Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
MY LIFE MY PURPOSE
KUMBUKUMBU ZA RAIS BENJAMIN WILLIAM MKAPA
Rais Mkapa ameandika kitabu cha historia ya maisha yake na ni historia ya Tanzania na kwa hakika ni historia inayoanza wakati wa Tanganyika.KUMBUKUMBU ZA RAIS BENJAMIN WILLIAM MKAPA
Rais Mkapa anastahili pongezi kwa kutufanyia hisani hii kwani katika maraisi wetu ni yeye peke yake ambae kachukua ujasiri wa kuandika kitabu cha maisha yake na mtu anapoandika ni kuwa amejiweka wazi kwa mahasimu wake kumshambulia na pia kwa wapenzi wake kumshangilia.
Katika uzinduzi huu wa leo wa kitabu hiki, wapenzi wa Rais Mkapa wamepata fursa ya kumuadhimisha.
Kutakua na mengi katika kitabu hiki ambayo wasomaji watategemea kuyasoma na kama ilivyoelezwa kuwa kuna sura nzima ambayo kaandika kuhusu maisha yake Ikulu na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, sura hii huenda ikawa sura iliyobeba kitabu kizima.
Rais Mkapa amemwita Mwalimu Nyerere kuwa ni ‘’mentor,’’ wake akiwa na maana ni mtu aliyemjenga na kumfanya kuwa hivi alivyo hivi leo katika uongozi.
Mwalimu ana mengi katika historia ya Tanzania kuanzia enzi ya Tanganyika na inapokuwa unasoma tawasifu ya mtu aliyekuwa karibu na Mwalimu ukijua kuwa kuna sura ambayo mtu aliyekuwa karibu na yeye amemtengea kumweleza, kasi ya msomaji kutaka kufika katika sura ile ili ajue kuna nini kilichoelezwa inakuwa kubwa.
Kama ilivyoelezwa kuwa Rais Mkapa ameandika historia ya Tanzania, lakini inajulikana kuwa historia ya Tanzania inafahamika, kitabu kinapoandikwa kugusa historia hiyo huwa kazi yake kubwa ni kufahamisha ile historia ambayo haiko hadhir kwa wengi na hili ndilo linalofanya kitabu hicho kuwa kitabu.
Kitabu huwa hakiwi kitabu kwa kuandika yale ambayo yanafahamika, kitabu huwa kitabu kwa kuja na elimu mpya ambayo haikuwa inajulikana kabla.
Kitabu hiki sina chembe ya shaka kuwa kitakuwa kimesheheni mambo makubwa ambayo hayajapata kufahamika kabla na hapa haikusudiwi mambo mepesi ya kumfanya msomaji acheke, la hasha.
Kitabu hiki bila shaka kitakuwa na mazito ya kushtua na kusikitisha ambayo Rais Mkapa amekabiliananayo wakati wa utawala wake akiwa Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu.
Hatuwezi kujidanganya tukajifanya kuwa Tanzania haina manung’uniko kutoka kwa wananchi wake na naamini Rais Mkapa haya aliyajua hata kabla hajawa rais wa Tanzania.
Rais Mkapa ameeleza kuwa katika kumbukumbu hizi zake amegusia mauaji yaliyotokea Zanzibar mwaka wa 2001 baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2000.
Wasomaji vitabu watategemea kusoma katika kitabu hiki mengi, mathalan kipi kilichofanya utawala wake ikipige marufuku kitabu cha Prof. Hamza Mustafa Njozi, ‘’Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania.’’
Nayaandika haya kwa kujua kuwa Rais Mkapa ni msomaji hasa na anapenda kusoma vitabu na bila shaka aliteseka sana na uamuzi ule.
Hiki si kitabu cha kukosa tukinunue na tukisome si kwa kupata elimu tu bali kwa kuwatia moyo viongozi wetu wanyanyue kalamu na watuandikie maisha yao.