Lukuvi amsaka aliyelipwa fidia ya Sh30,000
Minael Msuya na Aziza Athuman - Mwananchi
SERIKALI mkoani Dar es Salaam inamtafuta mkazi wa Mbagala Kuu, Kaisi Salum aliyelalamika kupunjwa malipo ya fidia za waathirika wa mabomu baada ya kupewa Sh31,000 kwa ajili ya kuziba ufa uliotokea kwenye nyumba ambayo ujenzi wake bado haujaisha.
Mkuu wa mkoa, William Lukuvi, ambaye pia na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapa, aliliambia gazeti hili jana kuwa Kaisi aliyechukua fidia kwa ajili ya matengenezo ya nyumba namba 340, anatafutwa na polisi kujibu shutuma kwamba amepunjwa katika malipo hayo.
Kaisi alitengewa kiasi hicho baada ua nyumba yake kufanyiwa tathmini na kamati ya serikali ya maafa, lakini anadai malipo hayo ni madogo kwa kuwa hayalingani na gharama za Sh3 milioni alizotumia kujenga nyumba hiyo.
Lukuvi alisema jana kuwa uchunguzi wao umebaini kuwa nyumba hiyo ilikuwa bado iko katika hatua ya ujenzi na ilifikia kozi tano huku ufa uliosababishwa na milipuko hiyo ukionekana kuwa ni mdogo.
"Vyombo vya hahari vimeweza kupenyeza na kuipata nyumba hiyo ambayo inaonyesha kuwa na ufa mdogo ambao hata fidia aliyopewa ni kubwa kulingana na ufa ulioonekana," alisema Lukuvi akizungumzia Sh31,000 alizolipwa mkazi huyo, kiasi ambacho kinaweza kutosha kununulia takriban mifuko miwili ya saruji.
Alisema, polisi inamsaka Kaisi kwa kuwa mbali na kuishutumu serikali, alifanikiwa kuwashawishi waathirika wengine wa mabomu kugoma kuchukua fidia zao kwa madai kuwa ni ndogo.
"Mtu huyu ndiye mshawishi mkuu katika kukwamisha zoezi la kuwafidia waathirika wa mabomu kwa kuwa aliweza kuwashawishi wenzake wasichukue fedha za fidia," alisema Lukuvi.
"Huyu ni fisadi wa nchi kwa kuwa alitaka apate kiasi kikubwa cha fedha, bila kujali wenzake ambao hawana makazi ya kuishi kutokana na uharibifu uliojitokeza. Alitaka fidia itolewe kama ilivyotolewa kwa watu wa Tabata Dampo kipindi kilichopita, nyumba zao zilipobomolewa na kupewa Sh20 milioni bila kujali," alisema.
Mabomu yalilipuka kutoka ghala la silaha April 29 mwaka huu na kusababisha madhara kwa wakazi wa eneo la hilo, ikiwa ni vifo vya watu 24 askari sita na nyumba zaidi ya 9,000 kuharibiwa.
Serikali ya Tz ni kama fisi ambaye kwa ulafi wake,
anaamua kuvitafuna vitoto vyake.