Blue, unahitahitaji kupevuka akili. Kwa vitendo vyako huafai kuitwa mume wala kiongozi wa familia. Huwezi ukatatua matatizo kwa kupiga mkeo. Ubaya ni kwamba huwezi fahamu matokeo ya kipigo hicho. Unaweza ukafikiri umemweka mkeo mahala pake na atakuheshimu zaidi au labda atakuogopa ila hujui umepunguza pendo lake kwako kwa sehemu kubwa sana. Naomba nikupe mfano mdogo sana na labda hili litakusaidia wewe.
"Pendo la mke/mume ni sawa na sahani nyeupe. Kila unapomkosea mwenzi wako ni sawa na kuweka doa kwenye sahani hiyo. Kila doa linatofautiana na doa lililotangulia. Kuna madoa utaweza kuyatoa kwa kusafisha sahani ila kuna yale ambayo yanakomaa hata ufanye nini yanabaki kuwepo. Tatizo lingine madoa huwa yanaonekana sehemu ambayo ni safi kwenye sahani na siyo mahala ambapo doa lingine lilitangulia. Itafika mahala sahani hiyo itajaa madoa kiasi kwamba mwenye nayo ashindwe kuitumia tena. Usije ukafanya ndoa yako ijae madoa mengi hadi pale utakapohitaji upendo wa mwenza naye akakujibu , " roho yangu imejaa madoa mengi sana kutokana na matendo yako hadi nashindwa nikupende kwa kutumia sehemu gani".
Mkeo alipokukubalia uende zako club wewe hukutumia akili kumsoma amekukubalia kivipi. Ishi na mkeo kwa akili. Mpende ili akuheshimu. Piga piga itakuja kukuvunjia heshima mbele ya jamii, mkeo, familia, ndugu na hata watoto wako. Na kama una mtoto wa kiume, sijui unampa mfano gani. Na kama mkeo ana tabia mbaya ulikuwa wapi siku zote usigundue yeye siyo mke mwenye kukufaa wewe?
Mkeo alipokwambia una mwanamke nje ulipaswa umueleweshe kuwa huna ila kwa matendo yako inakuwa vigumu sana kwake kuamini huna mwanamke nje. Namalizia, "ndoa siyo lele mama"