Mwl. Mbelwa Petro: Tanzania ipo moja tu kwenye uso wa dunia hivyo tuwe chonjo na kauli za patachimbika!

Mwl. Mbelwa Petro: Tanzania ipo moja tu kwenye uso wa dunia hivyo tuwe chonjo na kauli za patachimbika!

Mkweliii

Member
Joined
Apr 15, 2025
Posts
16
Reaction score
5
Waasisi wa Taifa letu la Tanzania kwa uzalendo wao walipambana kuifanya ardhi yetu kuwa hifadhi ya viumbe vyote, wenye utamaduni (binadamu) na visivyo na utamaduni (wanyama). Watanzania wa leo tunayo sababu ya kuwashukuru wazee wetu kwa kazi hiyo iliyowashinda waasisi wa mataifa mengine mengi ya Afrika na nje Afrika. Wakati nchi ya Rwanda wanakinukisha Tanzania lilikuwa kimbilio lao, wakati Burundi panachimbika

Tanzania tulibaki hifadhi bora kwao, wakati Uganda wanamwagana damu Tanzania tuliwahi kuwasaidia, wakati Kenya hapakaliki Tanzania tulikuwa tunatuma wajumbe wa kidiplomasia kuhakikisha wanatulia waendelee kujenga uchumi wao, leo pale Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hapatawaliki, hakuna raia wa DRC mwenye faida na DRC kutotawalika.

Machafuko katika nchi zote hizo yalipelekea mateso yasiyosemeka kwa wanawake na watoto wao pakifuatiwa na biashara zao kuanza kuporwa mchana na usiku, miundombinu waliyoijenga kwa kodi zao wakazibomoa wenyewe, mashamba yao wakayachoma na uhai waliopewa na Mungu wakaanza kuutamatisha wenyewe.

Machafuko katika nchi hizo hayakudondoka kama mvua, yalianza na tabia na kauli za PATACHIMBIKA!, NCHI HAITOTAWALIKA!, DAMU LAZIMA IMWAGIKE MARA TUTAKINUKISHA na kadhalika.

Waanzilishi wachache wa vurugu hizo mara nyingi wanakuwa wameshafanya 'planned escape' kwenda uhamishoni Ulaya na kuketi sebuleni wakiwa na rimoti za televisheni kubadilisha chaneli ili kuona ni wangapi wameshakufa ama wangapi wamebakwa msituni nchi walizozikimbia, rejea machafuko ya Rwanda na Burundi kama mfano wa karibu. Waanzilishi wa vita wengi wako Ufaransa na familia zao.

Wito wa kuhamasisha vuguvugu na migomo siyo tu kwamba ni hatari kwa mustakabali wa nchi, bali pia unahatarisha maisha ya watu wasio na hatia wanaoweza kujikuta katikati ya machafuko yasiyo na maana wakiwemo wanawake, watoto, wagonjwa, walemavu na wawekezaji.

Kuingia madarakani kwa Rais Samia kulichora ramani mpya ya uhuru wa kisiasa kupitia falsafa ya Mageuzi {reforms}, Maridhiano {Re-conciliation}, Ustahimilivu {resilience}, na Kujenga upya {re-build} mifumo ya nchi yetu. Kuanzia Machi 2023 mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa ikaruhusiwa tena kwa misingi ya amani. Baadhi ya wanasiasa wakiwemo wa CHADEMA wakaanza kutumia mwanya huohuo kuhubiri machafuko na vita kupitia mikutano iliyoruhusiwa kwa misingi ya amani.

Linaweza kugeuka kosa kubwa kwa serikali yetu kuendelea kuilinda mikutano ya amani inayoliandaa Taifa kwa ajili ya vita. Kitu ambacho nijuavyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekataa na haiwezi kukubali hilo.

Katika kipindi hiki ambacho Tanzania inapiga hatua kubwa katika kuimarisha demokrasia na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wanasiasa wakichagua njia za uchochezi na kuvuruga amani kwa maslahi binafsi ya kisiasa.

Katika kila taifa linalothamini demokrasia, uchaguzi huru na wa haki ndio njia sahihi ya kushindana kisiasa. Kususia uchaguzi au kujaribu kuuvuruga kupitia miito ya maandamano ni kujaribu kuzima sauti ya wananchi, ambao kwa mujibu wa Katiba, wana haki ya kuchagua viongozi wanaowataka kupitia sanduku la kura. Kitendo cha Mheshimiwa Lissu kupinga uchaguzi na kupandikiza chuki miongoni mwa wananchi kinaonesha kuwa lengo lake si kushindana kwa hoja bali kuleta taharuki na mtafaruku wa kisiasa.

Kauli za PATACHIMBIKA na DAMU ITAMWAGIKA haziwezi kutumika popote pale, hata Amerika tunakosema wamekomaa Kidemokrasia kauli hizi haziwezi kusemwa na Serikali ikanyamanza.

Tusikubali amani yetu ichezewe, na kama tunda limeoza likichelewa kujidodosha mtini tulidodoshe wenyewe. Na wanaotaraji kuharibu amani yetu tusiwasubiri waiharibu tukajialaumu.

Mwl. Mbelwa Petro,
0759886429,
Biharamulo.
 
Back
Top Bottom