Rugemeleza Nshala alikuwa miongoni mwa viongozi waliothibitishwa na baraza kuu, yeye akiwa
mwanasheria mkuu wa chama cha demokrasia na maendeleo (
CHADEMA) lakini pia
amewahi kuwa rais wa chama cha wanasheria Tanganyika (
TLS) mwaka 2019 hadi 2020. Vilevile Dkt. Nshala ni miongoni mwa mawakili ambao wanamsaidia Tundu Lissu anayejitetea mwenyewe katika kesi ya Uhaini inayomkabili.
Kuanzia Septemba 08 hadi Septemba 11 siku nne mfululizo Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uhaini katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam amekuwa akiwasilisha mapingamizi yake na kuitaka mahakama kuifuta kesi hiyo kwa kile alichosema kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyosikiliza kesi hiyo katika hatua za awali haikuwa na mamlaka ya kisheria.
Madai
Ipo taarifa inayosambazwa mtandaoni ikitumia utambulisho wa grafiki za Jambo TV ikieleza kuwa mwanasheria mkuu wa CHADEMA amesema Lissu amekata tamaa anaomba maridhiano
Uhalisia wa taarifa hiyo
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia utafutaji wa maneno muhimu (Key Word Search) umejiridhisha kuwa taarifa hiyo si ya kweli kwani Mara baada ya kesi kuhairishwa Septemba 11, Dkt. Nshala akizungumza na wanahabari hakutoa kauli hiyo.
Vilevile grafiki iliyotumika kusambaza taarifa hiyo ni ya kughushi kwani haijachapishwa na Jambo TV katika kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii bali imetumika na wapotoshaji kusambaza taarifa isiyo ya kweli.
Aidha
Jambo TV ilichapisha taarifa iliyomuonesha Dkt. Nshala akizungumza na waandishi wa habari ambapo alieleza namna ambavyo Lissu aliwasilisha hoja zake mahakamani.
Rejea hapa alichokizungumza Dkt. Nshala
"Tarehe 11 mwezi wa 9, 2025 Mahakama kuu masjala ndogo ya Dar es Salaam chini ya jaji Ndunguru, Kiwonde ilikusanyika kusikiliza kesi ya Uhaini dhidi ya mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, ambaye leo alikuwa akifanya mawasilisho yake ya mwisho kuhusiana na hoja ambazo zilikuwa zimewasilishwa na mawakili wa serikali na Msingi wa mawasilisho yake ni kwamba Mahakama ya hakimu mkazi wa Dar es salaam Kisutu, yale yote ambayo iliyafanya kuanzia tarehe 10, mwezi wa nne 2025 hadi tarehe 18, mwezi wa nane 2025, yalikuwa ni batili.
Yeye kupelekwa pale katika mahakama hiyo na jamhuri wakati imemshika wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma tarehe 9 mwezi wa nne ilikuwa ni makosa, sheria iko wazi kwamba mahakama ya ukabidhi inatakiwa ni ile ambayo mshtakiwa ameshikwa.
Unapokuwa umekamatwa katika wilaya fulani na kuna mahakama ya ukabidhi, inayofanya majukumu ya ukabidhi ni mahakama ya pale ambapo mtu amekuwa amekamatwa, si ambako wanafikiria kosa lilitendeka.
Sasa Mwenyekiti Tundu Lissu ameweza kuonesha kabisa kwa marejeo ya sheria, na maamuzi ya mahakama kuu na mahakama ya rufaa, ambayo yameweza kuonesha kabisa kwamba hilo ni suala ambalo halina ubishi imeweza kuwasilishwa pale na kuonesha kwamba yale yote yaliyofanywa chini ya Hakimu Mfawidhi Kiswaga na yale aliyoyaleta hapa yote ni batili, hiyo ndiyo hoja yake na ameweza kuonesha kabisa kwamba majibu ya mawakili wa serikali katika hoja hizo yalikuwa kwa sehemu kubwa yanaunga mkono hoja yake.
Na baada ya hapo ameomba kwamba, Mahakama hii kwa kutumia mamlaka yake iweze kutamka kwamba yote yaliyofanyika kule yalikuwa ni batili na madhali ni batili, na kwa kuwa hapakuwa na kosa lolote kule Mbinga na mamlaka ya Hakimu mkazi Kisutu haina mamlaka hayo, yeye basi aachwe huru aweze kurudi nyumbani kwake na kuweza kuendelea na maisha yake. Kwa hiyo angalau kesi hii itakuwa imetibu makosa mengi sana ambayo yanafanywa na waendesha mashtaka wa serikali kuhusiana na kesi za namna hiyo.
Tunaiachia mahakama iweze kutoa uamuzi, Mahakama imesema itatoa uamuzi siku ya Jumatatu, Tarehe 15 saa tatu asubuhi. Kwahiyo kazi kubwa imefanyika mwenyekiti ameweza kuonesha kwa umakini kabisa na kuwasilisha hoja kwa majaji wa mahakama kuu, basi majaji hao wamesema wanaomba wapewe muda waweze kuzitafakari hoja za pande zote mbili na mwisho wa siku wafanye maamuzi yao, Asanteni."