Mwenyekiti wa bavicha amesema vyama vya upinzani vitapata katiba mpya wakiwa bungeni sio kususia uchaguzi kwenye ukurasa wake wa X (Twitter)
- Tunachokijua
- Tangu kumalizika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024 ambao ulishuhudia CCM ikishinda kwa zaidi ya 98%, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chini ya Mwenyekiti wake wa wakati huo Freeman Mbowe kiliasisi kauli ya No reforms no election kumaanisha pasipo kufanyika mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, chama hicho kitazuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Hata baada ya Tundu Lissu kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mnamo Januari 21, 2025, bado msimamo wa chama hicho hadi sasa umeendelea kuwa vilevile.
Hata hivyo, kauli hii imeshindwa kueleweka kwa watu wengi, jambo lililopelekea viongozi wa chama hicho kutoa ufafanuzi mara kadhaa. Mathalani, Lissu amesikika mara kadhaa akisema kauli yao haimaanishi kususia uchaguzi, bali watafanya jitihaha za kuzuia uchaguzi. Rejea hapa na hapa.
Je, Mahinyila ameipuuza kauli hii?
Imekuwa ni kawaida kwa binadamu kutokufanana mitazamo kwenye masuala mbalimbali, pengine hili ndilo analopitia Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), Deogratias Mahinyila ambaye andiko linalodaiwa kuwa lake limeanza kusambaa mtandaoni.
"Vyama vya siasa vya upinzani vitapata Reform na katiba Mpya kupitia uwakilishi Bungeni sio kususia uchaguzi hivyo ni wakati sahihi wa kuhamasisha wananchi kujiandikisha ili tuingie kwenye uchaguzi na wapiga kura wetu sio haya masuala ya No Reform na No Election ni Ujinga mkubwa."
JamiiCheck imechukua hatua za kufuatilia andiko hili na kubaini kuwa halijachapishwa na Deogratias Mahinyila kama inavyodaiwa. KWa kutumia utafutaji wa Maneno muhimu "Vyama vya siasa vya upinzani vitapata..." hakuna majibu yaliyopatikana kuhusisha andiko hilo na kuchapishwa na Mahinyila.
Pia, Wakili Mahinyila amenukuliwa mara kadhaa akiunga mkono hadharani msimamo huo wa chama wa no reforms no election. Mathalani, Makala ya gazeti la Mwananchi la Januari 26, 2025 linaelezea sehemu ya msimamo huu ambapo alisema kauli mbiu ya ‘No reforms, no election’ (Hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi) ni amri ya wananchi walioiweka Serikali madarakani.
JamiiCheck inakukumbusha kuwa makini na kufanya uthibitishaji wa taarifa unazokutana nazo kabla ya kuziamini na kusambaza.