Chadema yawashukia wanaompinga Mengi
2009-04-30 16:58:54
Na Muhibu Said
Chama Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewabeza baadhi ya viongozi wa serikali na vyama vya siasa wanaomjadili Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, kwa kuwataja wanaotuhumiwa kwa ufisadi mkubwa nchini.
Kimesema hatua ya viongozi hao inashangaza kwa vile watu hao, ambao Mengi alisema kuwa wanatuhumiwa kuwa ni `mafisadi papa`, si wapya kutajwa kuhusika na tuhuma zinazohusu ufisadi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema, jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge wa Chama hicho, John Mrema alisema baadhi ya watuhumiwa hao, walianza kutajwa kuhusika na tuhuma za ufisadi tangu mwaka 1992, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizokwishachukuliwa dhidi yao.
Mrema alisema mwaka 1992, Tume iliyoongozwa na Robert Aila kuchunguza kashfa ya Chavda, ilimtaja Shubash Patel kuhusika na kashfa hiyo, pia Tanil Somaiya, miaka michache iliyopita alitajwa kuchunguzwa katika kashfa ya ununuzi wa rada ya serikali, lakini hadi sasa wote hawajachukuliwa hatua.
Alisema watuhumiwa wengine, ni Yusufu Manji, ambaye miaka michache iliyopita, alituhumiwa kuhusika na ufisadi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Rostam Aziz alitajwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa kupitia ushirikiano wa vyama vya upinzani Septemba 15, 2007 kuwamo katika orodha ya watuhumiwa 11 wa ufisadi nchini.
``Sasa ni lipi lake (Mengi) jipya? Sisi (Chadema) tuko pamoja na Mengi, tunataka mafisadi wote na si mapapa peke yao washughulikiwe. Tunajua CCM wananufaika vipi na watu hawa,`` alisema Mrema.
Kutokana na hali hiyo, alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba aueleze umma kwanza alikopata fedha za kampeni ya uchaguzi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kabla ya kumjadili Mengi kuhusu suala hilo.
Pia, alisema ameshangazwa na kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye huko nyuma aliwahi `kuushikia bango` ununuzi wa rada kwa madai kwamba, ndani yake kuna harufu ya rushwa, lakini leo anadai watu hao hawakukosea.
Katika hatua nyingine, Chadema jana ilitoa tamko kushutumu hatua ya baadhi ya vyombo, watu, wakiwamo wabunge kutaka kumshughulikia Dk. Slaa kwa kutaja hadharani mshahara anaopokea bungeni.
Akisoma tamko hilo jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Victor Kimesera, pamoja na mambo mengine alitaka iundwe kamati maalum ya kudumu ya kupanga na kuratibu mishahara ya wabunge badala ya kuacha suala hilo kupangwa na wabunge wenyewe.
SOURCE: NIPASHE