SoC03 Mwarobaini Mmomonyoko wa Maadili

SoC03 Mwarobaini Mmomonyoko wa Maadili

Stories of Change - 2023 Competition
Joined
May 9, 2023
Posts
18
Reaction score
14
UTANGULIZI
Mmomonyoko wa maadili ni kutozingatiwa kwa utaratibu wa maisha unaokubalika katika taifa ambalo limejiwekea na madhara yake ni makubwa kwa jamii na hivyo kuathiri kuongezeka kwa vitendo vya ushoga, uasherati na uzinzi, wizi, ulevi, uvutaji bangi na matumizi ya dawa za kulevya ambavyo hivyo ni chukizo kwa Mungu. Kuporomoka kwa maadili katika familia na jamii kwa ujumla ni mojawapo ya sababu zinazotajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la wimbi la vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini Tanzania.

Hivyo Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inaowajibu wa kuhakikisha vitendo vya mmomonyoko wa maadili vinapatiwa ufumbuzi mahususi. Ili kuhakikisha jambo hili linapatiwa ufumbuzi ni wazi ya kwamba kuna ulazima wa kubaini changamoto zinazochochea uwepo wa changamoto hizi kama ifuatavyo;

1. Jamii kutokuwa na hofu ya Mungu ni sababu kubwa ya tatizo la mmonyoko wa maadili nchini; hali hii inatokana na muingiliano wa tamaduni za jamii mbalimbali ambayo inasababishwa na ukuaji wa maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hii imepelekea wazazi au walezi kuona fahari mtoto anavaa nguo zisizo na staha pasipo kumkemea au kumrekebisha mwishowe mtoto anaharibika kwa kukosa maadili yanayostahili ndani ya jamii. Hali hii inachochewa na utandawazi ambao sasa hivi unaleta changamoto kubwa katika suala la malezi na makuzi ya watoto wetu.

2. Wazazi kukosa nafasi ya kukaa na watoto wao kwa lengo la kusema nao kwa kuwaelekeza na kuwakemea pale wanapokuwa wakifanya mambo ambayo yanaonekana kutokuwa na maadili; watoto wengi wanalelewa na wadada au wakaka wa kazi jambo ambalo linafanya mtoto kuiga tabia ambazo zinafanana na anayemlea na iwapo mlezi wa mtoto huyo atakuwa na tabia mbaya hivyo hata kwa mtoto huyo atakuwa na tabia mbaya. Mfano Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 22 mwezi Aprili mwaka 2023 alisema kwamba wazazi ndio tatizo la mmonyoko wa maadili kwa watoto ( chanzo East Afrika Tv News)
inbound5350761410761248317.png


3. Teknolojia ya habari chanzo cha mmomonyoko wa maadili; mfano kuna maudhui ya mtandaoni, redioni, runinga, pamoja na vyombo vya habari vya magazeti yanachochea kasi ya kupolomoka kwa maadili. Pia ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo watoto na vijana wanaoiga tamaduni na desturi za jamii nyingine zinazokinzana na mila na desturi za mtanzania. (Chanzo gazeti la mwananchi la tarehe 8may 2023)
inbound9059170236807102305.png

4. Changamoto ya kiuchumi ndani ya familia kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili kwani wazazi au walezi wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi na kusahau wajibu wa kusimamia malezi na makuzi yenye maadili mema kwa watoto. Kutokana na shughuli nyingi za kufanya kwa lengo la kujipatia kipato imesababisha watoto wengi kutokupata mafundisho bora na kusababisha kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili.

NINI MWAROBAINI WA TATIZO LA MMOMONYOKO WA MAADILI NCHINI TANZANIA?
Suluhisho la tatizo hili ni uwajibikaji pamoja na utawala bora hususani kwa wizara yenye dhamana ya Kusimamia Utamaduni, sanaa na Michezo chini ya Mh. Dorothy Gwajima. Kwa kuweza kufanya jitihada zenye mabadiliko chanya katika kupambana na tatizo hili.

Zifuatazo ni baadhi ya hoja ambazo zinaweza kuchukuliwa kama ufumbuzi wa tatizo la mmonyoko wa maadili nchini Tanzania
1. Taasisi za kidini na mashirika mbalimbali yana wajibu wa kuwahamasisha wazazi na walezi kutekeleza wajibu wao wa kuwalea watoto katika maadili ya kitanzania; makundi ya viongozi wa dini, taasisi zinazotoa mafunzo kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo, wakuu wa shule, kamati ya ulinzi na usalama, waandishi wa habari, wasanii pamoja na wamiliki wa vituo vya kutoa mafunzo na kulea watoto wahakikishe wanatimiza wajibu wao kwa wakati wa kuhamasisha wazazi na walezi kutekeleza majukumu yao ya kuwalea watoto katika msingi imara ya maadili yanayostahili.

2. Kufanya mapitio ya sheria, kurekebisha sheria, kufanya maboresho ya sheria katika kulinda na kukuza maadili kwenye jamii ya taifa letu kwa mjibu wa sheria; sheria ya kanuni za Adhabu sura ya 16 licha ya kutoa adhabu kwa mtu mwenye hatia ya kufanya makosa yanayoenda kinyume na maadili bado inatakiwa kufanyiwa mapitio upya kwa kufanyiwa marekebisho na maboresho ya sheria hii ili mtu yeyote atakayepatikana na hatia katika makosa ya kimaadili aweze kupatiwa adhabu inayostahili tofauti na ilivyo sasa.

3. Jamii ishirikiane na jeshi la polisi katika kuhakikisha matukio yanaripotiwa na kufikishwa mahakamani kwa haki. Jamii yetu inakumbwa na kasumba ya uoga wa kusema au kutoa ushahidi na kuripoti matukio katika sehemu inayostahili kwa kuyakumbatia na kufikia hatua ya kumalizana wao kwa wao pasipo kuripoti watuhumiwa katika vyombo vya kisheria kwa kufanya hivyo hurudisha jitihada za serikali katika kutatua changamoto hii ya mmomonyoko wa maadili nchini Tanzania.

HITIMISHO
Ujenzi wa jamii bora, imara, yenye utu na maadili mema unaanzia ngazi ya familia kupitia malezi na makuzi mema kutoka kwa wazazi na walezi . Vijana ndio taifa la kesho hivyo ni lazima waandaliwe, kukuzwa na kujengwa katika maadili mema ili kujenga jamii bora sasa na baadaye.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom