kwa kundi la vijana wanaume la kimataifa ambao walitoka Columbia kwenye Kilele cha Mfalme wa Jedi ambapo ni mwisho wa mashindano hayo.
Picha hii ilipigwa pamoja na washindi watatu
Ili kurembesha na kuhifadhi mlima huo na vijito vyake, serikali ya mitaa ilijumuisha wenyeji wa huko kupanda miti mingi mlimani na kuzunguka mlima huo na kuufanya uonekane na rangi ya kijani kibichi inayomsababisha mtu asiamini kuwa ni mlima mkongwe kiasi hicho.
Pia juhudi ya kujenga vidato zaidi ya 6,000 kuanzia chini ya mlima hadi juu ili kuwawezesha wapandaji wasikatishe ovyo kwenye misitu na kuuharibu uzuri wa kimaumbile inafaa kupongezwa. Vidato hivyo vinaonekana adhimu sana kama kwamba ni ngazi moja ndefu ya kufikia mbinguni inayoning’inia angani.
Eneo la jumla la mlima huo ni zaidi ya kilomita 400 za mraba, kuna mawe mengi maarufu ya itale. Mawe ya itale yanayopatikana huko si kama ni ya aina nyingi na matumizi duni mbalimbali, bali rangi zake ni za kuvutia. Inasemekana kwamba Italia, Uholanzi, Guinea, Japani na Singapore ziliwahi kununua mawe hayo ya mlima huo kwa matumizi ya aina kwa aina.
Mnamo mwaka 1987, serikali ya mitaa iliamua kila mwaka kuanzia tarehe 14 hadi 16 Septemba kufanyike harakati za upandaji Mlima Taishan za kimataifa, katika siku hizo hujaa aina mbalimbali za maonyesho na shamrashamra za biashara na nchi nyingine. Nazo ni dalili nzuri ya kuuthamini mlima huo, kuendeleza ushirikiano na nchi za nje na kuwapa wafanyabiashara wa nchi nyingine fursa nzuri za kupanua uwanja wa biashara.
Hata hivyo ili kuuhifadhi vizuri zaidi Mlima Taishan, urithi wa kimaumbile wa binadamu wote duniani, kama alivyosema Dkt. H. Leo Teller, mwakilishi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa nchini China, kuna haja ya kuzingatia zaidi tahadhari za moto, usafi wa mazingira, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kudhibiti vyanzo vya maji na kuhifadhi maliasili za kimaumbile za huko.