Benzi alilowaibia walemavu Mengi liko wapi?
Na Manyerere kaandika hivi:
Reginald Mengi ni msafi kiasi gani?
Na Manyerere Jackton
NILIANZA kumjua Reginald Mengi, mwanzoni mwa miaka ya 1990. Siku moja, tukiwa nyumbani Msasani, alifika getini. Akazungumza na walinzi. Akaangaza huku na kule kutazama mandhari ya mahali hapo ambako ni nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ili kuona vizuri, alizunguka hadi nyuma ya kibanda cha walinzi. Akarejea mbele ofisini. Akatikisa kichwa. Kwa sauti yake ya upole, akasema, Baba wa Taifa hawezi kuishi katika mazingira kama haya. Naomba mfikishie ombi langu kwake. Nataka nimjengee fensi. Hii sengenge haifai.
Wale maofisa Usalama wa Taifa waliokuwapo, waliheshimu kauli hiyo. Wakati huo Mwalimu alikuwa Butiama. Baada ya siku chache, Mwalimu aliwasili Msasani. Mmoja wa viongozi wa Usalama akabeba msalaba wa kumweleza Mwalimu ofa aliyopewa na Mengi.
Mwalimu akabadilika. Uso ukawa mwekundu. Akatafuna midomo kama ilivyokuwa ada kwake baada ya kuguswa na jambo zito. Mwalimu akahoji, Mengi nani? Katoa wapi utajiri wa kunijengea fensi? Huyu ni (akatukana). Kama ana hela akawajengee masikini; wapo wengi wanaohitaji msaada. Sitaki kusikia upumbavu wa kunijengea fensi, kwani ameona hii fensi (ya nyaya, tena zilizochakaa) hainitoshi? Mwambieni sitaki kabisa.
Kweli, Mengi hakuonekana tena kwa Mwalimu, labda wakati wa msiba. Tangu siku hiyo, nikawa nataka kujua sababu za mtu huyu kuchukiwa na Mwalimu. Mwalimu alikuwa kiona mbali. Pengine alijua kwamba akiruhusu Mengi amjengee hiyo fensi, baadaye yangekuwa matangazo kuanzia kwenye televisheni, redio hadi magazeti anayoanzisha kama uyoga.
Mwalimu alipofoka kuhusu msaada wa Mengi, alifoka kwa sababu alijua Mengi si msafi kama anavyotaka jamii imtambue. Alijua Mengi jinsi alivyofaidi fedha kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), mali ya wananchi, lakini akawa anakwepa kulipa kwa kutumia wanasheria. Hadi leo bado Mengi anakabiliwa na utata mkubwa kuhusu mabilioni aliyokopa yeye au familia yake.
Mwaka 1996 aligombana na viongozi wa Habari Corporation Limited, iliyokuwa ikiongozwa na magwiji wa habari, kina Jenerali Ulimwengu, Johnson Mbwambo, Salva Rweyemamu, Dk. Gideon Shoo na wengine. Chanzo cha ugomvi kilitokana na kuandikwa kwamba anadaiwa mamilioni ya NBC.
Juzi, Mengi ameibuka kwenye vyombo vya habari. Akawa mlalamikaji. Akawa mwendesha mashitaka. Akawa jaji. Akatoa hukumu. Alifanya kile alichofanya kwa kigezo kwamba anapambana na mafisadi. Hivi kina Edward Sokoine, ambao ndiyo wanaoheshimika katika vita hiyo, wangetumia staili hii, nchi ingekuwaje? Mengi ni nani wa kuwahukumu wengine?
Kama ilivyotarajiwa, baada ya kubwabwaja, akawageukia wananchi. Akataka wamuunge mkono. Tena akasema anajua maisha yake yake yako hatarini! Hizi ni propaganda tu. Nani ambaye maisha yake hayako hatarini, hasa wakati huu ambao hata bajaj zinaua?
Akianzisha ugomvi, anataka wananchi wote wamuunge mkono. Wampigie makofi. Akilia, tulie naye. Akicheka, tucheke sote. Mengi anaweza kuanzisha ugomvi kisha akawataka Watanzania wote wamtetee. Akikosa biashara, basi huyo aliyemshinda kwenye biashara hiyo, ni fisadi. Atahamishia ugomvi kwenye televisheni yake.
Amegombana na kila kundi katika jamii. Amegombana kuanzia kwa maaskofu hadi kwenye kundi la Ze Comedy. Fikiria. Kama mtu anaweza kugombana hata na viongozi wa kiroho, huyo lazima atakuwa na matatizo.
Yeyote anayemwangalia vema Mengi kwenye televisheni, atagundua kuwa huyu Mtanzania mwenzetu anaelekea kuchanganyikiwa. Inawezekana kabisa akili ya leo ya Mengi si akili ile aliyokuwa nayo alipoanza harakati za kujikomboa kiuchumi. Amejisahau mno kwa kudhani kwamba wananchi wote ni wajinga.
Mengi wa leo amekuwa wa kukomoa wenzake kwa kivuli cha kupambana na mafisadi. Yeye ana usafi gani? Hivi kweli katika kundi la watoa rushwa, Mengi ataponea tundu gani? Juzi alipotaja hao anaowaita mapapa wa ufisadi, aligawa shilingi ngapi kwa kila mwanahabari? Mimi najua alitoa kiasi gani. Aseme usafi wake uko wapi?
Hakuna Mtanzania mwenye akili timamu anayeweza kujiweka nyuma katika mapambano dhidi ya ufisadi. Mara zote tumekemea na hata kuibua ufisadi katika wizara, idara na kila mahali katika jamii yetu. Ushahidi wa ushindi tulioupata upo.
Lakini vita dhidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi yetu tumeiendesha kwa misingi ya haki na kwa utu. Wapiganaji wa kweli hawawezi kutumia nafasi ya vyombo vyao vya habari, kuwadhalilisha watu wengine.
Mengi anawatukana wenzake kwa sababu anajua kwamba ana vyombo vya habari vinavyotazamwa, kusikilizwa na kusomwa na wananchi wengi-ndani na nje ya nchi. Anajua masikini hawa wenye rangi nyeupe wataonekana wa ajabu wakianzisha televisheni maalumu ya kumshughulikia Mengi.
Kama tunaweza kulaani matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi na watumishi wa Serikali, kwa nini Mengi asilaaniwe kwa matumizi mabaya ya vyombo vyake vya habari?
Hivi, tajiri Teddy Tunner, ambaye ni mmiliki wa kituo cha televisheni cha CNN, akiamua kufanya kama haya yanayofanywa na Mengi, mambo yatakuwaje? Lakini tofauti na Ulaya na Marekani, hapa Tanzania kuna kina Mengi wanaosimama na kutukana wengine, kisha wakaachwa hivi hivi. Sana sana mtukanaji eti anamweleza anayetukanwa, ukitaka nenda mahakamani.
Mengi amefika mahali amejisahau. Ameona anaweza kutumia silaha yoyote kufanikisha malengo yake anayoyajua yeye mwenyewe. Mengi anajua kwamba nchi yetu inafuata misingi ya kisheria. Tuna Mahakama, Bunge na Serikali. Kila chombo kinawajibu wake. Tuna Takukuru na vyombo vingine vingi tu. Kama ushahidi anao, kashindwa nini kuupeleka katika vyombo hivyo? Kama ameupeleka, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa, wa kulaumiwa ni mtuhumiwa au anayestahili kuwashitaki? Kwa nini mtuhumiwa atukanwe na kudhalilishwa?
Anajua fika kwamba baadhi ya watu anaowashambulia hadharani wana kesi mahakamani. Anajua kuwa Mahakama inapokuwa kwenye shughuli zake, inapaswa iheshimiwe. Ipewe wigo wa kupitia mashitaka na utetezi ili ifikie hatua ya kutoa hukumu ya haki. Je, katika mazingira ya aina hii, mazingira ya kutukanana, kubezana, kusemana ovyo, mahakama itakuwa na kazi gani?
Kama kweli Mengi alikusudia kuwataja mapapa wa rushwa, basi angewataja hata wale wenye rangi nyeusi! Kama hawa weupe wamechukua fedha, nani kawapa huko BoT. Je, BoT kuna gavana Mhindi au Mzungu? Yeye alipochukua fedha NBC, kulikuwa na mkurugenzi Mhindi au Mzungu? Je, mawaziri wanaoidhinisha, ni wa kutoka nchi gani? Hawa kwa nini asiwaunganishe? Kwa nini achague hawa wenye rangi tofauti tu?
Angewataja na kina Manyerere wenye ngozi nyeusi ili walau watu wajue kwamba anachofanya anakifanya kwa misingi ya haki. Lakini kutamka wazi kwamba hawa wenye asili ya Kiasia ndiyo watu hatari, ndiyo wanaoimaliza nchi, ni kutafuta tu kuungwa mkono na jamii ya watu masikini. Kuna Wahindi na wazungu waliofanya mambo mengi mazuri katika nchi hii. Kina Dereck Brycson, Alnoor Kassum, Amir Habib Jamal, Shamim Khan, Joan Wicken na wengine wengi.
Mengi amekuwa makini sana kutafuta sympathy kutoka jamii. Mara zote anatafuta mambo ambayo anajua akiyateremsha kwenye jamii, ataungwa mkono. Akishawaandalia chakula walemavu na watu wengine masikini, hazitopita siku nyingi, ataibua bomu.
Haya tumeyaona mwaka 1994 aliponunua ugomvi kwa nguvu kutoka kwa Watanzania wenye asili ya Kiasia, hata akafika hatua akadai kwamba kulikuwa na mpango wa kumtoa roho.
Rais wa wakati huo, Mzee Ali Hassan Mwinyi, akapata habari hizo. Mengi akapewa ulinzi wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU). Tena wengine walikuwa wakilinda kwa Mwalimu Nyerere. Wakatolewa ili wamlinde Mengi. Hakuna aliyelalamika maana Katiba ya nchi inazungumzia haki ya kila mwananchi kupewa ulinzi na hifadhi ya maisha yake.
Baadaye ikaja kubainika kuwa ugomvi ule ulitengenezwa na Mengi mwenyewe, akitaka wananchi wamwonee huruma. Hata alipokuwa akiuhadaa umma wa Watanzania kwamba matangazo ya mpira au ngumi yalikuwa yakiletwa moja kwa moja kutoka Ulaya na Marekani, akasema anasakamwa na wabaya wake. Ukweli ulikuwa kwamba badala ya matangazo yale kuwa yanatoka moja kwa moja Ulaya, yalikuwa yanatoka moja kwa moja Mikocheni!
Mengi, kama nilivyosema hapo awali, aligombana na maaskofu na wapinga matumizi ya kondomu. Yeye anajua wazi kwamba makanisa yana miiko. Hayaongozwi na utashi wa wamiliki au wenye hisa kwenye viwanda na biashara za kondomu. Akatetea kondomu hadi akaitwa nabii wa kondomu.
Bwana mkubwa huyu huyu aligombana na Wilson Masilingi baada ya kunyimwa umiliki wa hoteli ya Kilimanjaro. Hatuna hakika kama hoteli hiyo angepewa Mengi, ingekuwa na mwonekano mzuri na wa maana kama huu uliowekwa na mwekezaji aliyepewa.
Alishagombana na Shamin Khan, wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara. Mengi akawa anawanywesha watu maji ya kisima, lakini akitangaza kuwa ni ya chemchem kutoka mlimani. Waligombana wee, hadi Khan akaibuka mshindi. Maneno ya udanganyifu yakafutwa kwenye chupa za maji. Udanganyifu nao ni ufisadi.
Huyu huyu Mengi amegombana na Yusuf Manji. Amemtukana kadri alivyoweza. Akawaingiza hata baadhi ya wanasiasa mamluki ili wamtukane. Hapa naomba wasomaji watambue kuwa simtetei Manji au hao aliowabatiza kuwa ni mapapa wa ufisadi. Ninachotetea hapa ni maadili na namna ya kuwasilisha jambo. Kumparamia mtu na kuanza kumtukana kwa sababu tu mmenyanganyana michezo ya bahati na nasibu na kamari, si jambo la kiungwana.
Wiki kadhaa zilizopita alimvaa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha. Kila aliyefuatilia ugomvi ule kwa makini, alimshangaa Mengi. Mtu mzima kubishana, kutukanana na mtu mwenye hadhi ya mwanao, ni aibu.
Kutoka kwa Masha ameingia kwa wahariri kadhaa wa vyombo vya habari. Yeye kila siku anasimama kudai kwamba mafisadi wanaanzisha magazeti kumshambulia. Lakini anapuuza upande wake. Yeye kila anapokabiliana na mtu au kikundi cha watu, si ajabu tukaona gazeti maalumu kwa ajili ya kukabiliana na mtu au kundi alilokorofishana nalo.
Ni wapi ambako yeye anapata fedha safi za kuanzisha magazeti ambako wengine hawawezi kuzipata? Kuna vijana wamejiunga. Wameanzisha magazeti kwa nia njema, lakini ameingilia kati na kusema wamefadhiliwa na mafisadi.
Makala hii itazua mjadala. Nitafurahi sana mjadala huu ukiendelea. Mengi ameshapeleka uwongo hadi Ikulu akiwasingizia waandishi wa habari kwamba wameunda umoja kumchafua Rais Kikwete. Sina hakika, lakini inawezekana ndiyo mbinu yake ya kujipendekeza ili awe karibu na Rais Kikwete. Anajua hakumuunga mkono Kikwete wakati wa mchakato, sasa kufukia hayo, anafanya kila awezalo ili awe karibu naye. Lakini wenye akili wanajua hakuna kiongozi makini anaweza kufunga pingu za urafiki na Mengi. Hana uadilifu huo.
Ataibuka na kusema nimetumwa na mafisadi. Atasema nimelipwa ili nimwandike. Bora aseme uwongo huo, lakini nimeshindwa kuvumilia usanii huu anaoufanya sasa. Tumefanya kazi Habari Corporation kwa miaka mingi kabla ya kampuni hii kupata wamiliki wengine. Leo hatuwezi kukosa amani kwa sababu Mengi anatusema kwamba tumeajiriwa na mafisadi. Yeye ameuza kampuni ngapi? Siwezi kuendelea kukaa kimya na kumpa heshima haramu.
Mengi hana usafi huu ambao anataka watu waamini kuwa anao. Hana. Anapoamua kuwatukana wengine, lazima ajiridhishe kwanza kwamba yeye ni msafi. Hata Biblia inasema usikazane kukinyooshea kidole kibanzi kilicho kwenye jicho la mwenzio wakati lako lina boriti!
Lakini hatari kubwa ni hii ya kuanza kuhubiri maneno yanayoweza kuibua chuki kubwa miongoni mwa wananchi. Hakika, kwa maneno ya kusema Wahindi ndiyo waporaji wakuu wa uchumi wa nchi hii, anataka kuwaeleza wananchi kwamba sasa waanze kuwachukia. Kwa nini udhaifu wa Waafrika kuongoza nchi na kumiliki uchumi wanasukumiwa Wahindi na Wazungu? Tangu Uhuru mwaka 1961, tumekuwa na rais yeyote Mhindi au Mzungu? Udhaifu ni wetu wenyewe.
Kwa maneno yake, sijui itakuwaje Watanzania wenye asili ya Kiasia wakiharibikiwa gari Manzese au Mwanjelwa. Je, hawatashambuliwa? Je, wakishambuliwa, kitu gani kitazima mwendelezo huo? Mengi anaipeleka wapi Tanzania? Yeye amezeeka. Amekula chumvi ya kutosha. Awaache vijana wadogo nao wawe wazee kama yeye.
Mengi ni mtuhumiwa wa ufisadi kama watuhumiwa wengine. Bahati yake ni kwamba hakuchota fedha za EPA. Tofauti na hapo, ni fisadi tu hata kama si wa fedha, basi wa tabia.
Wakati sasa dunia ikiwa kwenye mtikisiko wa uchumi, Mengi yeye yuko kwenye mtikisiko wa akili. Amekosa busara! Angekuwa na busara, vita dhidi ya mafisadi angeishiriki kiungwana kama wanavyofanya wenzake.
Kama nilivyosema, huu ndiyo mwanzo wa mjadala. Kama yeye amekuwa mbele kuwasema wenzake, naye avumilie kusemwa. Kama kutukana watu wengine ni ushujaa, ipo siku naye atakutana na vichaa watakaomtukana.
Kuendelea kumnyamazia Mengi ni kuitoa rehani amani ya nchi yetu. Kumwogopa hakuwezi kusaidia kumrejesha kwenye mstari. Leo anatangaza hatari kama hii kupitia vyombo vyake vya habari, kesho kitu gani kitamzuia iwapo ataamua kutumia vyombo hivyo hivyo kutaka rais angolewe? Huyu ni hatari kama zilivyo hatari nyingine zinazoikabili nchi yetu. Wazanaki wanasema, nyambisabisa obhurweri, ekiriro kirambura. Tafsiri nitaitoa toleo lijalo.
manyerere@hotmail.com
0713 335469
Hii ni kwa Pundamilia,
Wizi ni kosa la jinai (criminal). Mwenye uwezo wa kumfikisha mwizi mahakamani na kumsomea mashtaka ni Jamhuri. Raia ukishuhudia wizi, kama anaibiwa mwenzako, au jamii au mwenyewe, huna uwezo wa kwenda kumshitaki mwizi mahakamani.
Kazi yako ni kutoa ushirikiano kwa Jamhuri (kupitia jeshi la polisi), kwa kuiambia au kutoa taarifa na kuwa tayari kutoa ushahidi mahakamni utakapoitwa kama shahidi.
Mengi ameiambia serikali, si kwa kwenda polisi. Kwa kuwa ananguvu ya vyombo vya habari ametumia nguvu hiyo kuiarifu Jamhuri kuwa kuna mwizi ameonekana ameiba na ushahidi anao.
Sasa sioni tatizo hapo ndugu pundamilia. Kuiambia polisi au kuiambia jamhuri mpaka uende mwenyewe kituo cha polisi na makaratasi? Hivi mtu huwezi kupiga simu polisi ukasema Mimi fulani niko mahali fulani nashuhudia au nimeshuhudia tukio la wizi??
Sijaona kosa la raia kusema kuwa mali ya umma imefujwa na yeye anao ushahidi!! Vyombo husika vichukue hatua na baada ya kufanya uchunguzi vije mbele na viseme ushahidi hautoshi kuwafikisha mahakamani. Halafu walituhumiwa ni juu yao kufungua kesi ya madai.
Pundamilia unaposema Mengi ilitakiwa afuate taratibu; naomba uwe wazi ni taratibu zipi hizo?
Naye Lipumba wa CUF kaingilia sakata hili -- na kama ilivyokuwa kwa mitambo ya Dowans -- amejikita upande wa mafisadi. Katika sakata la Dowans alijikuta alikamata pabaya kwani Hatimaye serikali imekacha kununua Dowans.
Huyu kiongozi wa CUf nilikuwa namheshimu sana lakini naona tayari ameharibiwa na RA kupitia kwa Jussa ambaye ni swahiba wa RA. Inasikitisha kuona Profesa hataki kukubali kwamba chama chake - CUF - kilitoka kapa huku bara (hata kiti kimoja cha ubunge hakikupata -- wala kiti cha udiwani ktk mkoa wa Dar) kutokana na mapesa waliyotumia CCM kutoka ufisadi wa EPA, radar, NSSF, ndege ya urais etc.
NILIKUWA DODOMA WAKATI WA UCHAGUZI WA UWT NA SOPHIA SIMBA ALIKUWA AKIGAWA KATI YA Sh 150,000 na 200,000 KWA WAJUMBE, JE, HUYO ANAWEZA KUPIGA VITA RUSHWAA? UNADHANI ATAWATENGA WALIOMPA FEDHA ZA KUGAWA?
Hata kama Mengi angekuwa ni ufisadi wa aina yake kama huyu Manyerere anavyodai bado TWO WRONGS DOES NOT MAKE A RIGHT. Twambie Bw Manyerere na wenzake wote wanaojaribu kufunika hao waliotajwa na Mengi na kuwa spokesperson wao je NI KWELI WATU HAWA NI MAFISADI PAPA AU NI WATU SAFI? Mbona issue yenyewe inayozungumzwa ni mafisadi wanaotafuna nchi yetu. Je watu hawa waliotajwa ni safiii? Kama Mengi naye ni fisadi basi wanaomjua wamtaje, na sio kutueleza kuwa alikopa fedha NBC akashindwa kulipa akaweka mawakili ili wamtetea asichukuliwe hatua. Sasa huo ni ufisadi? Hayo ni yale yaliyotajwa kuwa ni ufisadi wa Mbowe kukopa na kutolipa kwa wakati kisha kuweka mawakili. Labda watwambie huo ni uzembe wa kibiashara au ni mipango mibaya au hawakuwa makini walipobuni miradi yao lakini huwezi kutwambia huo ni ufisadi. Je ROSTAM na hao wenzake NI SAFI? Nakumbuka story moja nyani walipomlalamika binadamu kuwa anawaonea kwa kuwakamata kwa mitego na kuwapiga na kuwaua. Jibu la mwanadamu lilikuwa rahisi sina ugomvi na nyani ila napambana na wezi wa mahindi yangu. Bahati mbaya kila ninapoweka mtego wa kunasa wezi wa mahindi yangu nakuta walionaswa ni nyani. Sasa hata kama si wabaguzi ila kama kila mara issue za ufisadi papa zikitokea tunakuta ni kina Patel sasa tusemeje. Hawa wanacorrupt system nzima. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, Ahsanteni ndugu wana JFKatika hili mimi naungana na mtoa hoja kuwa ukimchunguza kuku hautakula nyama yake, ni kweli kila mtu anayo mapungufu ya aina fulani.hatuwezi kusema mengi ni msafi tutakuwa tunajidanganya.Lakini pamoja na kutokuwa msafi anapozungumzia swala ambalo viongozi wetu waliopewa dhamana ya kulikemea wanaliogopa yeye akajitoa mhanga hatuna budi kumshukuru,Mbona wahusika wakuu wamekaa kimya? nikosa kuwadharau watanzania kwa vigezo vya kuwafikiria kuwa hawajui mambo. Hawa watu tunaodhania hawajui wanajua mambo mengine hata Rais wanchi hayajui.kwa hiyo Manyerere mchango wako ni mzuri utufanye tupanue ulingo wa kufikiri na zaidi tusimame na watu wanaotetea masilahi ya wananchi. kuwa na vyombo vya habari si issue hata rostam anavyo tena anaweza kuwa anavitumia kwa siri jambo ambalo ni unafiki atoke wazi ajitete kukaa kimya kunaashilia mambo, Tusingefurahia viongozi wetu ambao tunawalipa kwa pesa zetu ndo wawe mstari wa mbele kushambulia wananchi kwani wao pia hawawezi kuacha serikali ichukue mkondo?Nazidi kusema siwezi kushangaa kwa sofia kuchemsha anapomsema Mengi kwa wale msiomjua fyatilieni mtamjua ni mama wa jinsi gani?.Mengine hatuyasemi hapa jamvini kwani ni mambo ya mtu binafsi,kama ambavyo Mengi si msafi ndo Sofia asivyo msafi pia pamoja na wengine wengi.
Kweli, Mengi hakuonekana tena kwa Mwalimu, labda wakati wa msiba. Tangu siku hiyo, nikawa nataka kujua sababu za mtu huyu kuchukiwa na Mwalimu.
Mwalimu alikuwa kiona mbali. Pengine alijua kwamba akiruhusu Mengi amjengee hiyo fensi, baadaye yangekuwa matangazo kuanzia kwenye televisheni, redio hadi magazeti anayoanzisha kama uyoga.
Mwalimu alipofoka kuhusu msaada wa Mengi, alifoka kwa sababu alijua Mengi si msafi kama anavyotaka jamii imtambue. Alijua Mengi jinsi alivyofaidi fedha kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), mali ya wananchi, lakini akawa anakwepa kulipa kwa kutumia wanasheria. Hadi leo bado Mengi anakabiliwa na utata mkubwa kuhusu mabilioni aliyokopa yeye au familia yake.