Mafisadi wa EPA kutajwa bungeni
- Ni kutokana na shinikizo la wananchi
- Ahadi ya Spika yasubiriwa kwa hamu
na mwandishi wetu
SHINIKIZO la wananchi la kutaka kujua watuhumiwa walioiba fedha za Mfuko wa Madeni ya Nje (EPA), limeifanya Serikali ifikie uamuzi wa kupeleka bungeni taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Vyanzo vya habari vimeidokeza MTANZANIA kwamba awali, Serikali ilikuwa na mpango wa kukiuka ahadi yake iliyotolewa bungeni, ya kuhakikisha taarifa ya uchunguzi, haifikishwi kwenye chombo hicho cha uwakilishi.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alishaahidi bungeni kwamba taarifa ya uchunguzi huo ingefikishwa na kujadiliwa bungeni.
Hata hivyo, kashfa ya kampuni hewa ya Richmond, ambayo iliibuliwa na Kamati Teule ya Bunge, ilizima kabisa mjadala wa fedha za EPA.
Habari zilizopatikana wiki hii zilisema, baada ya mjadala huo kukwepwa katika Mkutano uliopita, sasa utaibuka katika Mkutano utakaoanza mwanzoni mwa mwezi ujao.
Kulikuwa na mpango wa kulimaliza suala hili nje ya Bunge. Uamuzi huo ulitokana na kile kilichoonekana kwenye Richmond, Serikali haikuwa tayari kuona tena ikiumbuliwa.
Lakini baada ya shinikizo la wananchi, na kwa kuzingatia kuwa Serikali ilishatoa ahadi bungeni ya kujadiliwa kwa ripoti hiyo, Serikali imejikuta haina namna yoyote ya kukwepa, kimesema chanzo chetu cha habari.
Hofu ya Serikali, ambayo ilishaanza kuonyeshwa na Meghji, inatokana na ukweli kwamba ripoti ya EPA imesheheni majina ya viongozi wadogo kwa wakubwa, wafanyabiashara na watu wengine maarufu.
Tumetafakari na kuona hatuna ujanja katika suala hili, lazima suala hili lifikishwe bungeni. Lakini inawezekana isiwe kwenye Bunge la Aprili, inaweza ikawa kwenye Bunge la Bajeti.
Lakini vyovyote iwavyo, Bunge lazima lipewe taarifa kamili ya uchunguzi. Sasa ni wazi kuwa taarifa ya EPA, itapelekwa kusomwa na kuchambuliwa bungeni, kimesema chanzo chetu.
Katika Mkutano wa 10 wa Bunge uliomalizika, Spika Samuel Sitta, alikuwa mkali kuhusu ufisadi katika EPA, na akaitaka Serikali iwasilishe taarifa kamili ya uchunguzi.
Msimamo wa Spika ulitokana na taarifa isiyo ya kina, iliyowasilishwa na Meghji kwa wabunge.Waziri wa Fedha aliwasilisha bungeni mjini Dodoma, taarifa isiyo ya kina, inayofanana na iliyowahi kutolewa kwa waandishi wa habari.
Matarajio ya wabunge ni kwamba ingewasilishwa taarifa kamili ya uchunguzi, na si taarifa iliyokwishachujwa.
Baada ya Meghji kusoma taarifa hiyo, wabunge wawili walisimama wakitaka mwongozo wa Spika. Wabunge hao ni John Cheyo wa Bariadi Mashariki (UDP) na Christopher ole Sendeka (Simanjiro).
Mheshimiwa Spika naomba mwongozo wako. Kwamba taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imekwishafika katika meza yako na kama itajadiliwa kama taarifa nyingine. Na kama haijafika
itafikishwa lini ili tuweze kuijadili? Alihoji Cheyo.
Sendeka, ambaye naye alikuwa mkali dhidi ya Meghji, alisimama na kusema: Mheshimwa Spika, kwa kuwa Waziri amewasilisha summary (muhtasari) kuhusu uchunguzi wa BoT, je, itakubalika uielekeze Serikali watuletee taarifa rasmi ya ukaguzi, na si hii iliyokwishakuwa extracted (iliyochujwa) ili Bunge lichukue nafasi yake kama mhimili
ikiwezekana iwepo Kamati Teule ya Bunge
ili ukweli ubainike? Alihoji Sendeka.
Katika kutoa mwongozi, Spika alisema: Masuala haya yote (kuleta taarifa hiyo bungeni) yalikuwa katika mchakato wa mashauriano kati ya Bunge na Serikali. Wiki hii tutawapa taarifa hiyo. Pengine kwa kumbukumbu tu ni kwamba, nilikwishakubali katika Mkutano wa Tisa wa Bunge hili kuwa ripoti italetwa hapa na kujadiliwa, baada ya Mbunge Lucy Mayenga kuomba taarifa hiyo ipangiwe muda maalumu wa kujadiliwa, alisema Spika.
Aliendelea kusema: Hata kama Serikali haitataka, ombi hilo lipo live. Tutaanzia hapo
hizi ni zama za uwazi na ukweli, nadhani tutaafikiana tu, alisema Sitta, bila kufafanua zaidi wataafikiana na nani na katika jambo gani.
Julai 2, mwaka jana, Edward Lowassa, akiwa Waziri Mkuu, aliahidi kuwa ripoti ya uchunguzi wa ufisadi BoT, baada ya kukamilika itawasilishwa bungeni.
Lowassa alisema: Tumechukizwa na kushtushwa na taarifa kwamba kuna fedha zimepotea ndani ya Benki (BoT), kwa hiyo, baada ya kuchukizwa na jambo lenyewe, tumemwagiza CAG, tunamwamini ni mtu shupavu, ashirikiane na audit za kimataifa wakague benki wajue imekuwaje jambo hili kama ni kweli.
Je, ni kweli? Nani anahusika? Ni kina nani na tuchukue hatua gani ili jambo hili lisije likatokea tena kama kweli limetokea? Kwa hiyo, Serikali tumechukua hatua kabla ya kuja hapa. Baada ya taarifa hiyo kupatikana tutachukua hatua zinazopasa na Bunge hili litaarifiwa.
Rais Jakaya Kikwete aliteua timu inayoundwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Timu hiyo, hadi jana, ilikuwa imefanikiwa kuokoa Sh bilioni 64.
Source: Mtanzania