Na Chacha John
Habari Mwenyekiti wangu na Rais Dk. John Magufuli, pole sana na kazi kubwa ya kuwakomboa watanzania hasa kutokana na kazi kubwa ya kuleta maendeleo makubwa katika miaka mitano ya utawala wako.
Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti, tunapenda kukueleza wasaidizi wako uliowapa majukumu katika mkoa wa Mara hasa katika wilaya ya Tarime wanafanya mambo ya ovyo na hata kushindwa kusimamia taratibu na sheria katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Kitendo ambacho wanakuwa ni sehemu ya wanamikakati ya kuchuuza na kulaghua kura kwa wajumbe ili waweze kupanga safu za wagombea ambao wako imara na wenye kuleta mafanikio kwenye jamii.
Kitendo walichofanya watendaji wa Chama hasa katika jimbo la Tarime Mjini ni fedheha kubwa hasa kwa kushiriki kusambaza fedha ili kushinikiza Jackson Kangoye ashinde ni hatari sana kwa mustakabali wa Chama.
Chama kinapaswa kuishi kwa kusimamia maadili na hata kwenda na kasi ya Rais na Mwenyekiti wa Chama, Dk. John Magufuli ambaye yuko mstari wa mbele katika kuleta maendeleo kwa jamii na kuwaondolea madhira makubwa yaliyokuwa nayo.
Uimara na ushupavu wa Rais Dk. Magufuli unapaswa kwenda sanjari na kupata wagombea sahihi kwenye majimbo. Wagombea ambao wanatanguliza mbele maslahi ya Chama na wala si maslahi binafsi kama walivyofanya Tarime Mjini kuhakikisha wanapelekea wanasiasa maslahi ambao hawana uwezo wa kuleta maendeleo kwa jamii yetu.
Mheshimiwa Rais, kilichofanyika Tarime Mjini ni jambo la hatari hasa kwa mgombea kushirikiana na watendaji kununua kura kwa kiasi cha sh. 80000 na sh. 100000 jambo ambalo ni hatari kwa mtu huyo kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kitendo hicho kinatokana na mtu huyo atatumia muda mwingi kurejesha hela yake na si kuwatumikia wananchi, kwa kuwa sasa ni wakati wa wananchi kupata watu wanaokaribia usafi wako ambao umeingia Ikulu bila ushikaji au kwa fedha ya mtu bali umeingia Ikulu kwa dhamira moja ya kuwatumikia watanzania na ndio kitu kinachoonekana sasa.
Mheshimiwa Rais, naandika barua hii ya wazi kukueleza ya kwamba kinachoendelea Tarime ni mchezo wa hatari na tunapenda kukueleza tumaini kubwa la wanachama wa CCM ni kwako katika kutupa mwelekeo kwa kuwa wewe ni kiongozi madhubuti na mwenye dira thabiti ya kuleta ya maendeleo kwa Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Rais, rushwa ndani ya mchakato wa uchaguzi na kabla ya uchaguzi ndio imeamua mshindi kwa Tarime Mjini na wala si nguvu ya hoja katika kuleta maendeleo kwa jamii ya WanaTarime.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuomba sana utuokoe na hii dhahama tuliyofanyiwa Tarime kwa fedha ndio kuonekana muamuzi wa matokeo ya kumpata mgombea na si nguvu ya hoja ambayo iwe chachu ya kupata mgombea bora wa ubunge kwa jimbo hilo la Tarime ambalo kuongozwa na upinzani inatokana na hujuma inayofanywa na watendaji wa CCM.