kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,677
Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Selemani Isanzu Chasama (50), amefikishwa katika Mahakama ya HakimuMkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka ya kumiliki meno ya tembo vipande 347 vyenye thamani ya Sh. bilioni4.2 sawa na Dola za Marekani 216,000.
Askari huyo ambaye ni Ofisa Uvuvi wa JKT alisomewa mashtaka hayo ya uhujumu uchumi na Wakili wa Serikali,Shadrack Kimaro, mbele ya Hakimu Sundi Fimbo wa mahakama hiyo.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili Kimaro aliiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo anadaiwa kukutwa na nyara hizo Julai 4 mwaka huu maeneo ya Mbezi Makabe jijini Dar es Salaam, zenye thamani ya Sh. 4,249,080,000 kinyume cha sheria ya uhifadhi wa wanyama pori.
Hakimu Sundi alisema kuwa mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote na kesi hiyo itaenda kusikilizwa Mahakama Kuu na kama Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), atatoa kibali itasikilizwa katika Mahakama ya Kisutu.
Mshtakiwa huyo alirudishwa rumande kwa kuwa mashtaka ya uhujumu uchumi hayana dhamana na kesi hiyo litatajwa Julai 24, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE