Bwana Mengi kumsifia Rais Kikwete kuwa mpambanaji dhidi ya ufisadi, si ujasiri, bali ni kujipendekeza kwa bei rahisi, kwa kuwa hivi sasa yuko madarakani na akishamaliza kipindi chake na kuachia wadhifa, bila shaka atamponda vilivyo, alisema Profesa Lipumba.
Kiongozi huyo wa CUF ambaye anakuwa mwanasiasa wa pili mwandamizi kutoa matamshi ya kumpinga Mengi, baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) Sophia Simba, kufanya hivyo juzi, alisema kitendo cha Mengi kuwataja watuhumiwa Wahindi watupu, kinalenga kuwajengea imani wananchi kuwa tatizo la ufisadi Tanzania limeletwa na Wahindi wachache, jambo ambalo alisema ni la hatari na lenye nia ya kupotosha.
Lipumba, mmoja wa wachumi wanaoheshimika kimataifa, alisema...Mengi anacheza karata ya ubaguzi wa rangi, kwa kuwa umma wa Watanzania utakaposikia majina hayo, unashawishika kuamini kuwa tatizo la ufisadi Tanzania limeletwa na Wahindi wachache, na kwamba hao watano wakikamatwa na kuzuia wengine wasiibuke, watakuwa wamemaliza tatizo la ufisadi nchini. Hii ni dhana potofu, na ni ya hatari sana, hasa ukizingatia kuwa baadhi ya wananchi wengi wana mashaka na uzalendo wa raia wenye asili ya Kiasia, alisema Profesa Lipumba.
Alisema kauli ya Mengi haisaidii vita dhidi ya rushwa na kwamba i nadhoofisha na kupoteza malengo kwa kuwa matatizo ya ufisadi yamesababishwa na udhaifu na ukosefu wa uongozi imara wa rais na kusababisha kuchangia kuenea kwa rushwa nchini.
Kauli ya Mengi haisaidii vita dhidi ya rushwa na kwa kweli inaidhoofisha na kupoteza malengo. Udhaifu na ukosefu wa uongozi imara wa Rais Kikwete ndiyo unaochangia kuendelea kwa rushwa, alisema Lipumba kwa kujiamini.Akitoa mifano, Lipumba alisema, iwapo Kikwete asingekuwa dhaifu, angeweza kuingilia suala la ufisadi wa EPA Agosti mwaka 2006 wakati wakaguzi wa mahesabu ya Benki Kuu, Kampuni ya Delloitte & Touch walipoibua na kutoa ushahidi kuwa Kampuni ya Kagoda Agriculture ilichota kiasi cha dola milioni 30 kwa nyaraka za kughushi.
Alisema pia kwamba, iwapo Kikwete angekuwa imara, basi angeifanyia kazi taarifa ya taasisi ya Uingereza inayochunguza ufisadi mkubwa ya SFI, ambayo katika taarifa yake ya Machi mwaka jana iliwataja kwa majina maofisa wawili wa ngazi za juu serikalini waliohusika katika kashfa ya rushwa inayohusu ununuzi wa rada ya bei ya juu ya dola milioni 40 mwaka 1999.
Awali Lipumba alisema kitendo cha serikali kuamua kubadili maamuzi ya Baraza la Mawaziri lililotaka kuchukuliwa kwa Kampuni ya CDC Globeleq, kwa ajili ya kazi ya kufua umeme wa dharura na kuipa kazi Richmond, hakiwezi kuwa kilifanywa na (aliyekuwa) Waziri Mkuu (Edward Lowassa) na (aliyekuwa) Waziri wa Nishati na Madini pasipo rais kuafiki uamuzi huo.
Mengi anatumia vita dhidi ya ufisadi katika kupanda mbegu ya ubaguzi na kwamba tukipanda mbegu za ubaguzi wa rangi tunaweza kuteleza na kuingia katika ubaguzi wa kidini na kikabila , alionya Lipumba.
Alisema kwa kuwa Mengi ameonyesha kuwa na mahusiano mazuri na rais, ingekuwa ni jambo la busara kwake kuchukua ushahidi alionao kuhusu mafisadi papa hao na kumpelekea rais na TAKUKURU, na iwapo hatua zisingechukuliwa hapo ndipo angeweza kutoa kauli za namna ile alivyofanya.