👉Mwanafunzi akiri kufanya mapenzi na mwalimu kwa hofu ya kunyanyaswa shuleni.
👉Mkakati wa kuficha tuhuma kumsaidia mwalimu wabainika- viongozi watajwa kuhusika.
👉Mzazi wa mwanafunzi amaliza siku tatu akifuatilia jeshi la polisi kuchukua hatua.
Wakati serikali na Bunge kwa pamoja wakipiga mbiu ya kukemea vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na wasichana kingono, wasichana katika shule za bweni wilayani Kibondo wako katika hatari ya kuacha masomo au kufanya vibaya kwenye masomo kutokana na walimu kuwalazimisha kufanya mapenzi!
Hivi karibuni Mwalimu Peter Mahela kutoka Shule ya Sekondari ya wasichana ya Mkugwa iliyopo halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma alishikiliwa na jeshi la polisi wilayani humo kwa tuhuma za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na baadhi ya wanafunzi shuleni hapo.
Mwalimu huyo alifikishwa polisi mara baada ya kufumaniwa na mwanafunzi (jina linahifadhiwa) wa kidato cha tano majira ya saa sita usiku wa kuamkia tarehe 11 mwezi Mei 2024, akiwa amelala nyumbani kwa mwalimu huyo.
Katika shule hiyo wapo walimu wengine wawili, mwalimu Lamech Chanda na Enock Baraka ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakituhumiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi ya mara kwa mara na wanafunzi ikiwemo kuwapa ujauzito licha ya vikao vya nidhamu kukaa mara nyingi ila bado tabia hiyo imekuwa sugu shuleni hapo.
Akizungumza na timu ya waandishi wa habari wanaochunguza tukio hilo, mkuu wa shule hiyo Martha Kajoro amesema walimu hao watatu wamekuwa na matukio hayo na kwamba wamekuwa wakileta changamoto za mara kwa mara licha ya kukosekana kwa ushahidi dhabiti.
Ametaja baadhi ya tuhuma kwa walimu hao kwa kipindi cha mwaka 2019 mpaka sasa kuwa mwalimu Peter Mahela anasadikika kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi nane, watano wa kidato cha sita na watatu wa kidato cha Tano, mwalimu Lamech Chanda anasadikia kuwa na wanafunzi wanne na mwalimu Enock Baraka kuwa na wanafunzi watatu.
Mkuu wa shule amesema baadhi ya wanafunzi waliokuwa na mahusiano ya kimapenzi na walimu hao walishika ujauzito na kufukuzwa shule huku walimu hao wakiendelea na utumishi.
“Pale ambapo tumekuwa tukihisi kuwa kuna mahusiano ya kimapenzi baina ya mwalimu na mwanafunzi tumekuwa yukiwaonya walimu waliohusika kwa mdomo na kwenye vikao vya nidhamu ili kujaribu kuondoa au kupunguza hali ile sanbamba na kutoa taarifa kwa mamlaka za utumishi na udhibiti ngazi ya wilaya lakini tabia hizo zinaendelea jambo linaloshusha hadhi ya shule" Amesema mkuu wa shule.
Akizungumzia tukio la usiku wa tarehe 10 kuamakia tarehe 11 Mei, 2024 Makamu mkuu wa shule hiyo Mwl. Silas Kaige, anakiri kushuhudia tukio hilo kwakuwa aliamshwa na na askari polisi majira ya saa sita usiku kwenda kugonga mlango kwa mwalimu Mahela ambaye aligongewa mlango na polisi hao bila mafanikio.
“Niliitwa usiku majira ya saa sita ili kumgongea mwalimu Mahela afungu mlango, kwakuwa polisi waligonga kwa zaidi ya nusu saa ila hakufungua, nadhani ni kwasababu waligonga kimya kimya, ila nilipofika mimi na kugonga huku nikitaja jina lake aliamka na kufungua mlango ndipo tuliposhuhudia akiwa na binti na kisha jeshi la polisi wakamuweka chini ya ulinzi kwa kosa hilo” Alisema Kaige.
Alisema baada ya mvutano wa muda mrefu kati ya polisi na mwalimu Mehala walifikia makubaliano ambayo yeye hakuyafahamu na akaachiwa huru huku mwanafunzi akibaki kituoni.
“Kuna matukio mengi ambayo yamekuwa ni magumu sana, bila busara ya mkuu wa shule wangekuwa wameshafukuzwa shule kwa mfano mwalimu Lamech Chanda alishakutwa na matukio kama hayo, tutamuweka chini na kumuonya, alikataa kwakuwa hatukuwa na ushahidi wa kutosha kwakuwa masula ya mapenzi huwa yanafanyika kwa usiri mkubwa” Alisema Kaige.
Amesema tabia ya walimu hao imekuwa kama mazoea na kwamba hawaheshimu tena mamlaka za shule na idara ya elimu wilayani kwakuwa wamekuwa wakiongea mara nyingi hata kwa kutumia mamlaka za juu akiwemo mkurugenzi ila bado waliendelea na tabia hizo.
Mwalimu Kaige ametaja kukosekana kwa uzio katika shule hiyo kama sababu ya baadhi ya wanafunzi kwenda kwenye nyumba za walimu na kuiomba serikali kuwajengea.
Juhudi za kumpata kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma ili kueleza hatua zinazochukuliwa dhidi ya uhalifu huo hazikufanikiwa kutokana na RPC kutopatikana, hata hivyo imeelezwa kuwa jeshi la polisi linamsaka mwalimu Mahela ambaye alitoweka muda mfupi baada ya kukamatwa na askari polisi wa kituo kidogo cha Mkugwa
Mwanafunzi huyo ambaye kwa sasa anahifadhiwa kwa siri nyumbani kwa afisa ustawi ambaye pia anatuhumiwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuficha siri hiyo, anakiri kufanya mapenzi na mwalimu wake na kwamba alikubali kufanya hivyo baada ya kutongozwa sana huku kukiwepo na ushawishi wa wanafunzi wenzake kumhimiza akubali kitendo hicho ili asibughudhiwe kwenye masomo yake.
"Nilienda kwa mwalimu wakati wanafunzi wenzangu wakiwe Prepo, na tukafanya mapenzi na mwalimu na hatukutumia kinga, ilikuwa mara yangu ya kwanza kwenda kwake, ninaomba nisamehewe, sitarudia tena kufanya kitendo hicho," anasema mwanafunzi huyo kutoka mkoani Geita anayesoma katika shule ya sekondari ya wasichana Mkugwa wilayani Kibondo.
Aidha mzazi wa mwanafunzi amekiri kupeleka mashataka hayo kituo cha polisi Kibondo ambako anataja kupewa ahadi ya kulishughulikia jambo hilo na kumrejesha mtoto katika masomo yake.
Hata hivyo anaeleza kuwa hakufurahishwa na kitendo cha mwanaye kushikiriwa na Jeshi la Polisi na kusimamishwa masomo wakati mwalimu akiachwa bila hatua za haraka, huku akiweka msimamo wa kutokubali mwanae kukosa elimu.
KAULI YA KAMANDA WA POLISI KIGOMA
JamiiForums ilipomuuliza Kamanda wa Polisi Mkoa, Filemon Makungu amesema “Ni tuhuma kuwa kuna mambo kama hayo yanaendelea, kuhusu huyo Mwalimu uchunguzi unaendelea, tukikamilisha hatua kama kuna hatua zitachukuliwa kuhusu Mwanafunzi kusimamishwa hayo ni mambo ya shule.”