Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimesema ratiba ya Mwenge wa Uhuru mkoani Tanga ndio ilikuwa sababu ya kuzitisha ziara yao ya Operesheni C4C iliyopangwa kufanyika katika mikoa yote nchini kwa siku 16.
Itakumbukwa Mei 21, katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CHAUMMA, Salum Mwalimu alitangaza operesheni C4C akisema itakuwa ni ya siku 16 ambazo walipanga kuzunguka mikoa yote kwa helikopta.
Operesheni hiyo ilianza Juni 3, katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, hata hivyo siku hiyo hawakutumia helikopta na Mwalimu alieleza kuwa imechelewa kutoka nchini Kenya. Kesho yake Juni 4, helkopta ilifika na walianza kuitumia katika mikutano kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mikoa waliyotembelea ni pamoja na Mwanza, Geita, Simiyu, Mara na Arusha, Kilimanjaro, Kigoma, Tabora na Katavi.
Akieleza sababu ya kusitishwa kwa operehseni hiyo leo Julai 4, Mkurugenzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Uenezi wa CHAUMMA, John Mrema amesema ratiba ya Mwenge wa uhuru ndiyo ilikuwa sababu.
“Tulisitisha ziara ya Tanga kwa sababu ya ratiba za Mwenge wa Uhuru, lakini tutaendelea siku sio nyingi,” amesema.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba Juni 15, Mwenge Wa Uhuru 2025 ulitarajiwa kupokelewa wilayani Tanga Juni 16, 2025, katika uwanja wa Shule Ya Msingi Mabambani, Kata ya Chongoleani, ukitoa Wilaya ya Mkinga na kukimbizwa katika mitaa 43 ya Jiji la Tanga.
Hata hivyo, mmoja wa maofisa wa CHAUMMA ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema sababu iliyotolewa wakati wa kusitisha ziara hiyo ni matengenezo ya helkopta.
“Walisema helkopta inarudishwa kutengenezwa, si unajua ile chopa inatakiwa kutengenezwa mara kwa mara. Halafu viongozi waliitwa kwa Msajili wa vyama vya siasa kulikuwa na kikao. Lakini siku sio nyingi operesheni C4C itarusishwa.
Juni 30, Katibu Mkuu wa CHAUMMA, Salum Mwalimu alizindua uchukuaji wa fomu za kuwania ubunge na udiwani nchini utakaokamilika ndani ya Julai.