Sheria ya ki-Islam haimpi mwanamke haki ya kutoa talaka, maoni yoyote kwamba mwanamke apasa kupewa haki ya kumtaliki mumewe yatakuwa ni kuingilia maadili ya dini, ambayo waraka umekariri kusema, sio nia ya Serikali.
Familia ni msingi wa jamii, na kama ilivyo kila jamii, huhitaji mamlaka ya mwisho kuhifadhi nidhamu na ustawi wa jamaa (wa familia). Uislamu umetoa nafasi hiyo kwa mume ambaye amepewa haki ya kutoa talaka.
Lakini mwanamke wa ki-Islamu anapasika kutoa maombi ya kuvunja ndoa au kuibadilisha yeye mwenyewe katika mazingira yafuatayo:-
- Anaweza kuomba (Khula) ambayo yaweza kukubaliwa juu yake na mume.
- Anaweza kumuomba Mujtahid (ambaye ni Kadhi katika Sheriat za Shia Ithna Asheri) kumpa talaka kama mume ametoweka, au anakataa kumtunza.
- Anaweza kuifuta ndoa kama mume ni mwenda wazimu au akawa mwenda wazimu baada ya ndoa.
- Na anaweza kuibatilisha ndoa (baada ya kupeleka suala lake kwa Mujtahid) kama mume ni *******.
Itakuwa muhimu, wakati wa kuandika hati ya rasimu, kutambua talaka iliyotolewa na Mujtahid na ubatilisho wa ndoa kwa kadiri ambavyo ndoa za Shia Ithna-Asheri zinavyohusika.
Hukumu zilizotajwa hapo juu zinauhusiano juu ya masharti ya waraka kuhusiana na mume aliyetoweka. Kutoa talaka kwa Mujtahid (au hakimu katika suala la wasio kuwa Shia Ithna Asheri au wasiokuwa Waislamu) ni sahihisho bora zaidi kuliko kudhania kwamba mume kafa (kwa madhumuni ya ndoa yake) na kudhani anaishi (kwa madhumuni mengine, pamoja na ndoa nyingine kama ipo yoyote) wakati mmoja na huo huo!
Kwa vile Waraka kwa usahihi hutambua talaka iliyotolewa na mume mwislamu kama mwisho (wa ndoa), na kuitaka mahakama kusajili talaka hiyo bila uchunguzi wowote zaidi, tunataka kusisitiza kwamba talaka kama hiyo iwe inafanya kazi kuanzia tarehe ya kutamkwa kwa utaratibu wa talaka na mume, na sio tarehe ya kusajiliwa.
source;
UTETEZI WA SHERIA ZA KIISLAMU SEHEMU YA PILI