Historia ya utawala wa Raisi wa Romania.
Wakati sauti za kupinga zilipoanza kusikika kote nchini kuhusu mauaji ya TimiΘoara na nani hasa aliyepaswa kulaumiwa kwayo, CeauΘescu aligundua kuwa alikuwa amefanya makosa. Siku tatu baada ya mauaji hayo, aliitisha mkutano wa hadhara huko Bucharest, ambapo aliwalaumu "waharibifu" wanaopinga Romania kwa kuchochea uasi huo. Umati wa watu haukukubaliana naye; mkutano huo, ambao ulikusudiwa kuwa wa kumuunga mkono CeauΘescu, ulibadilika ghafla na kuwa maandamano ya kumpinga, huku watu wakianza kumzomea na kumtukana dikteta huyo aliyebaki ameduwaa. Kwa kutambua kuwa alikuwa katika hatari kubwa ya kuuawa na umati wenye hasira, CeauΘescu alikimbilia ndani ya jengo la serikali lililokuwa karibu, wakati huo huo Bucharest ikitumbukia katika machafuko makubwa.
Siku iliyofuata, huku maandamano yakizuka kote nchini, mmoja wa viongozi wakuu wa jeshi la Romania, Vasile Milea, alijiua. Uvumi ulisambaa kwa kasi kubwa ndani ya jeshi kwamba kwa kweli aliuawa kwa amri ya CeauΘescu. Vikosi vya ulinzi, ambavyo hapo awali vilikuwa waaminifu kwa dikteta huyo, vilimgeuka na kujiunga na waandamanaji. Bila matumaini yoyote ya kurejesha udhibiti, na huku umati wenye hasira ukizingira jengo la bunge la Romania, CeauΘescu na mkewe Elena walitoroka kwa njia ya kusisimua kwa kupanda helikopta kutoka juu ya paa la jengo. Hata hivyo, baada ya jeshi la Romania kutishia kutungua helikopta hiyo kwa kutumia kombora, wawili hao walilazimika kutua na wakakamatwa mara moja. Kesi ya haraka iliandaliwa kwa ajili ya siku iliyofuatatarehe 25 Desemba.
Kesi dhidi ya wanandoa hao wa familia ya CeauΘescu iliendeshwa kwa haraka sana, na matokeo yake yalikuwa tayari yanajulikana kabla hata haijaanza. Walishtakiwa kwa kutenda mauaji ya kimbari huko TimiΘoara, kufuja mamilioni ya fedha katika akaunti za siri za benki, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali ya umma wakati wa mapinduzi hayo. Katika kipindi chote cha kesi hiyo, ambayo ilichukua saa moja, CeauΘescu alikataa kutambua uhalali wa mahakama hiyo. Mahakama ilimhukumu dikteta huyo na mkewe adhabu ya kifo.