Dk. Mwakyembe naye halipi ankara ya maji (Tanzania Daima)
na Hellen Ngoromera
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kuchunguza Mkataba wa Richmond, Dk. Harrison Mwakyembe, anatuhumiwa kulihujumu Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam na Pwani (Dawasco) kutokana na kujiunganishia maji kwa njia ya wizi.
Kutokana na tuhuma hizo, Dk. Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela (CCM), anayemiliki nyumba hiyo namba 102 iliyopo Kata ya Kunduchi Mtaa wa Kilongawima, ametozwa faini ya sh 796,272 na Dawasco.
Hayo yalibainika jana wakati wa ziara ya kuwangolea mabomba wadaiwa sugu katika maeneo ya Boko, ambayo iliandaliwa na shirika hilo. Katika operesheni hiyo wateja 11 walingolewa mabomba yao.
Kwa mujibu wa Dawasco, iwapo Dk. Mwakyembe hatolipa fedha hizo za faini, watamshtaki.
Wengine waliongolewa mabomba ni Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel ole Naiko anayedaiwa sh 791,379.60 katika nyumba yake iliyopo Bahari Beach, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Peniel Lyimo (sh 678,295), aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Edgar Maokola Majogo (sh 673,573) na Vincent Mrisho (sh 613,752).
Pamoja na hao, wadaiwa wengine sugu ni Kanisa la Tanzania Christian (TCC) lililoko Boko ambalo linadaiwa sh milioni 1.2, Abubakar Somo, sh milioni 2.4, Stamford Masulube sh milioni 1.9, Miraji Msuya sh milioni moja, Dominic Pallangyo sh 982,003 na Roger Magwaza anayedaiwa sh milioni 1.9.
Meneja Uhusiano wa Dawasco, Badra Masoud, alisema pamoja na operesheni hiyo ya kuwakatia maji wadaiwa sugu kuendelea, lakini wanasikitishwa na kitendo cha viongozi wengi wa nchi kupuuzia kulipia huduma hiyo.
Bado tunaendelea na operesheni hii, hata hivyo tunasikitishwa na kitendo cha viongozi wetu kutoitikia wito wetu wa kulipia maji, usipolipa hatutajali wewe ni nani, hatutaki kusubiri mzungu aje ndio afanye kazi hii, acheni tufanye kazi, alisema Badra.
Naye Meneja wa Dawasco eneo la Boko, Ramadhani Mtindasi, alisema wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali ikiwemo mafundi wao kutishiwa kwa silaha.
Vikwazo ni vingi, wateja wetu hawataki kutulipa hivyo kutufanya tufanye kazi katika mazingira magumu, tunawashauri watulipe ili tuwahudumie.
Eneo langu lina matatizo mengi, naweza kuwatuma wafanyakazi wangu mara nyingi kufuatilia malipo bila mafanikio, wakati mwingine nalazimika kwenda mwenyewe, alisema Mtindasi.
Aliwaomba wateja wa Dawasco kuwa na ushirikiano kwa kulipia ankara zao ili kujiepusha na usumbufu unaoweza kuupata.