Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini, Alhaj Omar Shamba, amefariki dunia ghafla Septemba 22, 2025 akiwa nyumbani kwake
Alhaj Shamba aliwahi kuhudumu kama Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017 hadi 2022, ambapo alishindwa kutetea nafasi hiyo na kuchukuliwa na Mwenyekiti wa sasa, Faraj Swai
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Moshi Mjini, Athuman Ally, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza kuwa marehemu amefariki Septemba 22, saa tano asubuhi
“Ni kweli Mzee wetu Shamba amefariki nyumbani kwake leo saa tano asubuhi. Jana alikuwa msibani na pia alihudhuria swala msikitini, lakini ghafla leo akafariki. Tutatoa taarifa zaidi baada ya kufika nyumbani kwake jioni hii,” amesema Ally
Akizungumzia msiba huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amesema chama kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mzee Shamba, hasa katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu
“Shamba alikuwa ni mtu mzuri, mchapakazi na mwenye msimamo. Kabla ya kuwa mwenyekiti, aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Njoro kwa miaka mitano na alifanya kazi kubwa kwa maendeleo ya kata hiyo,” amesema Boisafi
Chanzo: Mwananchi_official