BURIANI PADRE JEAN-FRANCOIS GALTIER “MSELA WA KIJIWENI”
Mzaliwa wa nchini Ufaransa tarehe 27/06/1943 = 5, baada ya masomo yake na majiundo yake ya ukasisi alipadrishwa tarehe 21/05/1972 = 9.
Yeye alipadrishwa kuwa Padri wa Shirika la “White Fathers” na alipangiwa utume wake katika nchi ya Ufaransa, Italia, na hatimaye nchini Tanzania ambapo alidumu zaidi katika Parokia ya Manzese jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika Parokia hiyo tokana na ucheshi wake na ukaribu wake na watu hasa vijana, basi wakampachika jina la “MSELA WA KIJIWENI”.
Padre Francois Galtier atakumbukwa sana kwa mchango wake wa Kitume Jimboni Dar es Salaam, hasa kwa kufanikisha uanzishwaji wa REDIO BINAFSI ya kwanza kwa jina la REDIO TUMAINI na kuanza rasmi kurusha matangazo yake tarehe 03/02/1994.
Watangazaji wa kwanza ambao walianza kufanya kazi na Redio Tumaini mwaka huo wa 1994 ni hawa wafuatao. Martin David Kuhanga, Rose Joseph Msoka “Rose Mdami”, Evelyn Mpasha, Mpendwa Mgweno, na Joseph Mujule.
Mwaka 1995, Redio Tumaini walitoa tangazo la ajira kwa ajili ya kuongeza watangazaji ambapo katika waliojitokeza walifanikiwa kuajiriwa watangazaji watatu ambao ni Grace Kabogo, Fortunata Kasege, na Jerome Gausi.
Kwa ujumla watangazaji hao walifanya kazi nzuri kiasi cha Redio Tumaini kujizolea sifa kubwa kwa wakati ule. Kwa sasa imekua zaidi na hata jina limebadilishwa na kuwa TUMAINI MEDIA ikiwa pia ina kituo cha Televisheni.
Padre Franswaa kama ambavyo tulimtambua kwa urahisi zaidi, alikuwa na kibwagizo chake Redioni ambacho kilikuwa kinatumika kama ndio “JINGLE” ya redio. Kibwagizo kilisema “SIKILIZA REDIO TUMAINI, LAKINI USISAHU KULALA JAMANI….” Kibwagizo hicho kilikuwa kikivutia mno wasikilizaji.
Nakumbuka marehemu Bibi yangu Mzaa Baba alipokuja jijini Dar kwa ajili ya matibabu alikuwa akipenda mno kuigiza na kufurahia kibwagizo cha Padre Franswaa kila alipokuwa akikisikia.
Familia ya wafanyakazi wote wa TUMAINI MEDIA wale wa zamani na hata wa sasa nawapa pole sana kwa msiba huo wa Mwanzilishi wa Kituo hicho cha Matangazo.
BWANA ALITOA NA BWANA SASA AMETWAA! JINA LAKE LIHIMIDIWE!