Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania, Hassan Mwakinyo anashikiliwa na jeshi la Polisi mkoa wa Tanga, akituhumiwa kumshambulia mtu anayedaiwa kuingia katika eneo lake bila ridhaa yake.
Mwakinyo anashikiliwa na jeshi hilo tangu jana alhamisi katika kituo cha polisi Chumbageni kutokana na sakata hilo huku mtu aliyemshambulia akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Bombo iliyopo Tanga.
Chanzo cha kuaminika kimelieleza gazeti la Mwananchi kuwa sababu kubwa ya bondia huyo kushikiliwa na jeshi hilo ni kutokana madai ya kumshambulia mtu huyo na kumsababishia majeraha makubwa mwilini.
Mwananchi limemtafuta kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, ACP Maket Msangi amekiri pia wanamshikilia bondia huyo.
"Sisi tunamshikilia Hassan Mwakinyo hatumshikilii bondia.
Hakuna shia ila ana tuhuma za kumshambulia mtu ambaye inasemekana alipita katika maeneo ya nyumbani kwake na kujaribu kuingia kwa namna ya mazingira ambayo inadaiwa ni kwa nia ya kutenda kosa kwa hiyo akamkamata," amesema Msangi.
"Wakati tunapewa taarifa alikua amemkamata Polisi tulienda kwaajili ya kumchukua mtuhumiwa lakini alikua kidogo ana majeraha tukampeleka akapate huduma ya kwanza Bombo kwa hivyo tunamshikilia kutokana na kumkuta mtuhumiwa kidogo ana majeraha, Tunaendelea kumhoji Mwakinyo kwanini mpaka akajeruhiwa hivyo.
"Hivyo elewa kwamba tunamshikilia kwasababu hiyo tutafikisha suala hilo ofisi ya mashitaka kwaajili ya kutafsiri sheria na kama kuna tatizo ushahidi unathibitisha kosa basi hatua nyingine stahiki zitachukuliwa," alisema Msangi.